SWAGG: Don Cheadle
Na THOMAS MATIKO
DONALD Frank Cheadle Jr ‘Don Cheadle’ ni kati ya waigizaji wanaoaminika sana katika ulimwengu wa filamu.
Don mwenye umri wa miaka 54 ametokea kwenye filamu kibao katika tasnia ya uigizaji ambayo amekuwepo kwa zaidi ya miongo miwili.
Kipaji chake ndio chanzo cha maisha yake bomba anayoishi.
Ni kati ya waigizaji wanaolamba mkwanja mnene kutokana na kipaji chao.
Pochi
Utajiri wake unakadiriwa kufikia dola 35 milioni.
Mkwanja wake wote umetokana na kazi yake kwenye ulimwengu wa filamu.
Kule Hollywood jina lake ni kubwa na amehusishwa katika filamu kibao huku ya hivi punde ikiwa ni Avengers: End Game ambayo tayari imeshatengeneza zaidi ya dola 1 bilioni sokoni ndani ya miezi miwili toka ilipoachiwa.
Sanaa
Don alizaliwa kule Marekani. Lakini sio tu mwigizaji, pia ni produsa wa filamu na mwelekezi vilevile.
Alijipatia umaarufu wake katika miaka ya tisini.
Haikuwa rahisi kwake kutoka hadi 1987 alipotokea kwenye filamu yake ya kwanza Hamburger Hill. Japo filamu hiyo ilifanya vizuri, haikumtangaza sana.
Filamu zake zilizofuatia Devil in a Blue Dress (1995), Rosewood (1997) na Boogie Nights (1997) zikachangia kulisukuma jina lake zaidi. Baadaye alitokea kwenye Ocean Eleven (2001) mojawapo ya filamu kubwa miaka hiyo na hapo umaarufu wake ukazidi. Pia alitokea kwenye Ocean Twelve na Ocean 13.
Umaarufu wake ulikoleza hata zaidi na kupenya hadi Barani Afrika alipoigiza kama mhusika mkuu katika filamu ya Hotel Rwanda (2004) iliyotoa kumbukumbu ya mauaji ya halaiki yaliyotokea nchini humo baada ya makabila mawili makubwa Hutu ana Tutsi kugeukiana. Filamu hiyo ilimwezesha kupata uteuzi wake wa kwanza wa kuwania tuzo za Oscars.
Toka 2010 mpaka leo, Don katokea katika misururu yote ya filamu za Marvel kuanzia Iron Man 2 (2010), Iron Man 3 (2013), Avengers: Age of Ultron (2015), Captain America: Civil War (2016), Avengers Infinity War (2018) na Avengers: Endgame (2019).
Maisha yake yote, yameishi kuwa katika uigizaji. Alianza kupenda kuigiza toka akiwa kidato na baada ya kufuzu 1982 alijiunga na Taasisi ya Sanaa ya California alikofuzu na Shahada ya Usanifu wa Sanaa.
Baadaye alianza kusaka kazi kwa kushiriki kwenye maigizo ya ukumbini kisha televisheni kabla ya kupata mwanya na kupenyeza Hollywood.
Mjengo
Don anamiliki mjengo wa kifahari katika mtaa wa Oxford Avenue, Venice uliopo California.
Jumba hilo alilinunua kwa dola 894,000 (Sh90 milioni) miaka mitano iliyopita. Jumba hilo ni la orofa mbili na limejengwa kwenye eneo la ukubwa wa futi 2,400 mraba.
Usafiri
Anamiliki magari kadhaa ya kifahari likiwemo Audi Q7 alilonunua kwa dola 40,000 (Sh4 milioni) na Jaguar XJ lenye thamani ya dola 75,000.
Swagg
Don anapenda kuvaa vizuri na akiamua kupiga pamba akiambatanisha na mazagazaga mengine, utakubali.
Moja kati ya virembesho vyake vya thamani ni saa zake za mkononi. Anamiliki Jules Audemars aliyoinunua kwa dola 42,000, Classic Audermars piguet 46,000, Patek Philippe Nautilus dola 200,000 na Maurice Lacroix Masterpiece Fylback dola 4,000.
Familia
Don amekuwa katika ndoa na mke wake Bridgid Coulter kwa miaka 27, toka 1992. Katika kipindi hicho wamejaliwa watoto wawili. Walikutana wakati wa uandaaji wa filamu ya Rosewood 1992.