Ujanja unaotumiwa na wafisadi kufilisisha serikali waanikwa
Na LEONARD ONYANGO
MAAFISA wa serikali na wafanyabiashara wenye ushawishi sasa wanatumia raia na kampuni za kigeni kuiba fedha za umma humu nchini, Taifa Leo Dijitali imeng’amua.
Kulingana na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji, wafisadi hao wanatumia mashirika feki kuomba kandarasi serikalini.
Wafisadi wanawashirikisha raia wa kigeni na kampuni za ughaibuni katika mtandao wa wizi wa fedha za umma kwa lengo la kuwakanganya maafisa wa uchunguzi.
“Shirika linahonga wajumbe wa kamati ya kutoa zabuni na kupewa kandarasi ambapo wanasambaza bidhaa au huduma duni.
“Tukilifuatilia shirika hilo unapata kwamba linamilikiwa na watu watatu. Mkurugenzi wa kwanza ni Mkenya, mkurugenzi wa pili ni raia wa kigeni na msimamizi wa tatu ni kampuni ambayo ikichunguzwa inabainika kwamba haina wafanyakazi wala ofisi na pia inamilikiwa na kampuni nyingine nyingi zikiwemo za ughaibuni,” akaelezea Bw Haji.
DPP alikiri kuwa kuchunguza kesi za ufisadi zinazohusisha raia au kampuni za kigeni huwa vigumu hivyo kufanya kesi kukosa ushahidi wa kutosha.
“Ili kutaka kampuni ya kigeni ichunguzwe si kazi rahisi. DPP analazimika kuandikia barua afisi ya Mkuu wa Sheria (AG) wa Kenya ambaye baadaye pia anaandikia barua Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kenya.
“Waziri wa anapeleka barua hiyo kwa balozi wa nchi husika humu nchini. Balozi wa nchi hiyo anatuma barua hiyo kwa Mkuu wa Sheria wa taifa la mshukiwa. Mkuu wa Sheria anamkabidhi Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye atatakiwa kwenda kortini kuomba mshukiwa achunguzwe,” akaelezea Bw Haji.
Mkurugenzi wa mashtaka alisema baada ya kulipwa fedha, kampuni hizo hutoa kwenye benki hela zote na kuzipakia kwenye mafurushi na kisha kuzisafirisha nje ya nchi.Bw Haji, hata hivyo, alisema kuwa abuni mbinu za kukabiliana na maafisa wa serikali na wafanyabiashara wakora wanaotumia raia wa kigeni kuiba fedha za walipa ushuru.
Bw Haji alifichua hayo alipokutana na viongozi wa kidini katika hoteli ya Serena, Nairobi huku akiwa ameandamana na Mkurugenzi wa Idara ya Upepelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak kati ya maafisa wengineo.
Sakata za ufisadi ambazo zimehusisha raia na kampuni za kigeni ambazo zimempa kibarua kigumu Bw Haji kuchunguza ni ile ya wizi wa mamilioni ya fedha zilizolipwa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror Dam katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Bw Haji, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari mnamo Machi, alisema kampuni ya CMC Di Ravenna ya Italy tayari imelipwa Sh21 milioni na hivyo afisi yake itahitaji ushirikiano wa kimataifa kuwafichua wamiliki wa kampuni hiyo.
Kampuni ya CMC Di Ravenna imewasilisha kesi mahakamani nchini Italy ikitaka itangazwe kuwa imefilisika.
Viongozi wa kidini wakiongozwa na Kiongozi wa Kanisa la Anglikana Jackson Ole Sapit walisema wanataunga mkono vita dhidi ya ufisadi.
“Tunawasihi waumini kujiepusha na ufisadi na wanasiasa wakome kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi,” akasema Askofu Mkuu Sapit.