• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
WANDERI: Utamaduni wa Mwafrika tiba ya matatizo ya ndoa

WANDERI: Utamaduni wa Mwafrika tiba ya matatizo ya ndoa

Na WANDERI KAMAU

MIMI bado sijaoa. Ningali kapera. Sababu yangu kuu kutokuwa katika ndoa si kwa kukosa mchumba, kutokuwa ‘mwanamume kamili’ au kutoipenda ndoa; nazingatia tu ushauri wa babu yangu kwamba ndoa haina pupa.

Naam, ndoa ni taasisi muhimu ambayo lazima iwekewe msingi ufaao. Wanandoa wanaodhamiria ama kupanga kuishi pamoja lazima wafahamiane kwa undani kabla ya kufikia uamuzi wa kuwa mume na mke. Huu ndio wosia niliopewa na babu yangu.

Natoa urejeleo huu kutokana na ongezeko la visa vya mauaji miongoni mwa wanandoa, ambavyo vinashtua. Vinaogofya na kutia kiwewe, hasa miongoni mwa wale wanaopanga kuanza maisha ya ndoa.

Katika utoto wangu, miongoni mwa siku tulizotamani sana kama wavulana wa kuchunga mifugo ni wakati wowote ambapo tungefahamu kuwa kuna harusi kijijini mwetu. Tulifurahi. Tulifahamu kwamba chakula kingekuwa kwa wingi. Si kwetu pekee, mbali hata kwa mbwa wetu ambao tuliwatumia kuwinda.

Hafla ya harusi ingekuwa kama Siku ya Masihi Yesu kurudi duniani. Kila mmoja kijijini alikuwa na nafasi ambayo alifurahia. Pengine walioomboleza tu ni ng’ombe, kondoo ama kuku waliochinjwa.

Akina mama walifurahia kuwapikia wageni jikoni. Wasichana walijiunga na mama zao kujifunza kupika na kuchota maji.

Wazee wangeshiriki katika utengenezaji jukwaa ambalo lingetumiwa kuendeshea harusi. Wavulana nao walifurahia kubeba vyakula kupeleka mahali ambapo akina mama wangewapakulia wageni wa bwana na bi harusi, ilmradi kila mtu alifurahi. Mbwa walisherehekea makombo ya vyakula yaliyotupwa. Ilikuwa furaha kuu!

Hata hivyo, furaha hiyo imekuwa kinaya. Vifo, vifo! Kila siku vifo! Usaliti! Unyama na ukatili! Maisha ya ndoa yamegeuzwa Jehanamu ya Kidunia! Kunani?

Wanaouana ni watu waliopendana walipoamua kuoana. Upendo wao ukawa mapenzi; mapenzi nayo yakageuka kuwa mahaba makubwa ambayo yaliwaunganisha.

Baadhi ya wanaouana walifanya harusi kubwa za kifahari. Waliwaita jamaa na marafiki. Wakaenda fungate katika maeneo ya mbali—mapenzi kati yao yalisheheni hali ya kujaliana. Walikuwa wapenzi wa kweli mbele ya Mungu na binadamu.

Sijui kiini cha usaliti huu, lakini nahisi kuna nuksi. Kuna sababu halisi ya hali hii kuwepo. Haiwezi kutokea tu. La hasha!

Kwanza, lazima tujilaumu wenyewe kwa hali hii iliyojaa ushetani na ubinafsi. Naam, tunajipenda! Tumejaa ubinafsi na kutaka kutambulika. Mke anataka ‘atambulike’ na mumewe; mume naye anataka kuonekana kama ‘shujaa’ kwa mkewe. Matokeo yake ni mikwaruzano inayozaa majeraha na vifo visivyotarajiwa.

Kinyume na ilivyokuwa katika maisha ya vijijini, kila mmoja anajitakia makuu. Wanakijiji walipendana. Waliheshimiana. Walijaliana na kuthaminiana.

Linalohitajika kwa sasa ni kila mmoja katika jamii kutathmini tuelekeako. Je, mustakabali wa ndoa ni upi? Katika uumbaji wake, Mungu aliiweka ndoa kama msingi mkuu wa kuendelea uumbaji huo. Je, mwanadamu hatimaye amevunja mpango huo?

Naamini kuwa hilo si gumu, ikiwa sote tutapunguza mtindo wa kujivika maisha na mitindo ya usasa. Uafrika ndio msingi mkuu utakaorejesha hadhi iliyoyaandama maisha ya ndoa.

[email protected]

You can share this post!

NGILA: Tutumie Microsoft kujifua na kuvumisha teknolojia...

ONYANGO: Tangatanga wasionewe, sote hutoa hela chafu...

adminleo