Michezo

WAFALME: Zamalek mabingwa wa CAF Confederations Cup

May 28th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

ALEXANDARIA, MISRI

KOCHA Christian Gross wa Zamalek SC alikuwa mwingi wa sifa kwa masogora wake baada ya kuyazima makali ya Renaissance Berkane na kunyanyua Kombe la Masharikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) msimu huu.

Zamalek walisajili ushindi wa 1-0 katika mkondo wa pili wa fainali uwanjani Borg el Arab, Alexandria na hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 1-1 baada ya kupigwa kwa mechi za mikondo miwili.

Ililazimu mwamuzi wa mechi kutafuta mshindi wa kupitia mikwaju ya penalti iliyoshuhudia Berkane wakipoteza tuta la kwanza na hivyo kuwapa Zamalek fursa ya kusajili ushindi wa 5-3.

“Ilikuwa tija na fahari tele kuwaangusha miamba Berkane, hasa mbele ya umati mkubwa wa mashabiki wa Zamalek jijini Alexandria,” akasema Gross.

Ushindi kwa Zamalek ulimaanisha kwamba kikosi hicho kinakomesha ukame wa miaka 16 bila ya taji lolote la CAF kabatini mwao. Bao la pekee katika kipindi cha kawaida cha mchezo huo lilifumwa wavuni kunako dakika ya 55 kupitia penalti ya Mahmoud Alaa iliyohitaji kutathminiwa mwanzo na teknolojia ya video ya VAR.

Awali, refa Bamlak Tessema Weyesa wa Ethiopia alikuwa amepuuza kilio cha Zamalek kutaka kupokezwa mkwaju wa penalti baada ya Najji Larbi wa Berkane kuonekana akiunawa mpira.

Alaa alifuma wavuni penalti hiyo na kuamsha wingi wa hisia zilizotamalaki kipindi cha pili cha mchezo huo. Iwapo Berkane wangalifunga bao la kusawazisha, basi wangalitia kapuni ubingwa wao wa kwanza wa CAF katika historia ya kivumbi hicho.

Zamalek walilazimika kutegemea ukubwa wa tajriba na uzoefu mkubwa wa mabeki wao pamoja na kipa Mahmoud ‘Gennesh’ Abdel Rahim ili kulazimisha kupigwa kwa penalti mwishoni mwa mchuano huo.

Berkane walikamilisha mchuano huo wakiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya kurejelewa kwa video ya VAR kuonyesha kwamba kiungo Omar Nemsaoui alikuwa amempiga kumbo Mahmoud Kahraba; na hivyo kulishwa kadi nyekundu.

Khalid Boutaib aliwafungia Zamalek penalti ya kwanza kabla ya Hamadi Laachir wa Berkane kupiga nje kombora lake. Mabao mengine ya Zamalek yalijazwa kimiani kupitia kwa Alaa, Abdallah Gomaa, Youssef Ibrahim na Ayman Sayed.

Ushindi wa Zamalek uliendeleza msururu wa mafanikio ya klabu za Kaskazini ya Afrika ambazo kwa sasa zinajivunia kutwaa ubingwa wa Kombe la Mashirikisho mara 11.

Katika fainali ya Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League), Wydad Casablanca na mabingwa watetezi Esperance ya Tunisia waliambulia sare ya 1-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Ijumaa uwanjani Rabat.

Wachezaji wawili wa Ivory Coast – Fousseny Coulibaly wa Esperance na Cheick Comara wa Wydad walifunga mabao mawili katika mchuano huo ulioshuhudia teknolojia ya VAR ikitumiwa mara mbili kuhesabu magoli yenyewe.

Mkondo wa pili utaandaliwa mwishoni mwa wiki hii huku Wydad wakipania kulipiza kisasi dhidi ya Esperance waliowapepeta kwenye fainali ya 2011.