Kipsang' alenga tena kuvunja rekodi ya dunia kwenye Tokyo Marathon
Na GEOFFREY ANENE
BAADA ya kukosa rekodi ya dunia ya saa 2:02:57 kwa dakika moja na sekunde moja mwaka 2017, Wilson Kipsang’ ataivizia rekodi hiyo tena kwenye Tokyo Marathon hapo Februari 26, 2018.
Mkimbiaji huyu Mkenya, ambaye atafikisha umri wa miaka 36 mwezi ujao Machi 15, aliwahi kushikilia rekodi ya dunia ya mbio hizi za kilomita 42 mwaka 2013 aliposhinda Berlin Marathon nchini Ujerumani kwa saa 2:03:23.
Rekodi yake ilivunjwa na Mkenya mwenzake Dennis Kimetto katika Berlin Marathon mwaka 2014.
Hakuna mtu amefanikiwa kuvunja rekodi ya Kimetto. Hata hivyo, tangu mwaka 2016, rekodi ya Kimetto imekuwa hatarini. Karibu ifutwe katika Berlin Marathon mwaka 2016 Muethiopia Kenenisa Bekele na Kipsang’ walipomaliza umbali huo kwa saa 2:03:03 na 2:03:13, mtawalia.
Pia bingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge alikosa rekodi hiyo pembamba katika mbio za London Marathon mwaka 2016 aliponyakua taji kwa saa 2:03:05. Kipchoge alitwaa ubingwa wa Berlin Marathon kwa saa 2:03:32.
Wapinzani wakuu
Baadhi ya wapinzani wakuu wa Kipsang’ katika makala haya ya 12 ni mabingwa wa Tokyo Marathon mwaka 2014 Dickson Chumba (Kenya) na mwaka 2016 Feyisa Lilesa (Ethiopia).
Wakenya wengine wanaoshiriki makala haya ni Vincent Kipruto, Amos Kipruto, Gideon Kipketer na Bernard Kipyego. Mahasimu wa jadi wa Kenya, Ethiopia, pia wanawakilishwa na wakimbiaji Tesfaye Abera na Tsegaye Mekonnen.
Bingwa wa Tokyo Marathon mwaka 2016, Helah Kiprop ataongoza kampeni ya kinadada kutoka Kenya. Atashirikiana na Purity Rionoripo, ambaye alishinda Paris Marathon nchini Ufaransa mwaka 2017.
Tishio kubwa ni kutoka kwa Waethiopia Shure Demise, Ruti Aga, bingwa wa mwaka 2015 Birhane Dibaba, na Meseret Defar, ambaye atashiriki marathon kwa mara ya kwanza kabisa. Kiprop ameonya wapinzani wake watarajie vita vikali vya kuwania taji.