• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
JAMVI: Sababu kuu za pwani kulemewa kujibunia chama kimoja thabiti

JAMVI: Sababu kuu za pwani kulemewa kujibunia chama kimoja thabiti

KALUME KAZUNGU na CHARLES WASONGA

MASWALI mengi yameibuliwa kuhusu sababu ya eneo la Pwani kutokuwa na chama kimoja cha kisiasa ambacho kutaliwezesha kuwa na usemi mkubwa katika siasa za kitaifa kando na kusukuma ajenda zake serikalini.

Wadadisi wanasema kuwa ukosefu wa msemaji wa hadhi ya marehemu Ronald Ngala, Sheriff Nassir bin Taib na Karisa Maitha katika eneo hili ndio imedidimiza juhudi za kuliunganisha chini ya chama kimoja.

Kufikia uchaguzi mkuu wa 2017, pwani ilikuwa na takriban vyama sita vya kisiasa lakini ajabu ni kwamba vyama vya ODM na Jubilee, vilivyoasisiwa na watu wa bara, ndivyo viliwavutia watu wengi.

Kwa mfano katika kaunti ya Kilifi chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kilifagia viti vyote vitano, kuanzia ugavana hadi udiwani. Kwa upande mwingine chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta kilitwaa idadi kubwa ya viti katika kaunti za Lamu na Tana River.

Hii ni licha ya kuwepo kwa vyama asilia kama vile; Shirikisho, Kadu-Asili, Chama cha Majimbo na Mwangaza na Uzalendo Party of Kenya (UPK). Vingine ni; National Labour Party of Kenya (NLPK), Federal Party of Kenya (FPK) na Republican Congress (RC) kilichobuniwa na Waziri wa Utalii Najib Balala mnamo 2012.

Na hivi majuzi wanasiasa fulani wa pwani walisajili chama kipya kwa jina; Umoja Summit Political Party (USPP) katika juhudi za kufufua Kundi la Wabunge wa Pwani (CPG) na wabunge na maseneta wa eneo hilo.

Mchakato mpya wa kufufua kundi hili ambalo lilimekuwa kiliongozwa na Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori, unaongozwa na maseneta Stewart Madzayo (Kilifi) na Mohammed Faki (Mombasa).

Magavana sita wa kaunti za eneo hili pia wako mbioni kuipa uhai Jumuiya ya Kaunti za Pwani (JKP), muungano ambao unalenga kustawisha eneo hilo kiuchumi.

Utafiti uliofanywa na Jamvi la Kisiasa umebaini kuwa tatizo lingine sugu linalopelekea pwani kukosa chama thabiti cha kisiasa chenye usemi katika ngazi za mashinani na kitaifa ni jinsi wanasiasa wanavyokinzana kimawazo na hivyo kutozungumza kwa sauti moja kuhusiana na mustakabali wa siasa za eneo hilo.

Licha ya magavana Hassan Joho (Mombasa) na mwenzake wa Kilifi Amasoni Kingi kutangaza azma ya kuwania urais mnamo 2022, hawajaafikiana kuhusu nani atamuunga mwenzake mkono.

Aidha, wawili hao bado ni wanachama wa ODM na hawajaanza mikakati ya kujiondoa katika kivuli cha chama hicho na kiongozi wake Bw Odinga.

Kwa upande wake mchanganuzi wa siasa za pwani Sharif Salim Kambaa, anataja ukosefu wa uzalendo halisi na ubinafsi miongoni mwa wanasiasa wa Pwani kuwa changizo kuu ambayo inazidi kudidimiza kabisa matumaini ya jimbo hilo kuibuka na chama kimoja kitakachotetea Wapwani siku za usoni.

Bw Kambaa, ambaye ni mwenyekiti baraza la wazee Lamu anaonya kuwa ndoto ya pwani kuwa na chama kimoja shakiki huenda isitimie ikiwa wanasiasa wa sasa hawataweka kando tamaa ya uongozi na ubinafsi

“Inasikitisha kuwa wanasiasa wetu wameingiwa na ubinafsi na tamaa ya uongozi. Siasa sasa imekuwa biashara. Tuko na viongozi dhabiti kama vile Gavana wa Mombasa, Hassan Ali Joho na wenzake, Amason Kingi (Kilifi) na Salim Mvurya (Kwale), ambao wana uwezo mkubwa wa kupigania umoja wa siasa za Pwani. Lakini je? Watakaowaunga mkono ni akina nani?” anauliza.

Bw Kambaa anaongeza: “Wamesambaratika sasa, wengine wanaunga mkono Raila, wengine Naibu Rais William Ruto na vuguvugu lake la Tanga Tanga huku wengi wakisailia kwenye ua, hawajui waegemea mrengo upi. Hii ndio maana vyama vyetu vya asili ya pwani vimesahaulika au kuendela kufifia.”

Mmoja wa wanasiasa wakongwe wa Pwani ambaye amewahi kuhudumu kama Mbunge maalum katika Bunge la nne kati ya mwaka 1979 hadi 1983, Bw Omar Bwana anasema siasa za Pwani zilianza kukosa mwelekeo hasa tangu kigogo wa siasa za Pwani Ronald Ngala alipofariki.

Bw Omar pia alitaja ukosefu wa ushauri miongoni mwa wanasiasa ibuka ambao wengi ni mabarobaro wasiojua umilisi wa siasa za pwani kuwa mojawapo ya sababu ambazo Pwani inazidi kukosa mwelekeo wa kisiasa.

“Vijana wanaoingia uongozini katika dunia ya leo wamesahau wanasiasa wakongwe. Hawataki kutafuta ushauri wowote kutoka kwa wanasiasa hao wazee. Wanajihisi wamefika ilhali wanaendelea kudidimiza matumaini ya pwani kuwa na sauti moja katika siasa zake,” akasema Bw Omar.

Pia alitaja ukosefu wa kuaminiana, wivu na ukabila wa viongozi kuwa miongoni mwa vigezo vinavyopelekea Pwani kukosa msimamo dhabiti wa kisiasa.

Mbunge wa Kinango Bw Benjamin Tayari amenukuliwa katika safu hii akisema kuwa juhudi za kuwaleta pamoja unaendelea vizuri.

“Tuliketi chini na baada ya kuona kwamba Pwani inayumba kisiasa na kimaendeleo kutokana na siasa zenye migawanyiko. Ndipo tukaamua kufufua tena umoja wetu kupitia kwa kundi la CPG,” akasema Bw Tayari.

Itakumbukwa kuwa baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuridhiana kisiasa, mgawanyiko ulizuka kati ya wanasiasa wa pwani. Hii ni baada ya Naibu Rais kuanzisha kampeni kali za kujinadi kama mgombeaji urais anayefaa kuungwa mkono na wakazi wa pwani kuingia Ikulu 2022 Rais Kenyatta atakapostaafu.

Wabunge walianza kujinasihibisha na makundi mawili, maarufu kama, Kieleweke (yaani wanaounga mkono muafaka wa Raila na Kenyatta na kupinga azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu) na Tanga Tanga wanaounga mkono ndoto ya Ruto kuwa Rais 2022.

Mabw Kambaa, Omar na Tayari wanaungama kuwa mgawanyiko huu umeendelea kuathiri azma ya wanasiasa wa pwania kusema kwa sauti moja kisiasa na hata kuungani chini ya mwavuli wa chama kimoja.

Lakini kwenye mahojiana na safu hii, Bi Naomi Cidi ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama kipya cha USPP kiliasisiwa Januari mwaka huu, alikuwa mwingi wa matumaini kwamba umoja wa wapwani utafikiwa.

“Hatufai kupoteza matumaini katika mpango wetu wa kuibuka na chama kimoja kitakachosimamisha mgombea urais ifikapo uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema.

You can share this post!

JAMVI: Ukosefu wa mrithi Mlima Kenya kunavyomfaidi Ruto

Wakazi waishinikiza kaunti kukarabati barabara

adminleo