Michezo

Juve yakanusha inammezea Sarri

May 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

UONGOZI wa Mabingwa wa Serie A Juventus umekanusha habari zinazodai kwamba wanavizia huduma za kocha wa Chelsea Maurizio Sarri ili kurithi nafasi ya Massimiliano Allegri ambaye ataagana nao kufikia mwisho wa msimu wa 2018/19 Jumapili Mei 26.

Naibu Rais wa Juventus Pavel Nedved amepuuzilia mbali habari hizo akisema hawana haraka ya kumtafuta mrithi wa Allegri na watachunguza na kufanya udadisi wa ndani kabla ya kuteua kocha mpya.

Kocha wa zamani wa Chelsea Antonio Conte, mkufunzi wa Lazio Simone Inzaghi, meneja wa Tottenham Mauricio Pochettino na mkufunzi wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps ni baadhi ya makocha wanaotajwa kuwa wenye uwezo wa kujaza pengo la Allegri.

“Kumchagua kocha mpya si rahisi. Tunajua ufanisi wa Allegri hauwezi kurudiwa na ndiyo maana itakuwa vigumu sana kupata mrithi atakayetimiza makubwa aliyoyafanya. Kwa sasa hatujafikia uamuzi wowote kuhusu kocha mpya na hatuma haraka kufikia uamuzi huo,” akasema Nedved.

Allegri ataondoka Juve baada ya kushinda mataji matano ya Serie A na kutinga fainali mbili za Klabu Bingwa Barani Uropa (Uefa).

“Klabu ililazimika kufikia uamuzi na tunamshukuru sana Allegri kwa ufanisi aliouleta Juventus. Kocha huyu alishinda mataji 11 na kutimiza malengo tuliyomwekea kama uongozi wa Juventus. Mlinzi wetu Andrea Barzagli ambaye pia hatakuwa nasi msimu kesho amefanyia klabu hii mengi kisoka na tunamtakia kila la kheri,” akaongeza Nedved.