SAKATA YA DHAHABU FEKI: Raila ajikaanga
MACHARIA MWANGI Na CHARLES LWANGA
HATUA ya Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga kujitokeza kueleza mchango wake kwenye sakata ya dhahabu feki, imetoa fursa kwa wandani wa Naibu Rais, Dkt William Ruto kumshambulia zaidi.
Bw Odinga alipokuwa Kisii mnamo Ijumaa, alikiri kwenda Dubai kukutana na kiongozi wa taifa hilo Mohammed bin Rashid Al Maktoum, lakini akasema alienda kumweleza jinsi matapeli walivyokuwa wanatumia sauti ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kufanya biashara ya kilaghai ya dhahabu feki.
Lakini sasa madai hayo yake yamemgeuka, na mahasimu wake wa kisiasa wanataka aende akaandikishe taarifa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusu kile anachofahamu katika sakata hiyo.
Wakizungumza jana katika kanisa Katoliki la St Xavier mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru, wafuasi wa kundi la Tangatanga wakiongozwa na Dkt Ruto walisema wahusika wote katika kashfa hiyo wanahatarisha uhusiano mwema uliopo baina ya Kenya na Dubai.
“Kazi ya Raila katika AU haihusu kufanya biashara za madini,” Dkt Ruto akasema, akirejelea wadhifa wa Balozi wa Miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU) anaoshikilia Bw Odinga.
“Waache kutaja jina la Rais Kenyatta katika maelezo kuhusu sakata hiyo ya dhahabu feki,” akasema Dkt Ruto.
Wiki iliyopita, cheche za maneno kuhusu kashfa hiyo zilikuwa zimeanza kutulia wakati wakuu wa Chama cha Jubilee akiwemo Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale walipotaka wanachama wakome kumshambulia Dkt Matiang’i.
Mambo yalibadilika punde baada ya Bw Odinga kujitokeza na madai yake, na kutifua upya kivumbi kuhusu dhahabu feki.
Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika, ambaye aliandamana na Dkt Ruto mjini Naivasha, alishangaa ni kwa nini wale ambao wamehusishwa na sakata hiyo hawajaitwa kwa DCI kuandikisha taarifa, akidai hiyo ni ishara ya ubaguzi.
“Ikiwa DCI imejitolea kupigana na ufisadi na haifanyi hivyo kwa ubaguzi, wale ambao wametajwa kuhusika katika sakata ya dhahabu feki waende wakaandikishe taarifa,” akasema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichung’wa alipuuzilia mbali madai ya Bw Odinga kwamba ndiye aliyefichua utapeli uliokuwa ukiendelea.
“Mwarabu ana ghadhabu kuhusu dhahabu yake na anataka waliohusika waadhibiwe,” akasema.
Kwa upande mwingine, viongozi wa ODM walimtetea Bw Odinga dhidi ya makombora kutoka kwa Dkt Ruto na wandani wake.
Jana, Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi aliwakashifu wanasiasa kwa kuingilia kazi za asasi za upelelezi.
Alitaka DCI, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zipewe nafasi kufanya kazi zao.
“Ikiwa wameshindwa na wajibu wao wa kuleta maendeleo kwa Wakenya, wasiingilie kazi za DCI George Kinoti na DPP Noordin Haji,” Bw Kingi akasema.