Makala

AKILIMALI: Talanta ya kuunda vyungu vya maua yampa kipato cha hakika

May 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMUEL BAYA

NI wazi kuwa kila unapobahatika na ujuzi au talanta fulani, basi huna budi kuitumia kujikimu.

Hiyo ndiyo hali halisi aliyo nayo Kijana Bidii Kwicha, mmoja wa jamaa ambao wameibuka maarufu sana katika kaunti ya Kilifi kwa sababu ya kuunda vyungu vya kuwekea maua na mapambo mengine ya nyumba.

Baada ya kugundua kwamba yuko na uwezo wa kutengeza vyungu hivyo, basi alijua ujuzi huo ndio mojawapo ya njia za yeye kujikimu.

Tulipokutana naye mjini Kilifi, hatua chache tu baada ya kulivuka daraja la Kilifi, tulimpata akiwa na shughuli tele akiendelea kutengeneza vyungu hivyo ambavyo anasema ndio njia ya pekee ya kujipatia riziki kwa sasa.

Mbali na kutengeneza vyungu hivyo, Bidii pia ni fundi wa kujenga na kupaka rangi mijengo aina mbalimbali na haya yote huyatimiza bila tatizo lolote.

Anajulikana katika maeneo mengi ya Mtwapa, Mombasa, Kilifi na mjini Malindi na tulipokutana naye kwa mahojiano ilisema kwamba hakwenda zaidi ya darasa la nane kimasomo.

“Mimi sijasoma sana lakini nina ujuzi huu wa kutengeneza vyungu vya kuwekea maua, ujuzi ambao niliupata kutoka kwa rafiki yangu katika kaunti ya Mombasa. Mimi huchanganya simiti, mchanga na kokoto. Kisha baadaye mimi huweka rangi za kila aina zaidi ikitegemea maelekezo ya mteja. Hutengeneza aina tofauti tofauti ya vyungu hivi,” akasema katika mahojiano na Akilimali.

Na ili kudhihirisha ukweli huu, eneo lake la biashara lilikuwa limejaa vyungu vya rangi mbalimbali. Baadhi yavyo vilikuwa bado vinasubiri wenyewe waje kuvichukua.

Bidii Kwicha akiangalia baadhi ya vyungu vyake ambavyo anatengeneza kwa kokoto, simiti na mchanga. Chungu kimoja hugharimu kiasi cha Sh5,000 na wakati biashara inakuwa nzuri yeye hutia mfukoni hata Sh30,000 kwa siku. Picha zote/ Samuel Baya

Kwa chungu kikubwa, Bidii hukiuza kwa Sh5,000 na vile vidogo kabisa hugharimu Sh500 kila kimoja.

Anasema kuwa hupata kiasi cha Sh20,000 au hata zaidi kwa siku wakati biashara inakuwa nzuri.

“Ni biashara ambayo inalipa sana ila inataka uvumulivu kwa sababu mara nyingine mtu anaweza kukaa hadi wiki mbili bila mauzo yoyote. Lakini inapotokea kuuza bidhaa hizi, basi unaweza kupata kipato kizuri,” akasema katika mahojiano yetu.

Mbali na vyungu hivyo vya maua, yeye pia hutengeneza vyungu vya kiasili kwa kutumia udogo, biashara ambayo alisema pia kwake imeanza kumpatia faida.

“Ingawa nikipata mteja anataka vyungu vya kiasili mimi humtengenezea, lakini ari na bidii yangu yote huiweka katika kuunda vyungu vya kifahari ambavyo vinatumika kuwekea maua hasa hasa katika mitaa na hoteli za kifahari za kitalii,” akasema Bidii.

Akieleza historia fupi kuhusu biashara hii, Bidii alisema kuwa alianza mwaka wa 2015 na hadi wakati huo bado hajarudi nyuma wala kufikiria kuiacha.

“Nilianza kazi hii nikiwa kama mpaliliaji maua katika nyumba moja mtaa wa Tudor, Mombasa. Na tangu wakati huo basi sijarudi nyuma kwa sababu nimegundua hii kuwa mojawapo ya kazi ambazo zina mapato mazuri ambayo yanaweza kumsaidia mmoja kufanikisha maisha,” akasema.

Alisema kuwa siku moja, mmilki wa nyumba alikokuwa akifanyia kazi alimtuma amtafutie maua katika eneo la Nyali na hapo ndipo akaenda katika mtaa huo wa kifahari kuyaangalia.

“Tukiwa na mdosi wangu katika eneo la Nyali, aliambiwa kuwa bei ni ghali mno na hapo ndipo aliponiuliza kama ninaweza kumpata mtu akamtengeneza vyungu hivyo kwa bei nafuu,” akasema.

Amleta mweledi

Ndani ya wiki moja alikuwa amepata mtu ambaye ni mweledi wa kuunda vyungu hivyo na akamleta katika eneo la Tudor.

“Nilimuangalia jinsi ambavyo alikuwa akiunda vyungu hivyo na kwa hakika nilifurahia kile alichokuwa akifanya. Nilimwambia huyo mzee anifunze na hakudinda. Akanionyesha na nikajua hadi leo hii,” akasema Bidii.

Na ili kuonyesha kwamba biashara hii inalipa, Bidii tayari amenunua pikipiki na yuko na mpango wa kununua pikipiki nyingine ili kuzidi kujichumia riziki.

“Siku moja mwezi wa Julai mwaka wa 2015, mwanamke mmoja Mkenya ambaye ameolewa na raia wa kigeni alinunua vyungu vya thamani ya Sh10,500 na baada ya mauzo hayo, nigakundua kwamba usaanii huu unalipa. Nilipata motisha zaidi wa kuendelea kuunda vyungu vyengine,” akasema.

Kufikia Mei 2016, Bidii alikuwa amefanya mauzo yaliyokuwa yamefikia kiasi cha Sh96,000.

Akiwa na fedha hizo, aliamua kuacha kibarua alichokuwa akifanya jijini Mombasa na kurudi kwao Kilifi kuendelea mbele na biashara yake.
“Mara nyingi sisi huwa tuko na biashara nzuri sana wakati wa mwezi wa Oktoba, Novemba na Desemba.

Huu ndio msimu ambapo wageni ni wengi Pwani na mara nyingi wao hutaka kununua vitu vya kurembesha nyumba au hoteli zao. Msimu kama huu unaweza kufanya hata mauzo ya Sh20,000 kwa siku,” akasema Bw Bidii.

Miaka miwili iliyopita alipata fursa ya kuuza vyungu vyake vya maua katika hoteli nzuri ya Titanic iliyoko mjini Kilifi.

“Meneja wa hoteli ya Titanic alipita hapa siku moja akaniona nimeunda hivi vyungu na vikampendeza. Alinunua vingi na mauzo hayo yalinisadiai sana katika kufanikisha biashara yangu,” akasema Bidii.

Ingawa jamaa huyu mwenye umri wa miaka 36 anafahamu fika uwepo wa taasisi za serikali kama ile ya mikopo ya vijana pamoja na hazina ya Uwezo, hajakuwa na uhakika kuzihusu.

“Mimi kwa sasa ninajichumia mwenyewe na hata tunavyoongea kwa sasa ninatafuta kupanua biashara yangu hadi katika maeneo mbalimbali ya kaunti ya Kilifi,” akasema.