Michezo

Shujaa hatarini kutemwa Raga ya Dunia

May 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imepata pigo kubwa katika juhudi zake za kukwepa kuangukiwa na shoka kwenye Raga ya Dunia baada ya kuchapwa 29-21 na Scotland katika robo-fainali ya Challenge Trophy na kuteremka katika mduara wa kupigania nafasi tatu za mwisho katika duru ya London nchini Uingereza, Jumapili.

Dhidi ya Scotland, nambari 13, Shujaa ilijiliwaza na miguso kutoka kwa Andrew Amonde (miwili) na Jeffery Oluoch iliyoandamana na mikwaju kutoka kwa Johnstone Olindi (miwili) na Daniel Taabu (mmoja).

Alama nyingi ambazo Kenya, ambayo itarukwa na Wales kwenye msimamo wa ligi hii ya mataifa 15 baada ya nambari 14 Wales kuchapa nambari 15 Japan 17-0 katika mechi nyingine ya robo-fainali ya Challenge Trophy, inaweza kupata jijini London ni tatu.

Kwa sasa, Kenya imezoa alama 26 kutoka duru nane za kwanza, pointi moja mbele ya Wales, ambayo itazoa kati ya alama tano na nane kulingana na nafasi itakayomaliza katika mechi za kuorodhesha nambari tisa hadi 12.

Vijana wa kocha Paul Murunga walianza kampeni ya London Sevens kwa kulemewa 24-17 na Fiji, wakazima Samoa 21-20 na kunyamzishwa 31-17 na Ufaransa katika mechi za Kundi B hapo Mei 25.

Kichapo cha nne mfululizo dhidi ya Scotland kinamaanisha kwamba lazima Kenya ipepete Japan saa nane na dakika 58 Jumapili ili ipunguze presha inayozidi kuiandama