Michezo

PIGO: Pigo Arsenal ikikosa Mkhitaryan

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

ARSENAL imepata pigo kubwa baada ya kubainika kuwa haitakuwa na kiungo wake stadi, Henrikh Mkhitaryan katika kikosi kitakachovaana na Chelsea kwenye fainali ya Europa League nchini Azerbaijan.

Hii ni baada ya Arsenal kutangaza kwamba imemuondoa kikosini kwa kuzingatia usalama wake kutokana na uhasama kati ya nchi yake ya Armenia na Azerbaijan.

Tofauti hizo za muda mrefu zimepelekea Arsenal kuamua kutomjumuisha staa huyo kwenye kikosi kitakachosafiri Jumatano ijayo kwa fainali hiyo itakayochezewa mjini Baku.

Taarifa ya Arsenal ilisoma: “Tunasikitika sana kuwatangazieni kwamba Henrikh Mkhitaryana hatasafiri na kikosi cha kwenda Baku kucheza fainali ya Europa League dhidi ya Chelsea.

“Tumejaribu tuwezavyo kumjumuisha, lakini tumepingwa vikali na taifa lake pamoja na jamii yake ndipo tukuaamua kumwacha nyuma. Tumeandika barua kwa Uefa kuelezea masikitiko yetu kuhusu hali hii. Micki amekuwa na mchango mkubwa kikosini hadi tukatinga fainali, hivyo kukosekana kwake ni pigo kuu kwa timu hii.”

“Tunamsikitikia pia kama mchezaji kwa kukosa fainali ya hadhi kubwa kama hii kwa kuwa wengi hutamani kuichezea timu yao katika mechi kama hiyo. Ni fainali ambayo huja kwa wakati mmoja tu kwa wengi. Hata hivyo, ataendelea kuwa mawazoni mwetu hadi tutakapoondoka tukielekea Baku mwishoni mwa wiki.”

Nyota huyo wa zamani wa Manchester United kwa, upande wake alieleza masikitiko yake kuhusu hali hiyo.

Alituma ujumbe, “Baada ya njia zote za kujumuishwa kikosini kutibuka, ilibidi uamuzi huu ufikiwe na ikaamuliwa nisiende kucheza fainali.

“Ni mechi ambayo huja kwa wakati mmoja tu kwa wachezaji wengi na sasa nimeikosa nafasi yangu. Lazima nikubali nilivyoudhishwa na hali hii. Nitabakia kuwashangilia tu kupitia kwa runinga. Jameni leteni kombe nyumbani.”

Masaibu Manchester United

Wakati huo huo, kocha Jose Mourinho amesema klabu ya Manchester United ina matatizo mengi kuliko Paul Pogba ambaye uhusiano wake naye ulikuwa mbaya.

Mreno huyo ambaye alitimuliwa mwezi Desemba na kazi yake ikapewa Ole Gunnar Solskjaer alisema hata iletewe kocha wa aina gani, klabu hiyo ina shida nyingi zitakazochukua muda mrefu kutatuliwa.

“Si kweli kusema Pogba ndiye aliyekuwa chanzo pekee cha matatizo klabuni, kwani kuna wachezaji wengine ambao ni vigumu kufanya nao kazi, kwa sababu wanajisikia hata kuwa juu ya kocha. Nilikuwa huko na kuonekana kama sikuwa mtu asiyekuwa na manaa wala asiyefaa kutetewa wakati shida zikitokea.”

“Baada yangu, aliingia Solskjaer, akaanza vizuri kwa kushinda mechi 10 kati ya 11, lakini msimu umeisha vibaya kwake baada ya timu kushinda mechi mbili pekee kati ya tisa za mwisho na kumaliza katika nafasi ya sita jedwalini, mbali kabisa na nafasi ya kushiriki soka ya Klabu Bingwa barani Ulaya.”