Griezmann akubali kugura Atletico na kutua Barcelona
Na MASHIRIKA
MADRID, Uhispania
MSHAMBULIAJI matata wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann anajiandaa kujiunga na klabu ya Barcelona kwa kitita cha Sh16.2 bilioni.
Akizungumza na waandishi kuhusu mpango huo baada ya kukutana na kocha wake Diego Simeone na afisa mkuu wa klabu hiyo, Miguel Angel, Mfaransa huyo alisema tayari ameamua kuyoyomea Camp Nou kuanza maisha mapya.
Akizungumza moja kwa moja na mashabiki wa klabu hiyo, staa huyo mwenye umri wa miaka 28 alisema, “Ningependa kuwaelezeni kwamba nimefanya uamuzi wa kuondoka na kuanza maisha mapya kwingineko. Haikuwa rahisi kutoa uamuzi huu, lakini nimeamua kuondoka. Ningependa kuwashukuru kwa kuniunga mkono kwa kipindi cha miaka mitano ambayo nimekuwa hapa, nikisaidia klabu kutwaa mataji mbalimbali. Nitaendelea kuwakumbuka kutokana na mambo mbalimbali. Ukweli ni kwamba mtazidi kuwa moyoni mwangu milele.”
Griezmann aliyezaliwa Macon, Ufaransa alijiunga na Atletico Madrid akitoka Real Sociedad, alikojifunza soka katika kituo cha kunoa vipaji vya vijana.
Tangu wakati huo, ameibukia kuwa mshambuliaji matata duniani, na alitoa mchango mkubwa kwa kuisaidia Madrid kutwaa ubingwa wa Europa League msimu wa 2017/18.
Ufaransa mabingwa wa Kombe la Dunia
Alifunga mabao mawili fainalini dhidi ya Marseille, kabla ya kuisaidia Ufaransa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2018.
Alitarajiwa kuagana na Atletico mara tu baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia, kabla ya kubadili nia yake na kuamua kuendelea kuichezea klabu hiyo ya La Liga.
Kwingineko, vigogo wa soka nchini Ufaransa, PSG wameonyesha nia ya kumsajili winga Wilfried Zaha wa Crystal Palace.
Klabu hiyo tajiri imesema iko tayari kutoa kitita cha Sh9 bilioni ili kumsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 26.
Wakati uo huo, mshambuliaji matata Gareth Bale wa Real Madrid huenda akafikiria kuhamia Uarabuni, Amerika au China ambako kuna fedha za kumtosha.
Hata hivyo, hilo litawezekana tu iwapo klabu kutoka mabara hayo itakuwa tayari kumlipa Sh52 milioni kwa wiki kama anavyolipwa na Madrid.
Kwingineko, klabu ya Wolves inafuatilia mpango wa kumsajili mshambuliaji Andre Silva wa AC Milan ambaye amekataliwa na Seville ya Uhispania alikokuwa kwa mkopo.
Seville inamrudisha Milan nyota huyo, raia wa Ureno, wakati mabingwa wa Serie A, Juventus wakiripotiwa kutenga kiasi cha Sh11.1 bilioni kuishawishi Real Madrid iwape kiungo Isco.
Hatima ya staa huyo kwa sasa haieleweki pale Bernabeu tangu klabu hiyo iingie kwenye kipindi cha mpito kufuatia kuwasili kwa kocha Zinadine Zidane.