Michezo

Lucy Wambui apigiwa upatu kutamba Ufaransa

May 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa Riadha za Dunia za mbio za milimani Lucy Wambui Murigi kutoka Kenya anapigiwa upatu kuanza vyema Kombe la Dunia la mwaka 2019 katika duru ya kwanza mjini Annecy nchini Ufaransa mnamo Mei 24, 2019.

Murigi alitwaa mataji ya dunia ya mwaka 2017 mjini Premana nchini Italia na 2018 mjini Canillo nchini Andorra. Kombe la Dunia linajumuisha duru saba ambazo ni Salomon Gore-Tex Maxi Race (Annecy, kilomita 16.5) mwezi Mei, Broken Arrow Sky Race (Marekani, kilomita 26) mwezi Juni, Grossglocknerlauf (Austria, kilomita 12.7) mwezi Julai, Snowdon (Uingereza, kilomita 15.5) mwezi Julai, Sierre-Zinal (Uswizi, kilomita 31) mwezi Agosti, Drei-Zinnenlauf (Italia, kilomita 17.5) mwezi Agosti na Smarna Gora nchini Slovenia inayojumuisha kilomita 10 mwezi Septemba.

Riadha za Dunia za mbio za milimani zitafanyika Novemba 15, 2019 nchini Argentina.

Kuhusu mbio za Annecy ni kwamba Murigi atapata ushindani mkali kutoka kwa Sarah McCormack (Ireland), Waingereza Emma Clayton na Louise Mercer, Waitaliano Camilla Magliano na Samantha Galassi na Celine Jeannier, ambaye ni tegemeo wa Ufaransa.

Kenya pia inawakilishwa katika kitengo cha wanaume na Robert Panin Surum.