Sabina Chege alenga sheria za kuwapa kina mama wanyonyeshao faragha muhimu
Na MWANGI MUIRURI
UMESHAWAHI kuwazia shida kuu ambayo huwakumba kina mama wanyonyeshao wakati wako katika miji yenye shughuli nyingi na mtoto ndiye huyo analia akitaka haki yake ya maziwa?
Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Murang’a Bi Sabina Chege sasa anaandaa mswada bungeni wa kuzitaka serikali za Kaunti kuimarisha heshima ya kina mama hao ambapo zitashinikizwa kutenga maeneo spesheli ya kuwanyonyesha watoto wao.
“Hizi picha za kina mama wakitembea kwa mitaa wakiwa wametoa matiti nje wakinyonyesha watoto wao ni kudunisha usiri na heshima za kina mama. Tunataka wanawake hawa wawe wakitulia mahali, wananyonyesha watoto hao, wanawabadilisha nguo ikiwa wamejichafua na hatimaye wanarejelea safari zao au shughuli zao,” anasema Bi Chege.
Ni wazo ambalo linaungwa kwa dhati na mbunge wa Taveta, Bi Naomi Shaban ambaye anasema kuwa wanawake hao huhangaika si haba wakati wako safarini ambapo wakitaka kunyonyesha, kubadilisha mavazi ya watoto wao au hata kujikamua maziwa wanapokazwa nayo, ni lazima wajifiche nyuma ya maduka au waingie kwa vyoo vya umma
Alisema kuwa mtindo huo huwageuza kina mama hao kuwa sawa na wahaini katika miji mbalimbali ya hapa nchini wakiwa safarini.
Bi Chege anasema kuwa mswada huo ukiwa sheria, serikali za Kaunti zitahitajika kujenga vibanda spesheli katika maeneo yanayoafikika kwa urahisi na yenye usalama kuwafaa kinamama hao.
Bi Chege alisema kuwa huo ni mtindo wa kisasa ambapo afisi nyingi zimetengea kina mama maeneo spesheli ya kutekelezea majukumu hayo pasipo kujitwika aibu ndogondogo za kuanika matiti yao hadharani.
“Mswada huo utalenga kuimarisha heshima ya kina mama waliojifungua. Utapata kuwa wanawake hao huhangaika si haba wakati wako safarini ambapo wakitaka kunyonyesha, kubadilisha mavazi ya watoto wao au hata kujikamua maziwa wanapokazwa nayo, ni lazima wajifiche nyuma ya maduka au waingie kwa vyoo vya umma,” akasema.
Alisema kuwa sawa na jinsi wavutaji sigara huwa wametengewa maeneo yao, hali hiyo ndiyo itakayodumishwa kwa kina mama hao.
“Tunataka serikali iwe ya kwanza kutekeleza haki hiyo kwa kina mama wetu. Hatutaki hii tabia ya kuonekana kama wahaini katika safari zetu. Mama akihitaji kumtandika mwanawe nepi, atakuwa anaingia katika kibanda hicho na kufanya hivyo kwa raha zake. Akitaka kunyonyesha, atakuwa anajiunga na wenzake wengine katika vibanda hivyo na kutekeleza jukumu hilo,” akasema.
Alisema kuwa kuna wengine ambao kwa sababu kadha za kikazi au za kiafya huwa hawana nafasi au ruhusa ya kunyonyesha watoto wao wachanga.
“Katika hali hiyo, kina mama hao hubidika kujikamua maziwa kutoka matiti yao ili kujiepusha na mwasho au kuchomwa na maziwa hayo. Bila vibanda hivyo, mama huyo atahangaika mji mzima akisaka nafasi mwafaka ya kutekelezea wajibu huo,” akasema.
Alisema kuwa mswada huo utatua bungeni hivi karibuni akiwa na wingi wa matumaini kuwa utaungwa mkono na wengi na hatimaye uishie kuidhinishwa kuwa sheria.
“Ningetaka kuwaomba wanaume waheshimiwa katika bunge waniunge mkono katika mpango huu. Aidha, ukiidhinishwa kuwa sheria, natarajia kuwa watakaotwikwa wajibu wa kujenga vibanda hivyo watautekeleza kwa haraka iwezekanavyo,” akasema.
Alisema kuwa hadhi ya kina mama ni muhimu sana kutunzwa kwa kuwa ndio wanaobeba mbegu, kuitunza na hatimaye kuizaa na kuilea ili kuhakikishia jamii vizazi vya kesho.
“Mojawapo wa mbiu za kuwaonyesha heshima wanawake ni kuwapa fursa ya kutekeleza majukumu ya uzazi katika mazingara ya heshima. Hilo ndilo tu ninakimbizana nalo katika mswada huo wangu,” akasema.