Habari

Mvua yasababisha vifo na kuharibika kwa mali Pwani

May 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

MVUA kubwa ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika kanda ya Pwani imesababisha maafa ya watu watatu na kuwaacha wakazi zaidi ya 600 bila makao.

Vilevile, visa 30 vya kuendesha vimeripotiwa jijini Mombasa katika muda wa wiki moja kufuatia mvua hiyo.

Athari hizo za mvua zimeripotiwa katika kaunti tofauti za eneo la Pwani ambapo mvua imekuwa ikinyesha kwa kiwango kikubwa.

Kulingana na ripoti kuhusu athari za mvua hiyo iliyotolewa na serikali ya Mombasa, wawili kati ya wale waliofariki ni mwanamume ambaye alisombwa na maji eneo la Kadzandani na mwanamke ambaye alianguka kwenye shimo la choo eneo la Bamburi.

Mshirikishi wa kanda ya Pwani John Elungata amesema kuwa mtu mwingine alifariki eneo la Kaloleni kwa sababu ya mafuriko katika kaunti hiyo ya Kilifi.

Bw Elungata amesema kuwa wakazi 502 wameachwa bila makazi katika maeneo ya Vanga, Mangwei, Kikoneni na Kiweku kaunti ya Kwale.

Aidha, katika kaunti ya Lamu, Bw Elungata amesema kuwa nyumba mbili zilianguka na nynegine 25 kuzingirwa na maji ya mvua.

Waziri wa Ugatuzi wa Kaunti ya Mombasa Seth Odongo amesema Jumanne kwamba katika Kaunti ya Mombasa, watu 156 waliachwa bila makao wengi wakiwa wakazi wa maeneo bunge ya Kisauni na Nyali.

Waziri wa Ugatuzi wa Mombasa, Seth Odongo. Picha/ Kevin Odit

Katika eneobunge la Changamwe, Dkt Odongo amesema kuwa ukuta ulianguka na kuwacha wengi na majeraha. Majeruhi hao walitibiwa katika hospitali kuu ya mkoa wa Pwani.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa afya kaunti ya Mombasa Shem Patta alisema kuwa visa vya kuendesha viliripotiwa katika vituo vyao viwili ambavyo vimeekwa kupambana na tatizo ya mkurupuko wa kipindupindu.

“Visa zaidi ya 14 viliripotiwa katika kituo chetu cha Mwembe Tayari na vyengine 15 kuripotiwa katika kituo cha Bamburi. Kufikia sasa hakuna kisa cha kipindupindu ambacho tumepata kutokana na vile ambavyo vimekishwa katika afisi zetu,” amesema Dkt Patta.

Ameongeza kuwa zahanati nne zimefungwa katika maeneo tofauti ya kaunti ya Mombasa ili kuzuiwa mkurupuko wa kipindupindu.

Vituo hivyo ni pamoja na kile cha Ziwa la Ngombe, Maweni, Jomvu Model na Magongo. Zahanati hizo zinapatikana katika maeneo ya Kisauni, Changamwe na Jomvu.

Kukabili changamoto

Dkt Patta amesema kuwa tayari mikakati imewekwa ili kuyatibu maji ya matumizi ya nyumbani.

Wakati huo huo, serikali hizo za kitaifa na ile ya kaunti zilisema kuwa tayari zimeanza mipango ya kukabiliana na changamoto ambazo zinakumba wakazi wa maeneo ya Pwani.

Bw Elungata alisema kuwa vyakula pamoja na bidhaa nyengine za matumizi tayari vimeanza kupelekewa waathiriwa.

Serikali ya kaunti ya Mombasa kwa upande wake ilisema kuwa inashughulikia mitaro ya maji taka ambayo yamepelekea kushuhudiwa kwa mafuriko wakati wowote kunyeshapo.

Mvua kubwa imekuwa ikishuhudiwa katika eneo la Pwani kwa muda wa wiki mbili mfululizo sasa.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa ilikuwa imetabiri kuwa mvua kubwa ya idadi ya 30mm hadi 40 mm itashuhudiwa eneo hilo.