• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:10 PM
Waterworks FC yajiandaa kutetemesha ligi msimu ujao

Waterworks FC yajiandaa kutetemesha ligi msimu ujao

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya Waterworks FC sasa imepania kushusha ujuzi wake kwenye kampeni za michezo ya kuwania taji la Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao.

Waterworks FC inasadiki kwamba itakwenda kushindana wala siyo kushiriki tu hali inayotarajiwa kuzua ushindani mkali.

Wanasoka hao wameendelea kufana baada ya kumaliza ya kileleni kwenye mechi za Kundi A kuwania taji la Nairobi Regional League (NWRL) msimu huu.

Waterworks ilinasa tiketi ya kusonga mbele baada ya kumaliza kidedea kwa alama 27, tatu mbele ya Al Swafaa FC sawa na Nairobi Prisons, baada ya kukomoa Al Swafaa FC mabao 2-1 yaliyojazwa kimiani na Enock Momanyi.

Al Swafaa iliyopigiwa chapuo kubeba taji hilo ilishindwa kutimizwa azma yake dakika za mwisho ilipodungwa goli 1-0 na Nairobi Prisons baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 na Kibera Saints wiki iliyopita.

”Hatuna lingine tulikubali yaishe maana kwenye mechi hizo mbili tulikosa huduma za wachezaji sita tegemeo waliokuwa wameshikika shuleni,” kocha wa Al Swafaa FC, Charles ‘Stam’ Kaindi alisema na kuongeza kwamba yote wameachia Mungu kusaidia kupatikana kwa nafasi ya kusonga mbele msimu ujao.

Itakumbukwa msimu uliyopita maofisa wa Waterworks walinukuliwa wakisema wamepania kuendeleza mtindo wa kufanya kweli bila kushiriki ligi yoyote kwa zaidi ya msimu mmoja.

”Katika mpango mzima tunalenga kuhakikisha tunashiriki ligi kwa msimu mmoja na kubeba ubingwa ili kufuzu kupandishwa ngazi,” kocha wa kikosi hicho, Anthony Nderitu alisema na kuongeza kwamba wana imani tosha watafaulu kutimiza malengo yao huku wakiendelea kukuza talanta za wachezaji chipukizi.

Kikosi hicho kimeundwa na wachezaji ambao asilimia kubwa yao wamekuwa wakisakatia timu ya Ulinzi FC ambayo hushiriki soka la Ligi Kuu ya SportPesa nchini.

Bila mapendeleo wala kuongeza chumvi wanasoka hao huonekana wamekula fiti pia hushiriki mazoezi ya pumzi na stamina ili kujiweka vizuri kugaragaza gozi ya ngombe.

”Unajua nini kusema kweli wachezaji wengi ambao huchezea vikosi vinavyoshiriki soka la ligi za mashinani huandamwa na tatizo la kukosa pumzi hali na kutokuwa fiti michezoni,” meneja wa kikosi hicho, Fredrick Omondi alisema na kuongeza kuwa kwa wachezaji wa timu hiyo lazima wachape zoezi la pumzi.

Waterworks FC ilipandishwa ngazi kushiriki kipute hicho msimu huu ilipoibuka wafalme wa Ligi ya Kaunti ya FKF, Tawi la Nairobi West msimu uliyopita.

Kikosi hicho kilikomoa Kibera Saints mabao 4-0 katika fainali iliyopigiwa Uwanja wa Railway Training Institute (RTI), Nairobi. Timu hiyo ilishiriki mchezo huo baada ya kuibuka ya kwanza kwenye mechi za Kanda B Ligi ya Kaunti.

Meneja huyo alikiri kwamba wanafahamu bayana shughuli zito wanazotarajia kukutanishwa nazo kwenye mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Pili. ”Tunafahamu kipute hicho kinashuhudia ushindani mkali lakini vijana wangu wapo tayari kukabili upinzani wowote bila kulegeza kamba,” ofisa huyo alisema.

Aidha alipongeza maofisa wa FKF, Tawi hilo katika kile alichosema uongozi mwema na kutobeba timu zinazohusiana na viongozi wa shirikisho hilo.

Hata hivyo aliwataka waendeleze mtindo huo na kuzingatia zaidi mikakati ya kuipaisha soka la Kenya kutoa fursa kwa wachezaji wengi kuiva michezoni. Kadhalika alisema mafanikio hayo yatachangia wanasoka wengi kusajiliwa kushiriki soka la kulipwa katika mataifa.

You can share this post!

Kahawa Queens yaanza ligi mpya vyema

Foleni ya kilomita 12 wanandoa wakisaka talaka za haraka

adminleo