MakalaSiasa

RONALD NGALA: Mwanasiasa wa Pwani anayeshikilia rekodi ya uzalendo hadi leo

May 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na KYEB

WAKIORODHESHWA wanasiasa ambao uwepo wao ulihisiwa pakubwa katika ukanda wa Pwani kabla na baada ya uhuru, basi jina Ronald Gideon Ngala haliwezi kamwe kukosa kwenye orodha hiyo.

Mwansiasa huyu stadi alizaliwa mwaka wa 1922 katika Kaunti ya Kilifi kisha akosemea Shule ya Msingi ya St John Kaloleni na baadaye shule za upili za Shimo la Tewa na Alliance. Baadaye alijiunga na Chuo cha Makerere nchini Uganda kusomea Stashahada katika kozi ya elimu.

Kati ya mwaka 1949 na 1954, Bw Ngala alirejea Kenya na kufundisha katika Shule ya St John na ile ya upili ya Mbale kabla ya kuhamia Taita. Kati ya mwaka wa 1955 na 1956 alihudumu kama Mwalimu Mkuu wa Shule ya upili ya Buxton mjini Mombasa.

Licha ya kuonyesha ustadi wake kwenye taaluma ya elimu, Bw Ngala alichangamkia siasa na akachaguliwa kama Mwakilishi wa Baraza Kuu la Kutetea Maslahi ya Waafrika wa Mombaasa (MCCA) ambalo lilipigania maslahi ya wenyeji wa mji huo mkubwa zaidi katika eneo la Pwani.

MCCA ilifanya kazi kwa ushirikiano na Muungano wa Waafrika kutoka Pwani (CAA) ambao ulikuwa maarufu sana eneo hilo kabla ya mwaka 1957. Hata hivyo, Bw Ngala alijiunga na Bunge la Kitaifa la Legco mwaka wa 1957 na ikawa mwanzo wa safari ya kujivumisha kisiasa sio tu katika ukanda wa Pwani bali pia katika ulingo wa kitaifa.

Hata hivyo, alijitokeza kama mwanasiasa aliyejali sana udhabiti wa taifa kuliko umaarufu wake wa kisiasa ndiposa alichaguliwa kwa urahisi kama Katibu Mkuu wa Kenya National Party (KNP) iliyobuniwa mwaka wa 1959.

Kuchaguliwa kwake katika Bunge la Legco hata hivyo hakukushangaza kwa kuwa kampeni zake zilijikita sana katika kutatua masuala yaliyowaathiri Wapwani huku wapinzani wake wakijipigia debe kuhusu masuala ya kitaifa.

Alipata kura 3,400 na kuwashinda wapinzani wake Dawson Mwanyumba na Francis Khamisi waliozoa kura 2,539 na 2,267 mtawalia ili kuteuliwa kama Mwakilishi wa Pwani kwenye Bunge la Legco.

Kutokana na umaarufu wake, jamii yake ya Mijikenda ambayo ndiyo kubwa ukanda wa Pwani ilimpa uungwaji mkono hasa katika eneo lake la kuzaliwa la Kilifi. Kiwango cha juu cha masomo yake pia kilimpa jukwaa bora la kutangamana na viongozi wa vyama vingine vya kitaifa kutoka maeneo mbalimbali mwa nchi na kumzidishia umaarufu.

Kati ya miaka ya 1956, 1957 na 1958, Bw Ngala ambaye sasa alikuwa amejizolea sifa kochokocho kama Msemaji wa Mijikenda na idadi kubwa ya Waafrika ukanda wa Pwani, alijiunga na vyama vya Kilifi African People’s Union (Kapu) na Kwale African Democratic Union (Kwadu).

Ingawa hivyo, aliwasisimua wengi alipotoa hotuba yake ya kwanza katika Bunge la Legco kwa kuwataka wazungu kubadilisha mtaala wa masomo kwa watoto Waafrika, aliosema walikuwa wamebaguliwa kwa kupata masomo duni kuliko wana wa wazungu.

Hotuba hiyo ilimsawiri Bw Ngala kama mzalendo, jambo ambalo lilimvutia uungwaji mkono kutoka kwa wawakilishi wenzake kutoka Afrika ndipo akawaongoza kwa Kongamano kuu la kwanza katika mji wa Lancaster nchini Uingereza mwaka wa 1960.

Ujumbe wa viongozi 30 waliokuwa kwenye kongamano hilo ulijumuisha Jaramogi Oginga Odinga, Arwing Kodhek, Tom Mboya, James Gichuru, Daniel Moi miongoni mwa wengine waliokuwa maarufu wakati huo.

Ili kudhihirisha umoja wao na kufanikisha vita dhidi ya mbeberu, viongozi hao walirejea nchini na kuungana kuunda Chama cha Kanu na Mabw Ngala, Kiano, Odinga, Argwings Kodhek, Mboya, Gichuru na Mungai wakawa wanachama wa kamati ya muda wa kusimamia chama hicho.

Mnamo Mei mwaka wa 1960, Kanu iliandaa uchaguzi wa wanachama wa kudumu na Bw Ngala pamoja na Daniel Arap Moi wakachaguliwa bila uwepo wao kama Mwekahazina na Naibu Mwekahazina mtawalia. Viongozi hao wawili hata hivyo walikataa nyadhifa hizo wakisema zilikuwa za hadhi ya chini na ndipo wakajiunga na kundi jingine kuunda chama cha Kenya African Democratic Union (KADU).

Katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka wa 1961, KADU ilipata pigo pale KANU ilishinda viti vingi kwenye bunge la Legco. Hata hivyo, Kanu ikiongozwa na Jaramogi Oginga Odinga ilikataa kubuni serikali ikipigania kuachiliwa kwa Mzee Jomo Kenyatta ambaye alikuwa amezuiliwa gerezani tangu mwaka wa 1953 kwa kushirikiana na kundi la Mau Mau kupigana na serikali ya mkoloni.

Kadu chini ya Bw Ngala hata hivyo kilitumia mwanya huo kuunda serikali ya pamoja na mbeberu kwa ahadi kwamba Mzee Kenyatta angewachiliwa katika kipindi cha miezi minne kilichofuata. Bw Ngala aliteuliwa Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni japo umaarufu wake ukapungua pale Mzee Kenyatta alipowachiliwa huru Agosti 1961 na akatwaa mamlaka hayo.

Chama cha Kanu kilishinda uchaguzi wa mwaka wa 1962 baada ya kupatikana kwa Katiba mpya iliyoleta mageuzi makubwa serikalini kwa matayarisho ya taifa kujinyakulia uhuru na Bw Ngala akawa Kiongozi wa Upinzani Bungeni.

Pigo zaidi lilimpata mwezi Juni 1963 Mzee Kenyatta alipoteuliwa kama Waziri Mkuu na mwaka uliofuatia 1964, Bw Ngala alimeza shubiri na kuvunja chama chake cha Kadu kisha akajiunga na Kanu.

Hata hivyo, hatua yake ya kuvunja Kadu kulimponza katika ngome yake ya Pwani baada ya wanasiasa mahiri kama Sammy Omari na Gilbert Mwatsama ambao walikuwa washirika wake kumshutumu na kusema hakushauriana na Wamijikenda kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Baada ya uhuru, Mzee Kenyatta alimteua Bw Ngala kama Waziri wa Vyama vya Akiba, Mikopo na Maslahi ya Kijamii. Ingawa miaka iliyofuatia hakuonekana sana kwenye ramani ya siasa za kitaifa, atakumbukwa daima dawamu kama aliyepigania tumia masomo na uweledi wake kupigania uhuru wa Kenya.

Hata hivyo, Bw Ngala alipigania mfumo wa utawala wa Majimbo ambao ni mfano wa serikali za ugatuzi zilizoko kwa sasa huku akipinga utawala ambao ulimpa Rais mamlaka ya juu kuliko asasi nyingine za serikali.

“Tuko imara katika imani kwamba demokrasia haifai kuwa na mipaka na uhuru wa kila raia unafaa kuheshimiwa. Kinyume na Kanu, sisi tunatoa jukwaa kwa kila kabila na kila Mkenya kuzungumzia masuala yanayowahusu bila kizuizi. Watu lazima wawe na chaguo badala ya kulazimishiwa kila jambo chini ya amri ya mtu moja,” akasema Bw Ngala mnamo mwaka wa 1962.

Ingawa alipigania majimbo, kinaya ni kwamba hakuruhusu Waarabu na Waswahili kujitawala katika ngome yake ya Pwani. Mnamo 1961 katika mkutano wa kampeni aliteremsha bendera ya Waarabu katika mji wa Malindi na kuwashutumu viongozi wa Waarabu-Waswahili Ali Abdalla na Shariff Abdalla kwa kuzua mgawanyiko Pwani.

Siasa za Bw Ngala hata hivyo zilianza kufifia 1966 alipoungana na kambi ya Bw Odinga huku Bw Mboya ambaye alikuwa akiibuka kama mpinzani wake mkuu serikalini akijiunga na kambi hasimu ya Mzee Kenyatta.

Aliendelea kuhudumu serikalini lakini hali ikawa mbaya zaidi baada ya kifo cha Bw Mboya mwaka wa 1969, ikidaiwa alikuwa akiandamwa kichinichini na utawala wa wakati huo kwa kuwa tishio kwa utawala wa Mzee Jomo Kenyatta.

Alihudumu kimyakimya hadi alipofariki mwaka wa 1972 kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Konza mjini Machakos kwenye Barabara ya Nairobi-Mombasa. Hata hivyo, wafuasi wake wameshikilia kwamba ajali hiyo ilipangwa ili kummaliza ndipo asiwe tishio kwa siasa za urithi baada ya kubainika mzee Kenyatta alikuwa akiendelea kuzeeka.

Daniel Moi alipochukua hatamu za uongozi baada ya Mzee Kenyatta kufariki mnamo mwaka wa 1978, utabiri wa Bw Ngala wa awali kwamba nchi ingeongozwa na mwanachama kutoka kilichokuwa chama cha KADU ukatimia.

Mwanawe Bw Ngala, Noah Katana Ngala ni kati ya wanasiasa wachanga waliotunukiwa nyadhifa serikalini na Mzee Moi ambaye alikuwa mwanachama mwenza wa marehemu katika chama cha Kadu.

Bw Katana Ngala alihudumu kama Waziri na mbunge hadi mwaka wa 2002 na ni kati ya wanasiasa waliokuwa waaminifu kwa Rais Mstaafu kipindi chote cha utawala wake.

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke