Makala

DINI: Tunavyogawa zaidi ndivyo tupatavyo zaidi, hatufilisiki kwa kuwa wakarimu

May 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

Ukarimu ni mtihani. “Tunatengeneza riziki kwa kile tunachopata, lakini tunatengeneza maisha kwa kile tunachotoa,” alisema hayati Winston Churchill aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Ukarimu unapozungumziwa kuna ambao wanajiweka upande wa kutoa na kuna ambao kila mara wanajiweka upande wa kupokea tu. Mtume Paulo anatuasa, “Kila mmoja, basi na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa (2 Wakorintho 9: 7).”

Tuna watu duniani ambao ukarimu ni kama jina lao la katikati. Tanzania imempoteza siku za karibuni mtu wa namna hiyo katika nafsi ya Dkt Reginald Abraham Mengi. Huyu ni mmiliki wa ITV, East Africa na Capital Televishions, magazeti ya Nipashe na The Guardian kutaja machache.

Mengi alitoa mengi, ukarimu ni kama jina lake la katikati. Sifa zake tatu ni utatu: Mfanyabiashara mwenye kuthubutu, Mtoaji anayemiliki kwa kutoa, Mwanaharakati wa kijamii aliyeyapa sura mambo mengi katika jamii. Mungu alianika, kifo kimeanua. Apumzike kwa amani. Amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia watu wa dini mbalimbali na watu wenye ulemavu.

Wakati kuna baadhi ya watu ambao hufikiria watapungukiwa kwa kutoa, Dkt Reginald Abraham Mengi alikuwa na mawazo tofauti.

Aliandika hivi katika kitabu chake, I can, I Must, I Will: The Spirit of Success, “Ninachokipata ni kutokana na mapenzi ya Mungu.

Hii ndio sababu wazo la kufilisika kwa sababu ya kutoa halijawahi kutokea kwangu. Nawezaje kufilisika wakati vyote nilivyo navyo ni mali ya Mungu? (Uk. 231). Maneno haya ya Dkt Reginald Mengi na maisha yake kwa ujumla katika kusaidia watu yanatufundisha mambo muhimu matano.

Kwanza huwezi kufilisika kwa kutoa. Mtu anaweza kufilisika si kwa sababu anatoa bali kwa sababu hatoi. Asiyepoteza haokoti. Anayekatalia kitu muda mfupi hatakuwa na cha kukatalia. Kusema kweli tunapanuka kwa kutoa. Ni kama shimo kadiri linavyotoa udongo ndivyo linazidi kupanuka.

Pili, tunazidisha kwa kugawana. Leonard Nimoy alisema, “Muujiza ni huu: tunavyogawana zaidi tunakuwa na zaidi.” “Binadamu ni kama shimo: kadiri unavyochukua zaidi kutoka kwake ndivyo anavyopata kuwa mkubwa. Ukubwa upo katika msingi wa kutoa, si kupata,” alisema Richard C. Jalverson.

Tatu, jambo gumu kutoa ni wema utakurudia. Tunabakiza jina zuri. Tunabakiza wema. Tunabakiza rekodi nzuri. Tunabakiza somo la kutoa. Tunabakiza baraka. “Tutakapoaga dunia msitufatute katika makaburi yenye malumalu na chokaa safi, bali tutafute katika mioyo ya watu tuliowatumikia,” alisema Ibn Battuta wa Morocco (1304-1368) mfanyabiashara na mwanafalsafa.

Hayati Reginald Mengi ingawa ameaga dunia anaishi katika mioyo ya watu. Amebakiza jina zuri. Unapowatumikia watu kwa upendo wote unabaki katika mioyo yao. Unapomnyunyizia marashi mtu matone yanakudondokea. “Tunachojifanyia kinakufa pamoja nasi. Tunachowafanyia wengine na dunia kinabaki na kinadumu daima,” alisema Albert Pine.

Nne, kutoa ni moyo. Moyo wa binadamu haupimwi kwa ukubwa wa pochi bali kwa ukubwa wa moyo wenyewe. Kutoa ni moyo vidole huachia. Tunazungumzia moyo usiofungwa, uliowazi. Gereza baya sana litakuwa moyo uliofungwa.

Moyo uliojaa uchoyo ni moyo uliofungwa. Kilijochaa hufurika. Moyo ukijaa ukarimu, ukarimu utafurika. Tano, ni jaza ujazwe. Dkt Mengi alipoandika “Ninachokipata ni kutokana na mapenzi ya Mungu.” Ndani ya maneno haya tunaisoma falsafa ya jaza ujazwe. Mpe Mungu kwa mkono wako akurudishie kwa mkono wake, kumbuka mkono wake ni mkubwa.

Changamoto kwa matajiri ni kuishi kwa moyo wa shukrani na mikono wazi kwa wengine. Ndugu msomaji usiseme wewe si tajiri. Hakuna maskini ambaye hana cha kutoa. Hakuna tajiri kiasi cha kutopokea chochote.