Habari

HUDUMA NAMBA: Wakenya ni wale wale tu!

May 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU
 
MAELFU ya wananchi kitaifa walisitisha shughuli zao za kawaida na wengine kukosa kupeleka watoto wao shuleni ili kujisajili kwa Huduma Namba kabla serikali ipunguze vituo vya usajili ifikapo Jumamosi.
 
Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i alikuwa ametangaza shughuli hiyo haitaongezwa muda na badala yake, watakaotaka kujisajili baada ya Jumamosi watalazimika kufanya hivyo katika afisi za machifu pekee.
 
Imekuwa kawaida kwa wananchi kusubiri hadi dakika za mwisho kutekeleza shughuli aina hii kila mara ikiwemo usajili wa wapigakura, na baadaye kuomba serikali kuwaongeza muda zaidi.
Taifa Leo Dijitali ilizuru baadhi ya vituo vya usajili katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Nakuru, Machakos na Kisumu na ifuatayo ndiyo hali halisi.
 
Katika Kaunti ya Mombasa, mamia ya wakazi walisongamana katika foleni kwenye vituo vya usajili wa Huduma Namba kutimiziwa shughuli hiyo, wengine tayari wakianza kuiomba serikali kuongeza siku za usajili.
 
‘Tumepiga foleni hapa kwa siku mbili, ikiwa tunaweza kupata muda zaidi Wakenya wengi watasaidika wasikose kusajiliwa. Ni aidha serikali iongeze siku ama iwe bunifu zaidi ama Wakenya wengi watafungiwa nje,” akasema Bi Sophia Mohamed.
 
Baadhi ya wakazi wamekuwa wakikesha katika foleni na wengine wakiamkia mapema kama saa tisa usiku, ilimradi tu wasifungiwe nje ya zoezi hilo.
 
Katika Kaunti ya Nakuru, foleni ndefu zilishuhudiwa baada ya wakazi kujitokeza kwa wingi, nayo maeneo ya usajili yakijaa watu waliofika kusajiliwa.
 
“Kufikia Jumanne takribani watu milioni 1,447, 875 walikuwa wamejitokeza na kujiandikisha na ninatumai kuwa kabla ya tarehe ya mwisho wakazi wote wa Nakuru ambao ni zaidi ya milioni mbili watakuwa wamesajiliwa,” akasema kamishna wa kaunti hiyo Erastus Mbui.
 
Alisema kuwa baadhi ya maeneo yamekuwa yakikumbwa na hitilafu za mashine za usajili kama matatizo ya mtandao.
 
Akizungumza mjini Matuu, Kaunti ya Machakos, aliyekuwa mbunge wa Yatta Francis Mwangangi naye alisihi serikali kusongesha mbele tarehe ya mwisho ya usajili, ili kuwaruhusu Wakenya wengi kuhudumiwa.
 
Bw Mwangangi alisema kuwa wakazi wengi wa maeneo kavu hawajajisajili kutokana na hali ya utovu wa usalama na kuhamahama wakitafuta lishe na maji kwa mifugo wao.
 
Katika mtaa wa Kileleshwa, Westlands Jijini Nairobi, aliyekuwa makamu wa Rais Moody Awori naye alikimbia kujisajili katika harakati hizi za dakika za mwisho, akiwataka watu wengine ambao bado hawajajisajili pia nao wafanye hivyo.
 
“Hujui wakati utahitaji kupokea huduma kutoka kwa serikali na ikiwa hujapata huduma hizo zitakuwa polepole,” akasema Bw Awori.
 
Katika Kaunti ya Kisumu, wakazi waliamkia zoezi hilo kuanzia saa tisa alfajiri pamoja na watoto wao, wakivumilia baridi kali ili tu wapate nambari hiyo ‘muhimu’.
 
“Nilikuwa hapa saa kumi na moja lakini nilipofika tayari kulikuwa na watu 300 mbele yangu na hadi sasa saa tisa bado sijasajiliwa,” akasema Bi Lorene Shidewa.
 
Wakazi wengi kaunti hiyo walilazimika kufunga biashara zao kwenda kupiga foleni, wengine peke yao na wengine na wanao, wakifanya juhudi wasifungiwe nje, hali iliyoshuhudiwa maeneo tofauti nchini.
 
PETER MBURU, WACHIRA MWANGI, PHYLIS MUSASIA, GASTONE VALUSI Na DONNA ATOLA