Handisheki imewazima wanaharakati, walikuwa wakimtegemea Raila – Wasomi
Na PETER MBURU
WASOMI na viongozi wa nyanja zingine wamedai kuwa mashirika ya kutetea haki nchini yamekosa nguvu baada ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuanza kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.
Wakizungumza mawazo yao katika kikao cha kujadili nafasi ya mashirika ya uanaharakati tangu muafaka wa Rais na Bw Odinga mnamo Machi 2018, viongozi na wasomi walisema kuwa mashirika yalikuwa yamezoea kubebwa na upinzani badala ya kujijenga yenyewe, na hivyo wakati upinzani uliamua kushirikiana na serikali yakabaki kama yatima.
Vilevile, wataalam hao walisema kuwa hali ya viongozi wa mashirika hayo kuwa na tamaa ya kupata pesa za ufadhili kutoka mashirika ya kimataifa badala ya kutetea wanyonge ilisababisha Wakenya kukosa imani nao, ndiposa kwa sasa hata yakiandaa maandamano hakuna anayejitokeza.
Kikao hicho cha muungano wa mashirika ya kijamii kwa jina ‘Uwazi Consortium’ kiliandaliwa Jumatatu, aliyekuwa naibu spika wa bunge Farah Maalim, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki Afrika Mashariki Joy Mdivo, Prof Macharia Munene wa chuo kikuu cha USIU na Dkt Duncan Ojwang wa Chuo Kikuu cha Africa Nazarene, wakiongoza mazungumzo.
“Mashirika ya kijamii yalikuwa yakibebwa na upinzani, ndiposa muafaka iliyamaliza kabisa. Yalidhani kuwa yana nguvu lakini sasa yamejua yalikuwa kama nyani anayebebwa na mamba kuvuka mto,” akasema Dkt Ojwang.
Bi Mdivo alisema hali ya mashirika hayo kukosa uhuru wa kujiamulia wanachotaka kwa sababu ya tamaa ya pesa za ufadhili imechangia pakubwa kwa hali yao kujimaliza.
“Hatukuwa na mashirika ya kijamii yenye msimamo ila yalikuwa tu ya kupaza sauti kuhusu mawazo ya watu fulani. Sharti yaanze kujijenga kutoka chini sasa na yalenge kuleta mabadiliko wala si kufurahisha mtu,” Prof Munene naye akasema.