KIKOLEZO: Nusra wachonge viazi
Na THOMAS MATIKO
UVUMILIVU ni sifa muhimu sana katika maisha ya mwanadamu.
Kwenye ulimwengu wa burudani, uvumilivu na bidii ndivyo viungo muhimu zaidi anavyohitaji mwanamuziki.
Wapo wasanii ambao wamepambana sana kwa miaka mingi kisanaa bila mafanikio.
Kuna wale walioishia kuachia ‘hit’ lakini ikabaki kuwa jina tu, huku maisha yakiendelea kuwa magumu kwao.
Wapo waliokata tamaa na kuachana na muziki, wapo waliovumilia na kuendelea.
Pia wapo wale ambao baada ya kuvumilia sana, walifika mwisho na walipokaribia kukataa tamaa, ndipo milango yao ya nuru ikafunguka.
Mercy Masika
Safari ya muziki ya staa wa injili Mercy Masika ilianza miaka 15 iliyopita japo jina lake limekuja kupata umaarufu mkubwa ndani ya miaka mitano au sita iliyopita.
‘Hit’ ya kwanza aliyoachia kipindi akianza safari yake ya muziki ilikuwa Amukomete (2008).
Wimbo huo ulitayarishwa na produsa mkongwe Robert Kimanzi al-maarufu R Kay. Ndio wimbo ulioishia kumpa tuzo yake ya kwanza ya Groove Awards akiibuka kama msanii bora wa 2008.
Japo ilimsaidia kupata umaarufu, haikuweza kumzalishia mkwanja wa maana.
Aliendelea kufanya muziki na katika pilkapilka hizo akafanikiwa kupata familia na kujaliwa watoto.
Majukumu yakaongezeka na maisha yakawa magumu kidogo kuliko hapo awali.
Akifunguka hivi majuzi katika mahojiano yake na Play House, Mercy alikiri kuwa baada ya kujaliwa watoto, maisha yalikuwa magumu sana kiasi kwamba muziki ulianza kumshinda.
Sababu kubwa ikiwa ni kwamba alikuwa akiufanya ila haukuwa ukimpa mkwanja wa maana.
“Ilifikia kipindi nilitaka kukata tamaa hata na huduma ya kanisani, pasta wangu akagundua na kunitia moyo.
Kuna nyakati nilikosa hata chakula cha kuwapa wanangu ila Mungu alinisimamia,” akafunguka.
Maneno ya faraja kutoka kwa pasta wake ndiyo yalichangia yeye kuendelea na muziki hadi alipoachia kibao Mwema miaka mitano iliyopita.
Anasema hakuwa na hamu tena ya muziki na wimbo huo Mwema aliufanya tu kuachia bila ya kuwa na matarajio yoyote.
Lakini ndio uliogeuka na kumfungulia milango ya nuru akaanza kupata michongo ya nguvu, shoo hadi nje ya nchi, dili za kimatangazo na mkwanja mrefu ukaanza kutiririka mpaka sasa.
“Niliingia darasani kusomea shahada ya uzamili kuhusu Huduma ya Jamii kwa sababu muziki haukuwa ukinipeleka vizuri.
Hata tulipokuwa tunashuti video ya Mwema nilikuwa nafanya ile ya basi tu. Tulitumia muda wa saa moja tu na cha kushangaza ni kwamba wimbo huo nilioufanya kimzahamzaha uligeuka kuwa Lulu iliyonitoa vizuri,” Masika akaongeza.
Toka hapo ameendelea kuachia fataki za mfululizo ikiwemo Shule Yako, Nikupendeze, Huyu Yesu na He Never Lies.
Hata hivyo japo kazi zake toka hapo zimekuwa na utazamaji mkubwa kwenye YouTube, hakuna iliyoweza kuifikia Mwema iliyotizamwa na zaidi ya watu 11.7 milioni.
Guardian Angel
Baada ya kuhangaika kwa miaka saba kwenye muziki wa injili, Audiphaxad Peter Omwaka al-maarufu Guardian Angel alichoka na kufikia hatua ya kukata tamaa.
Muziki aliokuwa akiufanya haukuwa ukilipa kabisa. Ikafikia wakati mmoja 2017 hangeweza kuendelea kumudu gharama ya kuandaa muziki na kushuti video.
Hapo Guardian Angel akafikia uamuzi wa kuachia wimbo mmoja wa mwisho na kisha afunge safari kuelekea Canada aliko mamake kusaka maisha mapya.
“Baada ya kuwa kwenye gemu kwa muda, nilihisi mambo hayakuwa yakiniendea vizuri kimuziki jinsi nilivyokuwa natarajia. Nilikuwa nahangaika hata kulipa kodi ya nyumba. Niliamua naachana na Muziki na nikamwomba Mungu anipe kibali cha wimbo mmoja pekee na baada ya hapo ningechana na muziki kabisa niende zangu. Septemba 2017 nikaachia Nadeka na jambo la kushangaza kazi hiyo ikaishia kuwa ‘hit’ kubwa na kunibadilishia maisha kabisa,” Guardian Angel alisimulia awali.
Ufanisi wa kazi hiyo ulimwezesha kukutana na wadau mbalimbali ikiwemo meneja mzoefu aliyemwezesha kujibrandi kivingine.
Kwa sasa maisha yake yapo kwenye kistari akiwa hata na uwezo wa kumiliki gari la kifahari la ndoto yake Mercedez Benz.
Nadeka ndio wimbo wake katika zote uliotizamwa sana Youtube ukiwa na ‘views’ 1.2 milioni.
Nyashinski
Baada ya kutamba na kundi la Kleptomaniax yapata mwongo mmoja uliopita, wakiachia ‘hit’ kama Tuendelee ama Tusiendelee, kundi lilisambaratika.
Nyamari Ongegu al-maarufu Nyash pamoja na familia yake wakahamia Amerika.
Katika mahojiano ya awali, alikiri kwamba umaarufu wa kipindi kile ulianza kumwathiri kiasi cha kuacha shule.
Lakini pia presha ya kuachia muziki kila kukicha ikawa inamlemea. Mkwanja walikuwa wakiupata lakini sio sana na huku kukiwa na fursa ya kwenda majuu, akaona kheri asafiri tu kusaka ulaji zaidi. Miaka 10 baadaye, alirejea nyumbani kwa ajili ya likizo na wakati huo akaachia kolabo Letigo akishirikishwa na Nameless.
Ni wimbo anaosema hakuwa makini nao sana ila aliufanya kutokana na ushikaji wake na Nameless. Lakini baada ya kuishia kuwa kete kali, ndipo mawazo yake ya kurejea nyumbani kuendelea na muziki yakarudi tena.
“Niliamua kurudi Marekani kuwaomba wazazi wangu baraka za kurudi nyumbani nifanye muziki. Waliniuliza kama nina uhakika nami nikawajibu ndio,” akasema.
Ndivyo alivyorejea 2016 akiwa hana hela zozote na kuanza upya akiachia ‘hits’ za mfululizo kama Mungu Pekee, Malaika, Free na Now You Know.
Kwa sasa ni kati ya wasanii wanaofukuziwa sana na mapromota nchini.
Bruno Mars
Akiwa na umri wa miaka 18, staa huyu wa Pop kutoka Amerika alihamia mjini Los Angeles kutoka kwao alikozaliwa Honolulu.
Alipohitimu umri wa miaka 19, Bruno alikata tamaa ya kuendelea na muziki baada ya kuchujwa na lebo iliyokuwa imemsaini wakati huo, Motown.
Alikuwa amepata mafunzo ya udijei lakini bado alihangaika kupata riziki kwani hata senti za kuliweka gari lake mafuta zilikuwa ni tatizo.
Akiwa amekataa tamaa kabisa, mjomba wake aliyekuwa mcheza gita, alizidi kumtia moyo apambane.
Bruno alimsikiza na nyota yake ilianza kung’aa 2008 alipomwandikia rapa Florida wimbo Right Round.
Wimbo huo uliishia kukamata nafasi ya kwanza kwenye chati za Bilboard Hot 100. Ukamfungulia milango kwani sasa huduma yake ya uandishi ilianza kusakwa na mastaa kibao.
Miaka miwili baadaye, msanii Travie McCoy alimhusisha kwenye kolabo Billionaire ulioishia kuwa ‘hit’ kubwa na hata kumfungulia milango zaidi. Kwa sasa ana zaidi ya tuzo 13 za Grammy na ni mmoja kati ya mastaa wa Pop matajiri.
Eminem
Huwezi kuwazungumzia marapa wenye mafanikio makubwa bila kulitaja jina la lejendari Eminem.
Safari yake haikuwa rahisi kabisa lakini alipambana. Akiwa na miaka 25, mwaka wa 1997 alishiriki kwenye shindano la kusaka vipaji vya Hip hop mjini Los Angeles ambapo tuzo lilikuwa ni dola 500 (Sh50,000).
Hata hivyo alipopanda stejini kuchana, alibaki kusimangwa, kukejeliwa na kukebehiwa na mashabiki wengi wao wakiwa ni watu wa asili nyeusi yeye akiwa ni mzungu.
Kitu hicho kilimuumiza sana na akaamua kuachana na muziki.
Hata hivyo produsa mkongwe aliyekuwepo katika shindano hilo Dr Dre alimchukua na kumpa fursa na hapo akaanza safari ya mafanikio yake kwenye gemu.