• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Obiri atamba Great Manchester Run

Obiri atamba Great Manchester Run

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Mkenya Hellen Obiri anazidi kutesa katika riadha baada ya kushinda mbio za kilomita 10 za Simplyhealth Great Manchester Run nchini Uingereza, Jumapili.

Malkia huyu wa dunia wa mbio za mita 5,000 ambaye alitwaa taji la dunia la Mbio za Nyika nchini Denmark mwezi Machi mwaka 2019 pamoja na kunyakua taji la duru ya kwanza ya Riadha za Diamond League nchini Qatar mapema mwezi huu wa Mei, amekata utepe kwa dakika 31:23.

Alimaliza sekunde 20 mbele ya Muethiopia Ruti Aga (31:44) naye Mkenya Edna Kiplagat akafunga mduara wa tatu-bora (32:34).

Obiri ni mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kushinda mbio hizi za Manchester katika kipindi cha miaka minne.

Kinadada wengine kutoka Kenya waliowahi kutamba jijini Manchester ni Vivian Cheruiyot mwaka 2009, Linet Masai (2012) na Betsy Saina (2015).

Wakenya waliowahi kushinda taji la wanaume jijini humu ni Paul Tergat mwaka 2003 mbio hizi zilipokuwa zikisherehekea kuanzishwa kwake nao Micah Kogo na Stephen Sambu wakashinda mwaka 2007 na 2015, mtawalia.

Malkia wa zamani wa mbio za kilomita 42 duniani Kiplagat alichaguliwa katika timu ya Kenya ya marathon itakayoshiriki Riadha za Dunia jijini Doha nchini Qatar kutoka Septemba 28 hadi Oktoba 6, 2019.

Obiri analenga kupeperusha bendera ya Kenya katika riadha hizo za dunia kwenye mbio za mita 5,000 na mita 10, 000.

Katika za Manchester za mwaka 2019 zilizovutia wakimbiaji 30, 000, nafasi tatu za kwanza katika kitengo cha wanaume zilitwaliwa na Mganda Jacob Kiplimo (dakika 27:31) nao Mwitaliano Eyob Faniel (28:24) na Mhispania Antonio Abadia (28:39) wakafunga tatu-bora.

You can share this post!

Kenya yaifundisha Rwanda voliboli

Mkenya matatani kwa kuwaua wanawake 11 Amerika

adminleo