• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
MAPITIO YA TUNGO: Sikitiko la Sambaya; Riwaya inayoakisi ukweli wa ‘mui huwa mwema’

MAPITIO YA TUNGO: Sikitiko la Sambaya; Riwaya inayoakisi ukweli wa ‘mui huwa mwema’

Mwandishi: Jeff Mandila

Mchapishaji: Jomo Kenyatta Foundation

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Riwaya

Jina la Utungo: Sikitiko la Sambaya

Kurasa: 142

NI riwaya ya kimkasa, inayoonyesha kwamba mui hatimaye huwa mwema na mvumilivu hula mbivu.

Ndio ujumbe mkuu anaowasilisha mwandishi Jeff Mandila kwenye riwaya hii ya kusisimua ‘Sikitiko la Sambaya.’

Hadithi katika riwaya hii inawarejelea wahusika wakuu, wasichana Sambaya na Linda, ambao ni wanafunzi katika Shule ya Mseto ya Mtakatifu Maria Makorongo.

Hata hivyo, kuna mpaka mkubwa kati yao.

Linda anatoka katika familia maskini sana, huku mwenzake Sambaya akitoka katika familia ya kitajiri.

Mpaka mwingine uliopo ni wa kimwenendo, ambapo Sambaya ni msichana mtukutu asiye mwadilifu kitabia, huku mwenzake Linda akiwa mwenye nidhamu kubwa.

Kwa utambuzi huo, walimu wao, Bi Wema na Bi Vunana wanajaribu kuwapa mwongozo kuhusu hatari mbalimbali zinazowaandama wanafunzi wa kike, hasa mahusiano ya kimapenzi.

Linda anazingatia nyaadhi hizo, ila Sambaya anazikaidi, pale anapoingia katika uhusiano wa kimapenzi wa Kijana Fwesa.

Awali, Sambaya alikuwa amehamishwa kutoka shule moja baada ya kupata mimba.

Kwa hayo, anatoroka shuleni na nyumbani kwao, ambapo anaolewa na mvulana huyo. Mikasa baada ya mikasa pia inaandama familia ya akina Sambaya, mojawapo ikiwa ni kifo cha babake, Abdul Machozi.

Mamake Sambaya, Bi Naumi, pia anaanza kuugua kutokana na mkasa unaoiandama familia yake.

Mkondo wa matukio unabadilika; ambapo baada ya kifo Bw Machozi, Bi Naumi pia anafariki kutokana na masaibu ambayo yanaikumba familia yake.

Ikumbukwe kwamba kwa kuzingatia mashauri ya walimu wake, Linda anafanikiwa sana maishani, ambapo mume wake ni mkurugenzi wa kampuni moja kubwa, huku mwenyewe akiwa na kazi nzuri sana.

Kutokana na watu waliomfaa wakati akiteseka, anaandika riwaya ‘Duniani Bado Mna Wema.’

Kwa upande wa Sambaya, hali inakuwa ya masikitiko na majonzi makuu. Fwesa anageuka kuwa mlevi chakari. Anamwachia majukumu ya kuwalea watoto wake.

Mtoto wake, Binti Kadogo pia anafariki katika kile kinaonekana kuwa malezi mabaya.

Mkasa mwingine unamwandama Sambaya pale mumewe anafariki katika ajali ya barabarani wakati akielekea katika uzinduzi wa riwaya ya Linda.

Tukio kuu riwayani ni wakati Sambaya pia anafariki katika hali ya kutatanisha, kifo chake kikiaminika kuchangiwa na Muronji Mpinga, aliyekuwa akimwonea gere pale mumewe (Mpinga) anaanza kuisaidia familia ya Sambaya.

Ingawa Muronji anahukumiwa kifo baadaye, tukio kuu ni kwamba kila mmoja anamsikitia Sambaya kutokana na yaliyomwandama.

Kijumla, mwandishi anafaulu kutumia baadhi ya mbinu za lugha kama barua, kiangaza mbele, kisengere nyuma, ndoto kati ya zingine kufanikisha kazi yake.

Ni riwaya yenye mafunzo tele, ila inayoishia kwa huzuni kubwa.

[email protected]

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Urasmishaji wa Kiswahili nchini Rwanda...

NDIVYO SIVYO: Mashimo shambani ‘huchimbwa makoongo’...

adminleo