• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Kibwana, Mutua na Ngilu watisha kumkata miguu Kalonzo

Kibwana, Mutua na Ngilu watisha kumkata miguu Kalonzo

Na BENSON MATHEKA

UMOJA wa magavana wa kaunti tatu za Ukambani ambao unaonekana kupata nguvu kila siku, unaweza kuwa pigo kwa maisha ya kisiasa ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka siku zijazo iwapo hatacheza siasa zake vyema.

Wadadisi wa siasa eneo la Ukambani wanahisi kwamba japo kwa wakati huu Bw Musyoka angali kigogo wa siasa za Ukambani na umaarufu wake uko imara, unaweza kuathiriwa pakubwa iwapo juhudi za magavana hao zitafua dafu.

“Kuna uwezakano wa umaarufu wa Bw Musyoka katika ngome yake ya Ukambani kuathiriwa na umoja wa magavana hao ikiwa wataweka mikakati ya kutosha kuthibitishia wapigakura kwamba wanajali maslahi yao. Hata hivyo, itategemea jinsi Bw Musyoka atacheza siasa zake,” asema mdadisi wa siasa Joshua Kisilu.

Magavana Alfred Mutua wa Machakos, Profesa Kivutha Kibwana wa Makueni na Charity Ngilu wa Kitui wamepiga hatua katika muungano wao kwa kuanzisha vikao vya pamoja vya serikali zao kupanga mikakati ya maendeleo.

Tangu mwaka jana walipotangaza muungano wao magavana hao wamekuwa wakimshambulia vikali Bw Musyoka wakidai hajafanya lolote kustawisha eneo la Ukambani kwa miaka 30 aliyokuwa serikalini.

Katika mkutano uliofanyika mjini Machakos wiki jana, magavana hao walisema wanalenga kuunganisha jamii ya Wakamba ili kuipatia mwelekeo tofauti za kisiasa.

Magavana hao wamekuwa wakimlaumu Bw Musyoka na wandani wake wa kisiasa kwa kuendeleza siasa za ubinafsi na kufanya eneo la Ukambani kubaki nyuma kimaendeleo.

Wanamlaumu Bw Musyoka kwa kile wanachodai kuwa siasa zake za kupalilia umasikini.

Kulingana na Dkt Mutua, wakati umefika wa jamii ya Wakamba kubadilisha jinsi inavyocheza siasa ili kujinasua kutoka utando wa umasikini.

Wadadisi wanasema ikizingatiwa kuwa Dkt Mutua ametangaza azima yake ya kugombea urais na ikiwa ataungwa mkono na magavana wenzake huenda ukawa mwanzo wa mabadiliko makubwa ya maisha ya kisiasa ya Bw Musyoka.

“Kumekuwa na vita vya ubabe wa kisiasa Ukambani kati ya Bw Musyoka na Bi Ngilu tangu siasa za vyama vingi zilipoanza nchini. Ni vita hivyo anavyoendeleza Dkt Mutua ambaye anasema vigogo wa siasa wa zamani wanapaswa kustaafu na kuachia kizazi kipya nafasi kupatia jamii mwelekeo mpya kisiasa. Profesa Kibwana pia hajakuwa na uhusiano mwema na Bw Musyoka,” asema Bw Kisilu.

Mtaalamu huyu anasema ikizingatiwa kwamba Bw Musyoka anaungwa mkono na mahasimu wa magavana hao ambao wana ushawishi mkubwa katika jamii hiyo na hata kitaifa, itabidi wakuu hao wa kaunti kuweka mikakati madhubuti kugeuza mkondo wa siasa Ukambani.

Kulingana na washirika wa karibu wa magavana hao, mikakati yao ni kuhakikishia wakazi kwamba wanajali maslahi yao kwa kuanzisha miradi ya maendeleo inayofaidi kaunti tatu za Ukambani.

Kwenye mkutano wa wiki jana mjini Machakos, magavana hao walitangaza kuwa watashirikiana kuanzisha benki ya pamoja chini ya mwavuli wa muungano wa kiuchumi wa kaunti za Kusini Mashariki mwa Kenya (SEKEB) miongoni mwa miradi mingine ya kuimarisha uchumi.

Kwa kufanya hivi, wanalenga kushirikiana na madiwani ambao wana ushawishi mashinani.

“Kamati ya pamoja ya kuweka sera za kisheria katika kaunti zetu itabadilishana maoni kuhusu jinsi ya kukuza uchumi na kuainisha sera kuimarisha ushirikiano na kupata masoko,” magavana hao walisema baada ya mkutano ambao ulishirikisha maafisa wakuu wa serikali za kaunti zao.

Kulingana na wadadisi, hii ni mbinu ya kuhakikisha kwamba iwapo watakubali kumuunga mmoja wao kugombea urais watakuwa na uungwaji mkono mashinani kwa msingi wa maendeleo na kukuza uchumi wa wakazi.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kwamba ikizingatiwa kuwa madiwani wengi kaunti za Ukambani na Wabunge ni wa chama cha Wiper cha Bw Musyoka, huenda ikawa ni mlima kwa magavana hao kumbandua kama msemaji wa jamii hiyo.

“Nafikiri hali halisi itajitokeza baada ya siasa za uchaguzi kuanza rasmi na jinsi Wiper kitaweka mikakati yake kuanzia mchujo. Kumbuka Dkt Mutua na Bi Ngilu wana vyama vyao vya kisiasa ambavyo wanaweza kutumia kuhifadhi wanasiasa wakihama Wiper na kujipiga jeki,” alisema Bi Jane Munyiva, mdadisi wa siasa za Ukambani.

Anasema Dkt Mutua na Profesa Kibwana wanahudumu vipindi vya mwisho kama magavana na huenda ushawishi wao mashinani ukapungua wakiondoka ofisini hata kama watagombea urais.

“Bi Ngilu ambaye anahudumu kipindi cha kwanza ana uzoefu wa kisiasa ilivyodhihirika kwenye uchaguzi uliopita ambapo alishirikiana na Bw Musyoka kuhakikisha alishinda mgombeaji wa Wiper na vigogo wengine wa kisiasa kaunti ya Kitui, anajua kubadilisha mkondo wa kisiasa kumfaa,” asema Bi Munyiva.

Aliyekuwa seneta wa Machakos Johnson Muthama anasema kwamba wanaodhani wanaweza kufifisha umaarufu wa Bw Musyoka Ukambani wanaota mchana.

“Hakuna mtu anayeweza kushindana na kiongozi aliyetawazwa rasmi na wazee kuwa msemaji wa jamii yao. Mzee wa kijiji hawezi kushindana na kiongozi wa hadhi ya Musyoka. Wacha wanaopanga mambo yao waendelee, wakati ukifika, watajua walijidanganya,” asema Bw Muthama.

You can share this post!

Polisi wanatimua wakazi ardhini kiharamu – Jumwa

JAMVI: Ni wasemaji watetezi au mabubu?

adminleo