Sikutarajia timu zinazojiita 'miamba' kugeuka vinyangarika – Oktay
Na GEOFFREY ANENE
KOCHA Hassan Oktay amepapura timu zinazojiita kubwa kwa kutotoa ushindani dhidi ya Gor Mahia baada ya kutawazwa kocha bora wa mwezi wa Aprili uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi, Alhamisi.
Alijishindia zawadi ya Sh75, 000 kutoka kwa wadhamini kampuni ya bima ya Fidelity inayoshirikiana na waandishi wa habari za michezo nchini Kenya (SJAK) kutoa zawadi hii kila mwezi. Tuzo hii ni ya pili ya Oktay baada ya kuibuka bora mwezi Februari.
Raia huyu mwenye asili ya Uturuki na Cyprus aliongoza Gor Mahia kuzoa ushindi dhidi ya Nzoia Sugar, SoNy Sugar, Bandari, Tusker, Ulinzi Stars na Mount Kenya United na sare dhidi ya Kakamega Homeboyz na Ulinzi Stars mwezi Aprili.
“Ni zawadi nzuri kwa kazi hii ngumu. Nafurahia kile timu yangu imefanikiwa kupata,”alisema Oktay kabla ya kupapura timu zinazojiita ‘kubwa’ kwa kutotoa ushindani dhidi ya Gor.
“Tumedondosha alama dhidi ya timu zinazoshikilia maeneo ya chini kwenye jedwali, lakini katika mechi kubwa hakukuwa na ushindani. Tulijiandaa kwa mechi kubwa, lakini tulizipata kuwa ‘vinyangarika’,” alisema, siku chache tu baada ya Gor kunyamazisha mahasimu wa tangu jadi AFC Leopards 3-1.
Oktay, ambaye aliongoza Gor kufika robo-fainali ya Kombe la Mashirikisho la Afrika (CAF Confederations Cup) mwezi Aprili, alizoa kura 12 katika kura zilizoendeshwa na SJAK akimlemea Nicholas Muyoti wa Kakamega Homeboyz na Casa Mbungo wa AFC Leopards.
Vijana wa Muyoti walishinda mechi nne na kupiga sare nne mwezi Aprili nao Leopards wakaandikisha ushindi nne na sare mbili katika kipindi hicho.
Makocha wengine waliozoa tuzo hili msimu huu wa 2018-2019 ni Paul Ogai (Western Stima) mwezi Desemba mwaka 2018), Francis Kimanzi (Mathare United) mwezi Januari 2019) na John Baraza (Sofapaka) mwezi Machi 2019.