• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
MWANAMKE MWELEDI: Mkondo wa maisha yake ulibadilika ghafla

MWANAMKE MWELEDI: Mkondo wa maisha yake ulibadilika ghafla

Na KENYA YEARBOOK

NI mmojawapo wa wanamitindo wachache kutoka Kenya ambao wamefanikiwa kupamba hafla za kimataifa za fashoni kando ya wanamitindo wa haiba ya juu kimataifa kama vile Naomi Campbell na Alek Wek.

Na katika harakati hizi Ajuma Nasenyana ameweka alama kwenye ramani ya dunia ya fashoni na uanamitindo huku mamia ya picha zake zikipamba baadhi ya majarida makuu.

Aidha ni mmojawapo wa wanamitindo wachache Waafrika kuwahi kushiriki katika hafla ya fashoni ya New York Fashion Week na kufanya kazi na baadhi ya wasanifu mavazi weledi kama vile Baby Phat na Carlos Mienes.

Isitoshe, amewahi kufanyia kazi mashirika makuu ya fashoni kama vile Ungaro jijini Milan, Italia.

Sio hayo tu, kazi yake imemzolea sifa na heshima dunini ambapo wakati mmoja katika hafla ya fashoni ya msimu wa baridi jijini Paris, msanifu wa mavazi Mwingereza Vivienne Westwood alimteua kuongoza wanamitindo kwenye shoo yake.

Si hayo tu, Agosti mwaka wa 2005, alipigiwa kura na jarida la Complex la Amerika, kumtambua miongoni mwa wanawake warembo zaidi duniani. Na mwaka wa 2012, alitajwa kama mwanamitindo bora wa mwaka na jarida la African Fashion Week.

Mzawa wa eneo la Lodwar, Kaunti ya Turkana, safari yake katika tasnia ya uanamitindo ilianza pindi baada ya kukamilisha masomo ya upili katika shule ya Greenacres and Greensteds International Schools.

Akiwa shuleni alijulikana kwa mwendo na tabia zake za kiume, vilevile werevu na ujasiri wake uliomfanya kuimarika katika riadha. Baada ya shule alianza kufanya mafunzo katika mbio za mita 400 na 800 ambapo mwaka wa 2002 alishinda katika majaribio ya kitaifa ya mbio za chipukizi za dunia na kumaliza wa tatu.

Baadaye alishiriki katika mashindano ya urembo ya Miss Tourism ya mwaka wa 2003 na kushinda taji la Miss Nairobi.

Ni hapa alinasa jicho la Lyndsey McIntyre wa shirika la Surazuri Modelling Agency, aliyevutiwa na kimo vile vile umbo la mwili wake.

Na baadaye kampuni ya uanamitindo ya Gamma Photo Agency ilipozuru nchini Kenya kuangazia kuhusu kazi yake McIntyre kama mtafuta vipaji vya uanamitindo, walifurahishwa na Nasenyana na wakapanga mkutano naye katika uwanja wa ndege alipokuwa akijiandaa kuondokaa nchini kuelekea Uswidi.

Walimshawishi kurejea Lodwar kwa kikao cha upigaji picha ambapo baadaye, hadithi yake ilichapishwa kwenye jarida la Ufaransa la Gala.

Picha hizo zilipigwa na kuwa jalada kabla ya kuwasilishwa kwa Ford Models, shirika la kimataifa la uanamitindo lenye makao yake Amerika, ambapo baadaye lilimuingiza katika shindano la Ford’s Supermodel of the World Competition.

Mwaka uliofuatia katika fainali za mashindano, Nasenyana alishinda tuzo ya Dola 50,000 na kuandikisha historia kwa kuwa mwanamitindo wa kwanza mweusi kushinda shindano la kimataifa ambalo halikuwa linaangazia wanamitindo weusi pekee.

Mwaka uo huo alishinda Euro 6,000 kwa kupigiwa kura ya kuwa mwanamitindo bora wa wiki katika hafla ya fashoni ya Spanish Fashion Week.

Chini ya mwongozo wa McIntyre, baadaye alisajiliwa na mashirika ya uanamitindo nchini Uingereza, Austria, Italia, Uhispania, Ireland, Canada na Uswidi.

Msemaji

Mbali na uanamitindo, amehudumu kama msemaji wa wanamitindo weusi ambao wamekumbana na ubaguzi katika sekta hii.

Amekuwa akikosoa ushawishi wa vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi hasa kwa kuchapisha matangazo yanayoonekana kuwapa mfichuo zaidi wanawake weupe.

Mwaka wa 2013, Nasenyana aliungana na City Models Paris kuzindua shirika la kimataifa la kusaka wanamitindo barani, huku nia ikiwa kuwapa wanamitindo wa Kiafrika, mfichuo wa kimataifa.

Pia, ni mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa City Models Africa jijini Nairobi, shirika linaloangazia wanamitindo wa matangazo ya kibiashara, badala ya fashoni hasa ikizingatiwa kwamba sekta ya uanamitindo nchini ingali mbichi.

Aidha, amekuwa akipaza sauti dhidi ya uchubuaji ngozi ambapo ameonyesha nia ya kuzindua vipodozi vya wanawake weusi, huku akitarajia kwamba bidhaa zake zitawahimiza watu wa asili ya Kiafrika, kukumbatia rangi ya ngozi zao.

“Viwango vya urembo vya Ulaya hutia shinikizo kwa wanawake weusi kwa jumla, na kuchangia ongezeko la visa vya uchubuaji ngozi, suala ambalo limekithiri nchini Kenya,” aeleza.

Mbali na kazi yake kama mwanamitindo, Nasenyana pia ameigiza katika filamu To Catch a Dream.

Kadhalika ni mjumbe wa hisani wa wakfu wa The Afya Kenya Foundation, unaosaidia wakazi wa mashambani kufikia huduma ya afya kuzuia vifo na mimba za mapema. Pia ni mwanzilishi wa wakfu wa Ajuma Nasenyana Foundation, unaonuia kuimarisha afya ya uzazi nchini.

You can share this post!

Msisimko Ingwe na Gor zikionana tena debi ya KPL

UMBEA: Upendo hauna husuda na huwa hauhesabu mabaya

adminleo