MAPOZI: Philip Makanda
Na PAULINE ONGAJI
KILA unaposikia baadhi ya nyimbo maarufu humu nchini; hasa za kizazi cha sasa, basi kuna uwezekano kwamba huenda zimepitia mikononi mwake.
Kwa takriban miongo miwili, Philip Makanda au Philo kama anavyofahamika miongoni mwa mashabiki, amehusika pakubwa katika sekta ya burudani humu nchini, mwanzoni kama mwanamuziki, kisha kama produsa.
Yeye ni mwanzilishi na mmiliki wa studio ya Mainswitch, inayofahamika kwa kuturekodia baadhi ya kazi safi. Amerekodia baadhi ya wasanii mashuhuri nchini Kenya na mbali, huku kazi zake zikipata umaarufu.
Mojawapo ya masuala ambayo yamemweka kwenye kilele cha orodha ya maprodusa maarufu nchini, ni ubunifu wake.
Aidha, anasifika kwa uwezo wake wa kutobagua aina ya muziki au wasanii anaofanya kazi nao.
Ndiposa kazi yake inahusisha kufanya kazi na wasanii wa muziki wa injili na hata wa nyimbo za kilimwengu.
Baadhi ya nyimbo ambazo amezifanyia kazi ni pamoja na albamu nzima ya Utamu wa Maisha yake mwanamuziki Daddy Owen, inayojumuisha kibao cha kichwa hicho hicho, alichoimba kwa ushirikiano na Juliani, vilevile Kipepeo, Huu Mwaka na Kioo zake Jaguar.
Ustadi wake umedhihirika kupitia orodha ndefu ya wasanii wa haiba ya juu ambao amefanya nao kazi. Humu nchini amefanya kazi na wanamuziki kama vile Daddy Owen, Jaguar, Nameless, Redsan, Amani, Vivian, Janet Atieno, G-kon, Kidis, MOG, Papa Dennis na Big Pin.
Nje ya mipaka
Barani Afrika anajionea fahari kufanya kazi na wasanii kama vile Iyanya kutoka Nigeria na Mafikizolo wa Afrika Kusini.
Safari yake katika uwanja wa burudani ilianza miaka 17 iliyopita kama mwanamuziki, wakati huo akiwa mwanachama wa bendi ya muziki ya Boomba Clan.
Pamoja na wenzake kwenye kikundi hicho walifahamika hasa kwa vibao kama vile Chonga Viazi na African Timer.
Ni hapa ndipo kiu ya kutaka kujihusisha na muziki kiliiongezeka, nia ikiwa kuwa produsa.
Kwa hivyo fursa ilipojitokeza, pamoja na wenzake hawakusita kujaribu bahati yao katika fani ya kurekodi. Huku wenziwe wakifuata mkondo wa kurekodi video, aliamua kujitoma katika masuala ya sauti.
Msisimko huu ulimpeleka katika lebo ya Ogopa, kampuni aliyoifanyia kazi kwa muda mrefu na kumpa fursa ya kuhusika katika kurekodi baadhi ya nyimbo maarufu.
Hii ilikuwa hadi mwaka wa 2012 alipoamua kushika hamsini zake na kuzindua rasmi studio ya Mainswitch.
Huu ulikuwa mwanzo wa safari yake kama produsa binafsi na mumliki wa studio, na hivyo kufungua mfereji wa ufanisi ambao ulimkutanisha na baadhi ya wadau maarufu katika sekta ya burudani.
Weledi wake katika fani hii umehimiliwa na kisomo chake katika taaluma hii ambapo amesomea shahada ya digrii ya mifumo ya habari na teknolojia (Information Systems and Technology) kutoka chuo kikuu cha USIU.
Haina shaka kwamba Philo amejiundia jina kama mmoja wa maprodusa wanaojulikana nchini.
Lakini swali kuu ni iwapo atafanikiwa kuzidisha mng’ao huu na kuendelea kuvuma sio kutokana na kazi zake za zamani, bali zijazo, tofauti na baadhi ya maprodusa waliomtangulia ambao mwanzoni walibisha kwa kishindo, ila wakaja kufifia wasijulikane waliko kwa sasa.