KAULI YA WALIBORA: Kwa Watanzania, Kiswahili ni amana isiyomithilika ila hawana mwao kuhusu hilo
Na KEN WALIBORA
KATIKA mitaa na vitongoji vya Dar es Salaam utakutana na mabango yenye maandishi ya Kiswahili kila mahali.
“Ujenzi wa barabara unaendelea” “Punguza mwendo kuna waenda kwa miguu,” “Tunauza samaki wabichi, “Tunauza pembejeo za kilimo.”
Utahisi upo katikati ya maskani ya Kiswahili, upo Uswahilini hasa.
Kiswahili kinatawala.
Na kwa Uswahilini naamanisha kwa wasemaji halisi wa Kiswahili, sio Uswahilini kwa maana ya walalahoi au akina yahe.
Maana hii ya pili ya Uswahilini pia hutumika hata na watu wa Uswahilini wenyewe kumaanisha eneo la watu wa tabaka la chini kiuchumi na kijamii.
Ukisoma riwaya za Shafi Adam Shafi kama vile ‘Vuta N’kuvute’ utaliona hili, yaani anaporejelea maeneo maskini kama Uswahilini.
Mathalani wakazi wa Sinza alikonipeleka nifikie au nifie hotelini Prof Aldin Mutembei nilipokwenda kutoa hotuba elekezi katika kongomano la vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili, wanaweza kujiita wakazi wa Uswahilini.
Na Mbezi Beach nilikofikia hivi karibuni zaidi katika hoteli ya ufukweni ni Uzunguni kwa ajili ya kuaminiwa wanakaa huku watu wa nafasi ya hali.
Basi huko Uzunguni Mbezi Beach nilikutana na wahudumu wa hotelini wanaopapia kuzungumza Kiingereza wasichokifahamu.
Mmoja aliniambia kwa bashasha, “I am happy I saw you,” akiwa anataka kumaanisha “I am glad to see you” au kwa Kiswahili chetu adhimu, “Nimefurahi kukuona.”
Sipendi kuwakosoa watu hadharani, ila nilimtazama usoni, macho yetu yakakutana nikaona mpole wa tabia.
Nikaamua nitamkosoa tu kwa upole na liwe liwalo.
Akafedheheka nami moyo ukaniuma.
Akashukuru na kusema hatorudia kosa hilo tena la kukisongoa Kiingereza huku mimi ndani kwa ndani najuta kumkosoa kosa lake la Kiingereza.
Kosa? Kosa lilikuwa nini? Kusema Kiingereza kibaya au kutosema Kiswahili anachokifahamu? Waswahili walisema: “Aliyezoea vya kunyonga vya kuchinja haviwezi.”
Mwajificho
Mtu kazoea kusema Kiswahili siku zote, kusikiliza Kiswahili redioni, (maana karibu kila kituo cha redio Dar es Salaam kinarusha matangazo kwa Kiswahili), kazoea kusoma mabango ya Kiswahili barabarani, kafundishwa masomo yote shule ya msingi kwa Kiswahili, anang’ang’ania nini Kiingereza kinachomcheza mwajificho?
Naona tatizo kubwa Dar es Salaam na kwingineko Tanzania ni mwelekeo wa Watanzania kutoamini thamani ya umilisi wao wa Kiswahili.
Kiswahili wanacho ila hawakijui thamani yake.
Hawajiamini kuwa nacho ni amana isiyomithilika. Ndiyo maana bango moja nililoliona mtaa wa Ohio katikati ya jiji la Dar es Salaam, linasema: “Are you confident speaking English?”
Bango haliulizi kama Mtanzania anajiamini anapozungumza Kiswahili chake.
Linauliza kama anajiamini anapokizungumza Kiingereza cha Theresa May na marehemu Margaret Thatcher.
Mhudumu wa hoteli ya Mbezi Beach aliyenisemea Kiingereza kibovu, alikuwa anajaribu kuonyesha kujiamini kwake katika Kiingereza.
Ana macho yake mwenyewe ila anataka kuonea macho ya watu wengine. Anataka Mwingereza atazame naye aone?
Tatizo la Watanzania kukimbilia Kiingereza wasichokielewa ni tatizo letu sote watu wa Afrika Mashariki. Tunawataka Waingereza wale nasi tushibe? Si umbumbumbu huu?