• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:44 AM
AKILIMALI: Mwajiri wake amempa ardhi ajipige jeki kwa kilimo

AKILIMALI: Mwajiri wake amempa ardhi ajipige jeki kwa kilimo

Na LUDOVICK MBOGHOLI

KIJANA Raphtone Lamangwa kutoka eneo la Mkanambio huko Laikipia anafanya kazi ya kupanda, kukuza, na kulinda miembe michanga sawa na kuwa mlinzi wa mimea mingine ya matunda ya mwajiri wake eneo la Mombasa.

Kabla ya kutoka Laikipia kuja Mombasa asema aliacha ufugaji akaanza mchakato mpya kwa kuajiriwa, kabla ya kujitosa upya kwenye shughuli za ukulima kujiendeleza kimaisha.

Kijana huyu amekuwa maarufu katika eneo la wakulima wa Kimijikenda la Utange, kwa kupiku umaarufu aliokuwa nao katika eneo la Nyali alikoajiriwa kazi ya ulinzi na kampuni ya Nakumatt.

Lamangwa, 30, sasa anajikakamua kwenye shughuli binafsi za ukulima katika shamba la mwajiri huyo huko Shanzu.

“Hivi sasa nalima mazao ya vyakula katika kipande hiki cha shamba lenye rutuba, nilichopewa na mwajiri waangu,” anapasha kijana huyu.

Lamangwa asema anaridhika na shughuli ya ukulima akidai ndiyo itampa faida kubwa sawa na mapato ya kutosheleza mahitaji yake siku za usoni.

“Uhuru niliopewa na mwajiri wangu ni dhihirisho la imani aliyonayo kwangu, kutokana na jinsi ninavyomtunzia mali. Anaridhishwa na jinsi nilivyohudumia wateja waliofika shambani awali wakitaka kununua matunda na mboga, kwani niliwauzia kwa bei ya kuridhisha,” alidai kwenye mahojiano yake na Akilimali alipotembelewa shambani.

Hata hivyo, anasema kwa kuipa kisogo itikadi ya ufugaji, anaendeleza juhudi za kupata riziki kwa kuwekeza nguvu nyingi kwenye ukulima wa kujitegemea.

“Lengo langu ni kuboresha ukulima wa mazao ya nafaka na mboga kama mahindi, maharagwe, pojo, mbaazi, na hata kukuza mihogo na viazi,” anasema Lamangwa.

“Vijana wenzangu wa Kimaasai wanazingatia ufugaji wa kuhamahama na kusahau ardhi zetu pia zinafaa kwa ukulima sawa na ardhi zinazomilikiwa na jamii nyingine, zinazotumiwa kwa ukulima wa mazao,” anasema Lamangwa akiwashauri vijana wenzake.

Ingawa anajishughulisha na ukulima wa mazao ya vyakula mjini Mombasa, angali anatii itikadi ya jamii ya Wamaasai.

“Ni lazima tuzingatie mila, tamaduni na desturi zetu. Lakini ndoto yangu itakapofanikiwa, nitarejea nyumbani Laikipia nikiwa na ujuzi wa kutosha wa ukulima wa kisasa ambao nitautumia kama somo la kijamii kwa vijana wenzangu,” anadokeza.

Asema tajriba anayopata kwenye ukulima mjini Mombasa pia itamwezesha kubuni kilimo mseto huko Laikipia, akizingatia ufugaji, ukulima wa mazao ya nafaka, mboga na matunda.

“Nitafanya hivyo nikinuia kuboresha mradi muhimu wa kilimo biashara kwa manufaa ya vijana wa jamii yangu yenye utamaduni wa ufugaji wa kuhamahama,” anasema.

Lamangwa anakiri idadi kubwa ya vijana wa Kimaasai inazingatia mno itikadi ya kitamaduni ya ufugaji wa kuhamahama, hali ambayo huenda ikawa chanzo cha wengi kukosa elimu bora. Hata hivyo anasisitiza hilo halifai kuchukuliwa kuwa kigezo cha jamii ya Kimaasai kushindwa kuboresha ukulima.

“Hatuna budi kujitolea kukuza mazao ya vyakula kibiashara sawa na shughuli tulizozoea za ufugaji mifugo.

“Endapo tutashirikiana na wazee, siku za usoni jamii yetu inaweza kuimarika zaidi kwa maendeleo na ustawi wa ukulima.”

You can share this post!

AKILIMALI: Harufu tamu ya kahawa ‘tungu’ kibandani...

AKILIMALI: Tafuta soko, panda ‘mishirii’ hela zije...

adminleo