WAKILISHA: Uvumbuzi wake utaokoa misitu
Na PAULINE ONGAJI
UKATAJI miti ni mojawapo ya mambo ambayo yamezidi kuchangia uharibifu wa mazingira.
Na katika maeneo mengi ambapo tatizo hili limekithiri, uharibifu huu wa misitu hutokana na shughuli za kutafuta kuni.
Hii ni mojawapo ya sababu zilizomsukuma Lawrence Kaburu kuvumbua jiko la kipekee kwa jina eco-stove.
Jiko hili lina sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na tanuu, pangaboi na mtambo maalum wa kubadilisha joto na limeundwa kwa safu ya chuma na udongo kidogo.
Kinachofanya chombo hiki kuwa na faida zaidi katika mazingira ni kwamba hakitumii kuni, na badala yake kinatumia jiwe maalum ambalo laweza kutumika upya kwa miezi na hata miaka.
Kuhusu jiwe hili, anasema kwamba bado hajajua jina lake kamili ambapo anapangiwa kukutana na mwanajiologia atakayemwambia iwapo lina jina la kisayansi.
“Nililipeleka katika Wizara ya Uchimbaji Madini na Petroli ambapo walilifanyia uchunguzi,” anasema.
“Nimekumbana na baadhi ya watu wanaochoma mahindi ambao wametambua sifa zake lakini hawana haja ya kujua kwa nini. Mawe haya ni mengi na mara nyingi yanaonekana kama uchafu na hivyo kuyafanya kutumika katika ujenzi wa kingo za kuzuia mmomonyoko wa udongo (gabions), au kuweka msingi wakati wa ujenzi wa barabara,” anasema.
Kulingana naye, pindi jiko hili linapoashwa, huendelea kuwaka kwa viwango vya juu vya halijoto, bila kutoa moshi ambapo waweza kulitumia kwa kati ya miezi saba na miaka minne pasipo kutumia mawe mengine.
“Kutokana na sifa hii, jiwe hili lina uwezo wa kusaidia kuhifadhi misitu, kumpa nguvu mtoto msichana kwani katika jamii nyingi ni yeye hukumbwa na jukumu la kwenda msituni kutafuta kuni, na hivyo kubadilisha maisha ya wengi,” anaeleza.
Kwa sasa jiko hili ni la bei ghali.
“Naliuza kwa Sh12,000. Kilichofanya jiko hili kuwa ghali mwanzoni ni kwamba nilikuwa nikijiundia mimi mwenyewe, wakati ambapo sikuwa nimeimarisha usanifu wake wa kiufundi. Lakini muda unavyozidi kusonga, tunapanga kutoa idhini ya chombo hiki kuundwa kwingineko baada ya kupata haki ya kuzuia kisiigwe (patent),” anaeleza, huku akiongeza kwamba tayari ameshapata wateja wawili wa eneo la Kilifi.
Kukabiliana na uchafuzi wa mazingira
Bw Kaburu ambaye ana shahada ya uhandisi katika masuala ya kemikali na kwa sasa anasomea shahada ya uzamili katika masuala ya sayansi ya mazingira, anasema mojawapo ya sababu zake kuunda jiko hili ni kukabiliana uharibifu wa misitu, tatizo ambalo limekumba hasa mataifa yanayostawi, Kenya ikiwa miongoni mwayo.
Pia ni uvumbuzi ambao umechangiwa pakubwa na masomo yake chuoni.
“Kwa mfano nikiwa katika mwaka wangu wa tano nikisomea shahada yangu ya kwanza, nilisanifu mtambo wa kupitisha joto kutoka uowevu mmoja hadi mwingine (heat exchanger),” anaeleza.
Aidha, amejifunza kuhusu mabadiliko ya hali ya anga na ongezeko la joto duniani, sera za masuala ya nishati miongoni mwa mambo mengine.
Ni uvumbuzi ambao bila shaka unapaniwa kuimarisha sio tu maisha ya watu hasa katika sehemu za mashambani, bali pia kuhifadhi mazingira. Lakini hili litaafikiwa tu iwapo atakabiliana na changamoto ambazo amekuwa akikumbana nazo katika shughuli hii.
“Changamoto kuu ni ukosefu wa ufadhili, suala ambalo linaathiri kasi yangu ya kuimarisha jiko hili. Hii imenilazimu kujihusisha na biashara zingine ili kufadhili shughuli zangu za kuunda mitambo mingine, vile vile kuimarisha usanifu wake taratibu,” anaeleza.