• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Lionesses yaimarisha maandalizi kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia

Lionesses yaimarisha maandalizi kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa raga ya wachezaji saba kila upande barani Afrika, Kenya wameimarisha matayarisho, huku wakiwa na matumaini makubwa watakuwa timu ya kwanza kutoka bara hili kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande mwaka 2021.

Akizungumza jijini Nairobi, Meneja wa Lionesses, Camilyne Oyuayo amesema, “Bila shaka tutafuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa sababu tuna timu nzuri.”

Lionesses imekuwa ikifanya mazoezi kila siku ya Jumatatu, Jumatano na Ijumaa asubuhi katika uwanja wa RFUEA jijini Nairobi.

Huenda ikajipima nguvu dhidi ya majirani Uganda katika Kombe la Elgon hapo Juni 22 mjini Kisumu kujiandalia mchujo wa Afrika.

Ili kupata tiketi ya kuwa nchini New Zealand kwa kombe hilo la mataifa 12, Kenya lazima ishinde Afrika Kusini, ambayo ndiyo tishio kubwa, Madagascar na Uganda katika mchujo wa Afrika utakaoandaliwa uwanjani Bosman mjini Johannesburg mnamo Agosti 9-17, 2019.

Afrika Kusini ni mabingwa wa Afrika wa raga ya wachezaji saba kila upande wa mwaka 2008, 2013, 2014, 2015, 2016 na 2017. Uganda ilipoteza katika fainali dhidi ya Afrika Kusini mwaka 2008 na Kenya mwaka 2018.

Timu itakayoshinda mchujo huu wa Bara Afrika itaingia moja kwa moja katika Kombe la Dunia litakalofanyika Julai 28 hadi Agosti 14 mwaka 2021 ikileta pamoja mataifa 12. Nambari mbili barani Afrika atapata fursa nyingine ya kufuzu kwa kukutana na timu kutoka Amerika Kusini ili kuingia mchujo wa mwisho utakaohusisha pia nambari mbili kutoka Bara Asia, Ulaya na Oceania.

Kufikia sasa, mataifa saba tayari yameshafuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2021. Mataifa hayo ni New Zealand, Uingereza, Ufaransa, Marekani, Canada, Australia na Wales zilizomaliza Kombe la Dunia lililopita katika nafasi sita za kwanza mwaka 2017. New Zealand ilichapa Uingereza 41-32 katika fainali katika nchi ya Jamhuri ya Ireland.

Ratiba ya mchujo wa Afrika

Agosti 9 – Madagascar na Kenya, Afrika Kusini na Uganda;

Agosti 13 – Kenya na Uganda, Madagascar na Afrika Kusini;

Agosti 17 – Madagascar na Uganda, Afrika Kusini na Kenya.

You can share this post!

ODM yamtetea Raila kuhusu sakata ya dhahabu

Mbunge ndani kwa kumzaba kofi kamanda wa polisi

adminleo