• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mashabiki wa Ingwe waikejeli timu yao baada ya kung’olewa kucha na Gor

Mashabiki wa Ingwe waikejeli timu yao baada ya kung’olewa kucha na Gor

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa AFC Leopards wanadai gozi la ‘Mashemeji’ dhidi ya mahasimu wao wa tangu jadi Gor Mahia limeisha ladha baada ya timu yao almaarufu Ingwe kubwagwa 3-1 uwanjani Kasarani, Jumapili.

Mvamizi Nicholas Kipkirui ameongoza maangamizi haya baada ya kumwaga kipa Ezekiel Owade mara mbili na kuchangia pasi iliyozalisha bao la tatu lililofungwa na Mrwanda Jacques Tuyisenge.

“Gozi limepoteza maana,” alisema shabiki Alfie Benedict Abur. Naye Davy Baba Samuel alisema kwamba ni aibu kubwa katika historia ya Ingwe kuendelea kuchapwa. Kichapo hiki ni cha nne mfululizo Leopards imepokea kutoka kwa Gor kwenye ligi.

Shabiki mwingine Amwayi Walter ametaka benchi lote la Leopards litimuliwe. “Benchi lote la Leopards linastahili kujiuzulu. Hakuna kitu tunajivunia kuwa nalo,” alisema.

Mechi ilianza kwa kasi, huku Gor ikionekana juu kimchezo mapema kabla ya Ingwe kuanza kuona mipira. Hata hivyo, krosi hatari za Gor kutoka nje ya kisanduku cha Ingwe zilitatiza vijana wa Casa Mbungo ambao waliadhibiwa na Kipkurui dakika ya 24 baada ya Owade kutema krosi ya kiungo matata Francis Kahata.

Kipkirui alifanya mambo kuwa 2-0 dakika ya 60 kabla ya kuchangia shuti lililofungwa na Tuyisenge kupitia kichwa chake Owade alipotema mpira wa juu kwenye mwamba dakika ya 64.

Leopards itajilaumu kutopata mabao zaidi zikiwemo Vincent Oburu na Brian Marita waliopoteza nafasi nzuri.

Hata hivyo, pasi mbovu kutoka kwa beki wa Gor, Joash Onyango kwa kipa wake Fredrick Odhiambo liliipa Ingwe nafasi ya kujifariji na bao safi kutoka kwa Oburu aliyepinduka vyema ndani ya kisanduku na kuvuta shuti kali kupitia mguu wake wa kushoto hadi wavuni dakika ya 87.

Ushindi unaweka Gor katika nafasi nzuri ya kutawazwa mabingwa kwa mara ya 18 katika mechi yao ijayo hapo Mei 22 dhidi ya Vihiga United inayoning’inia pabaya kuteremka Ligi ya Supa.

Gor ina alama 69 kutokana na mechi 31 kwenye ligi hii ya klabu 18. Nambari mbili Bandari imevuna alama 61 kutokana na idadi sawa ya mechi. Bandari imechabanga Zoo 3-0 na kuepushia Leopards aibu ya kufanyia Gor gwaride la heshima.

Vikosi vya ‘Mashemeji Derby’: AFC Leopards: Wachezaji 11 wa kwanza – Owade Ezekiel, Kayumba Soter, Kipyegon Isaac, Abdalla Salim, Oruchum Christopher, Ochieng David, Said Tsuma, Isuza Whyvonne, Marita Brian, Were Paul, Oburu Vincent; Wachezaji wa akiba – Bakame Eric, Sikhayi Dennis, Shami Kibwana, Mukangula Eugene, Kamura Robinson, Saad Mousa, Wayi Yeka.

Gor Mahia: Wachezaji 11 wa kwanza – Frederick Odhiambo, Philemon Otieno, Geoffrey Ochieng, Joash Onyango, Haron Shakava, Ernest Wendo, Francis Kahata, Kenneth Muguna, Jacques Tuyisenge, Samuel Onyango, Nicholas Kipkirui; Wachezaji wa akiba – Boniface Oluoch, Joachim Oluoch, Charles Momanyi, Boniface Omondi, Juma Lawrence, Francis Mustafa, Erisa Ssekisambu.

You can share this post!

Mkewe Gideon Moi akataa kazi ya serikali

Kenya yaifundisha Rwanda voliboli

adminleo