JAMVI: Ni wasemaji watetezi au mabubu?
Na PETER MBURU
WANASIASA vigogo nchini ambao ndio wasemaji wa jamii zao na mirengo ya kisiasa wanayoongoza wameendelea kupoteza umaarufu mbele ya umma na kufifisha sauti za kuzungumza kwa niaba ya wafuasi wao, kutokana na hali yao kukosa kusimama imara kuwatetea katika masuala tofauti mara kwa mara.
Tangu Machi 9, 2018 wakati Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga waliafikiana kuzika tofauti baina yao na kuanza kushirikiana, mazingira ya kisiasa na kiuongozi yamebadilika nchini, hali ikigeuka na kuwanyima vigogo hao sauti za kuzungumzia masuala ya kisiasa na kijamii yanayoathiri wafuasi wao, kama ilivyokuwa mbeleni.
Tukio la Rais kuafikiana na Bw Odinga liliwapata wengi wa wafuasi wake kwa ghafla, na hatua ambazo viongozi hao wamekuwa wakichukua baadaye hazijakuwa za kufurahisha ngome zao, hali ambayo imeathiri wadhifa wao wa usemaji kwa niaba ya jamii zao na mirengo ya kisiasa.
Katika eneo la Mlima Kenya, hali hii imejidhihirisha kutokana na mipasuko inayoonekana miongoni mwa viongozi, baadhi wakimtetea Rais, wengine kujiunga na Naibu Rais William Ruto na wengine kusalia bila msimamo.
Vilevile, wakazi eneo hilo wamekuwa wakimkashifu Rais kutokana na hali ya serikali yake kuchukua hatua zinazowaathiri kiuchumi, hali ambayo imemfanya Kiongozi wa Taifa kufyata ulimi na kukosekana eneo hilo kwa kuwa anajua huenda umma umeghadhabika naye.
“Watu wetu wanalia kwa kuwa wamefungiwa kila mlango wa kupata pesa, mara magari makuu yanazuiwa kuingizwa, bidhaa kutoka mataifa fulani zinazuiwa. Kuna vizingiti tele kibiashara na ni watu wetu tu vinaathiri,” mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria akasema majuzi.
Katika chama chake cha Jubilee vilevile, licha ya kuwa kiongozi wake Rais amekosa kujitokeza kutoa mwelekeo, akiwaacha viongozi kutawanyika kila upande.
Licha ya mito kuwa aandae mkutano wa wabunge wa chama hicho, Rais Kenyatta ambaye ndiye msemaji wa chama hajatamka lolote, wakati viongozi ndani ya chama hicho wanavurugika kila uchao.
Duru zinasema kuwa huenda kinachomfanya Rais kutoandaa kongamano la wabunge wa chama chake ni kuogopa kukabiliwa na maswali kuhusu ‘handisheki’, na msimamo wake kumhusu Naibu Rais. Hali hiyo imemwacha kuwa kimya licha ya kuwa msemaji wa chama, akisalia kukiona kikijikaanga tu.
Katika ngome ya Bw Odinga, mambo pia yamepamba moto, kiongozi huyo akiwa ndiye ameathirika na ukimya zaidi ya wote, tangu alipoanza kushirikiana na Rais.
Kabla ya muafaka, Bw Odinga ndiye alikuwa msemaji mkuu wa upinzani na sauti ya kutetea wanyonge, utetezi wake ukiwavutia hata baadhi ya watu kutoka ngome za mahasimu wake na mataifa ya nje.
Kelele za Bw Odinga zilisaidia kuiwajibisha serikali, lakini hali hiyo ilibadilika mara moja kwani sasa anafanya kazi kama sehemu ya serikali.
Kushirikiana na serikali katika mambo mengi kumemnyima kiongozi huyo sauti ya kuzungumza dhidi ya hatua za serikali ambazo zimewakera Wakenya, akigeuka kuwa wa kuitetea na kupuuza vilio vya Wakenya.
Aidha, hali yake kuwa karibu sana na serikali imesababisha kuanza kuonekana ishara za pingamizi ngome yake Nyanza, kisa cha majuzi ambapo vijana waliomkashifu na kumpigia kelele hadharani alipokuwa akihutubu eneo la Muhoroni, Kaunti ya Kisumu kikizingatiwa.
Tangu Bw Odinga aanze ushirikiano na Rais na kupata kazi katika Umoja wa Afrika, anaonekana kupoteza sauti ya kuzungumza kwa niaba ya jamii yake, upinzani na Wakenya wa kawaida kwa jumla.
Mambo si tofauti eneo la Mashariki, kwani msemaji wa jamii ya Wakamba, Kalonzo Musyoka naye kwake kumejaa pingamizi dhidi yake kutoka kwa viongozi mashuhuri, tangu alipojitangaza kuwa ‘kijana wa mkono’ wa Rais Kenyatta.
Magavana Kivutha Kibwana (Makueni), Alfred Mutua (Machakos) na Charity Ngilu (Kitui) ndio walianza vuguvugu la kumpinga Bw Musyoka wakisema hatetei maslahi ya jamii hiyo, na kukashifu hali yake kujiita ‘kijana wa mkono’ kuwa iliyomnyima sauti.
Bw Musyoka hajakuwa akizungumza kuhusu masuala ya jamii ya Kamba, mara nyingi viongozi hao wakiwa ndio picha inayojitokeza, licha ya kuwa yeye ndiye msemaji halisi wa jamii hiyo hadi sasa.
Tangu Bw Musyoka kumkaribia Rais na kuanza ‘kuwekwa karibu’, hata wakati mmoja ikasemekana alikuwa akitafutiwa kazi, kiongozi huyo aliweka jukumu lake la kutetea maslahi ya jamii ya Kamba na upinzani kando, siku hizi akipiga mwangwi tu wa matamshi ya serikali.
Eneo la magharibi, misukosuko baina ya viongozi wa eneo hilo imekuwa hali ya kila siku na hadi sasa hawajaketi katika meza moja kupata mwelekeo.
Japo wengi wanaamini kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ndiye msemaji wa jamii ya Waluya, kiongozi huyo amekuwa kimya viongozi wa eneo hilo wakivuma na wapinzani huko, na hawajaafikiana na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kuhusu kuunganisha jamii hiyo kisiasa.
Matukio haya yamewanyima vigogo hao nguvu za kuzungumza kwa niaba ya jamii hiyo, maeneo ama wafuasi wao, wakiishia kusalia kimya japo mambo yako kombo.
Hali hiyo, kulingana na wadadisi imewafanya wananchi kuanza kujitetea kwa mbinu zao moja kwa moja kama kupitia mitandao ya kijamii, na kuwakashifu vigogo hao kwa kuona kuwa hawana sauti tena.
Rais anakumbana na lawama tele eneo la Mlima Kenya, Bw Musyoka ni kama alishapoteza sauti kabisa, nako kwenye ngome ya ‘Baba’, ishara za pingamizi zimeanza kujitokeza, hali ambayo si ya kawaida.
Wadadisi wanasema kuwa hali hii imechangiwa na viongozi kuzingatia maslahi yao ya kibinafsi badala ya kutetea jamii, nao wananchi wakihisi “kuchoka kuongozwa na vipofu.”
“Viongozi hao wanataka kujitimizia maslahi yao wenyewe ndiposa wananchi wameanza pingamizi dhidi yao, kujipazia sauti kuhusu matatizo wanayokumbana nayo. Hakuna anayeweza kuamini mbwa kipofu kumwelekeza,” anasema Dkt Duncan Ojwang, mhadhiri katika chuo kikuu cha Africa Nazarene.
Naye Naibu Rais William Ruto pia amejipata katika njiapanda katika ngome kuu ya Bonde la Ufa.
Ingawa alipata uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa tangu 2012, baada ya chama cha URP kuungana na TNA kubuni muungano wa Jubilee, hali umaarufu wake wa kisiasa umeendelea kuyumba.
Hilo limeibua maswali ikiwa bado anaendelea kuonekana kama msemaji halisi wa jamii ya Wakalenjin kama ilivyokuwa wakati wa kuasisiwa kwa muungano huo.
Kufikia sasa, Dkt Ruto aanakumbwa na upinzani mkubwa, ukiongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi.
Aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto pia ameanza harakati za kufufua Chama Cha Mashinani (CCM) ambacho kilitumiwa na wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali za kisiasa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 katika ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Seneta Moi pia amekuwa akiendesha juhudi za kichinichini kufufua chama cha Kanu, ambacho anakiongoza.
Majuzi, baadhi ya waliokuwa waandani wa karibu wa Dkt Ruto walihama kutoka kundi la ‘Tanga Tanga’ na kujiunga na CCM. Mojawapo ya viongozi hao ni mfanyabiashara Zedekiah Bundotich, maarufu kama “Buzeki” aliyewania ugavana katika Kaunti ya Uasin Gishu.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho pia anakabiliwa na wakati mgumu kujinadi kama “mfalme na msemaji” wa ukanda wa Pwani.
Kulingana na wachanganuzi, umaarufu kwa kiongozi huyo umepungua maradufu, kinyume na ilivyokuwa 2013 na 2017.
Kwa sasa, baadhi ya wapinzani wake wakuu ni Gavana Amason Kingi (Kilifi) na mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa, ambao walikuwa nao katika kambi moja ya kisiasa mnamo 2013 na 2017.
Kati ya 2013 na 2017, Bw Joho alipata umaarufu mkubwa kama mtetezi wa eneo hilo, hasa kwa kuipinga serikali ya Jubilee.
Vile vile, asema kwamba itakuwa vigumu kwake kupata uungwaji mkono, hasa baada ya kutangaza atawania urais mnamo 2022.
Hali ni hiyo kwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale, ambaye anaonekana kupoteza udhibiti wa kisiasa katika ukanda wa Kaskazini Mashariki.
Wachanganuzi wanasema kuwa baadhi ya viongozi wanaoonekana kumpa ushindani mkubwa kama msemaji wa ukanda huo ni Gavana Ali Roba wa Mandera, ambaye anaonekana sana, hasa kwenye vita dhidi ya ugaidi.