Makala

MWANAMKE MWELEDI: Ameweka kumbukumbu angani

May 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KENYA YEARBOOK

TANGU jadi, katika biashara ya usafiri wa ndege, wanawake walitengewa nafasi za ajira zisizo za kiufundi kama vile wahudumu na wafanyakazi wengine wa kawaida.

Lakini ni dhana ambayo Koki Mutungi ameweza kuibadilisha na katika harakati hizi kuandikisha jina lake kwenye orodha ya wanawake waliojizatiti na kufanikiwa katika taaluma ambazo awali zilitengewa wanaume.

Mwaka wa 1995, mwanafunzi huyu wa zamani wa shule ya upili ya wasichana ya Moi Girls’ School, Nairobi, alivunja rekodi na kuwa rubani wa kwanza mwanamke kuendesha ndege katika shirika la kitaifa la ndege; Kenya Airways.

Jitihada zake katika kuweka kumbukumbu hazikukomea hapo kwani mwaka wa 2014, alienda hatua zaidi na kuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kupata cheti cha urubani kuendesha ndege aina ya Boeing 787 ‘Dreamliner’. Ni suala lilomfanya kubandikwa jina ‘Boeing Girl’.

Bi Mutungi alizaliwa mwaka wa 1976 huku penzi lake katika masuala ya urubani likianza akiwa mdogo kiumri.

Katika umri mdogo wa miaka mitano, ari yake ya kujitosa katika urubani ilizidi na kuchangiwa hasa na babake. Wakati huo alikuwa akimtazama babake ambaye kwa sasa ni rubani mstaafu, akiwa kazini.

Alipata leseni yake ya urubani kutoka chuo cha Kenya School of Flying (Private-Pilot license) kilichoko katika uwanja wa ndege wa Wilson Airport, Nairobi na hakutia kikomo bali aliendelea kutia bidii kujiimarisha.

Ili kupiga msasa ujuzi wake katika fani hii, aliongeza kiwango cha elimu kwa kupata mafunzo zaidi katika chuo cha Oklahoma City Flying School nchini Amerika.

Ni hapa ndipo alipata leseni yake ya urubani wa kuendesha ndege katika anga za kimataifa na kulipwa pia(Commercial-Pilot license) kutoka kwa halmashauri ya the Federal Aviation Authority nchini humo humo.

Ingawa kazi hii imemwezesha kuzuru mataifa mbalimbali, vile vile kumpa fursa ya kukutana na watu kutoka matabaka tofauti, ushupavu wake Bi Mutungi hauishii tu angani.

Ufanisi wake kama rubani umemfanya kuwa mstari wa mbele kushika mikono wanawake wengine katika harakati za kuwapitisha kwenye barabara aliyoiunda.

Afichulia wanawake taaluma

Kwa miaka amekuwa akinasihi kizazi kijacho cha marubani wanawake na katika harakati hizo kusaidia katika kufichulia wanawake taaluma hii ambayo kwa miaka imekuwa ikitengewa tu wanaume.

Mwaka wa 2014, aliongoza kundi la marubani na wahudumu wa kike walioleta nchini ndege ya nne ya aina ya B787-8 Dreamliner iliyokuwa imeagizwa na shirika la Kenya Airways, kutoka kiwanda cha ndege cha Boeing nchini Amerika. Kikundi hicho kilipewa jina ‘Dreamgirls’.

Japo urubani unahitaji ujuzi wa hali ya juu wa kiufundi, Bi Mutungi amekuwa makini kuakisi kama taaluma ambayo yaweza kufanywa na yeyote aliye na moyo na bidii ya kufanikiwa.

Ni suala ambalo limemfanya kuwa kigezo cha wasichana, na rubani anayestahili kuvuliwa kofia sio tu humu nchini, bali ulimwenguni kote.