• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Kenya yang’aa mbio za mita 3,000 Shanghai Diamond League

Kenya yang’aa mbio za mita 3,000 Shanghai Diamond League

BEATRICE Chepkoech na Celliphine Chespol wamefagia nafasi mbili za kwanza za mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji za duru ya pili ya Riadha za Diamond League mjini Shanghai, Jumapili.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia Chepkoech, ambaye alikuwa akitetea taji la Shanghai, alikamilisha kuruka viunzi 28, na maji mara saba kwa dakika 9:04.53.

Bingwa huyu wa Bara Afrika, ambaye anajivunia rekodi ya dunia ya dakika 8:44.32, alifuatwa na mshindi wa Riadha za Dunia za Under-20 wa mita 3,000 kuruka viunzi na maji Chespol (9:11.10) naye Mganda Peruth Chemtai akafunga mduara wa tatu-bora (9:17.78).

Wakenya wengine katika kitengo hiki Mercy Chepkurui na Fancy Cherono walimaliza katika nafasi za tano na nane mtawalia, huku Caroline Tuigong akisalimu amri mapema.

Kwa jumla, ziara ya Shanghai ilikuwa mbaya kwa Kenya kwani Mkenya wa kwanza katika mbio za mita 5,000 za wanaume Nicholas Kimeli alimaliza katika nafasi ya sita, Winny Chebet akawa Mkenya wa kwanza katika mbio za mita 1,500 katika nafasi ya saba naye bingwa wa Afrika katika urushaji wa mkuki Julius ‘YouTube man’ Yego akashikilia nafasi ya saba katika fani yake baada ya kuandikisha mtupo wa mita 77.82.

Riadha za Diamond League hujumuisha duru 14.

Duru ya kwanza ilikuwa jijini Doha nchini Qatar mnamo Mei 3.

Jiji la Stockholm nchini Uswidi litaandaa duru ijayo hapo Mei 30.

You can share this post!

MAPISHI: Keki ya karoti

Matiang’i aongoza sherehe ya kumuaga Boinnet

adminleo