• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
AKILIMALI: Tafuta soko, panda ‘mishirii’ hela zije kimpigo

AKILIMALI: Tafuta soko, panda ‘mishirii’ hela zije kimpigo

Na CHRIS ADUNGO

MAHARAGWE aina ya Mishirii hunawiri sana katika eneo lenye mvua nyingi ya takriban milimita 750-1200 kwa mwaka. Hii ni sababu ya mmea wenyewe kuwa maarufu miongoni mwa wakazi wa Mikoa ya Kati na Bonde la Ufa.

Wakulima wengi wanaojihusisha na kilimo hiki hawahitaji kipande kikubwa cha ardhi kutokana na shughuli nyingi za kutunza maharagwe haya.

Mishirii ni mmea ulio na uwezo wa kuathirika kwa urahisi kutokana na mvua nyingi kupita kiasi au ukame uliozidi kiwango.

Uangalizi wa karibu ni jambo la kutiliwa mkazo kwani hii ni mimea ya kigeni inayohitaji ujuzi na kutegemea maarifa ya hali ya juu kuikuza.

Kabla ya mbegu kuota na kuanza kutoa maua, urushiaji dawa kwa ajili ya kuangamiza magugu na vidudu sugu huja kabla ya mengine.

Na kwa sababu mbegu hutiwa katika kina kirefu mchangani, zipo zinazoweza kukosa kuota kwa wakati.

Hivyo, mkulima hutakiwa kupitiza Lime Water kwenye mbegu zake kabla ya kuzipanda.

Hili huyeyusha maganda ya nje ya mbegu za Mishirii, zisigande.

Changamoto kubwa katika ukuzaji wa Mishirii ni gharama ya kazi inayomlazimu mkulima kuajiri idadi kubwa ya wasaidizi ili kuangalia na kukagua mimea ambayo huchukua kati ya siku 45-50 kukomaa.

Mwishowe maharagwe yenyewe yavunwe, yapakiwe katika magunia, yapepetwe kuondoa mawe na uchafu mwingineo.

Baadaye, hupakiwa kulingana na kilo zinazobebwa katika kila gunia kisha yakasafirishwa sokoni; wanunuzi wengi wakitokea ulaya kwa sababu ya bei yake ghali. Kilo moja ya Mishirii huuzwa kwa kati ya Sh1,500 na Sh2,000.

Katika kijiji cha Kimbimbi, eneo la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga, Akilimali ilikutana na mkulima John Mwarano ambaye jina lake ni maarufu sana miongoni mwa wanakijiji kutokana na kilimo cha maharagwe.

Mkulima John Mwarano akiwa katika sehemu ya shamba lake la maharagwe aina ya mishirii au kwa Kimombo ‘French beans’ katika eneo la Kimbimbi, Mwea, Kirinyaga. Picha/ Chris Adungo

Katika miaka ya themanini (1980s), alijihusisha sana na kilimo cha maharagwe ya aina mbalimbali, lakini changamoto za ukosefu wa soko miongoni mwa nyinginezo zikamzuia kukiendeleza.

Hata hivyo, ameanza upya kilimo hiki na anasema kinamfaa kutokana na ujira anaoupata. Japo anakuza pia maharagwe aina ya Rose Coco, yale ya Mishirii ndiyo anayoyapendelea sana. Mishirii ni maharagwe ya kawaida lakini ambayo hayajakomaa na bado yako kwenye maganda.

Maharagwe haya hutumika katika upishi wa vitoweo vya kila sampuli. Kulingana na Mwarano ambaye ni baba ya watoto wanne, yeye huwa anashiriki kilimo hiki katika sehemu za shamba lake la ekari moja na nusu.

Anasema maharagwe aina za Samantha na Teresa huwa yanahitajika sana katika masoko, na kwa hivyo wakulima wengi hupanda kwa wingi aina hizi mbili.

Pia maharagwe aina ya Mishiri yanaaminika kuwa kiwango cha juu cha protini na madini mengine.

Mara kwa mara, yeye huwa anazmia haja ya kutoa majani yasiyohitajika shambani huku akitilia dawa maharagwe yake kwa minajili ya kupigana na wadudu.

Anakiri kuwa maharagwe huhitaji maji kwa wingi kwa hivyo huwa inambidi kunyunyizia kila mara ili kuboresha kukua kwa zao lake.

Katika msimu mzuri wa mavuno kulingana naye, mmea mmoja wa maharagwe ya Mishirii una uwezo wa kutoa mazao ya hadi kilo mbili.

Aghalabu mavuno ya mmea huu huchukua muda wa hadi miezi miwili kukomaa huku mkulima akivuna mara mbili kwa wiki, lakini pia huwa inalingana na bidii za mkulima mwenyewe.

Kuhusiana na soko la bidhaa zake, kuna kampuni mbalimbali ambazo hununua mazao yake na kuuza nje ya nchi kwa faida kubwa haswa kule Ulaya.

Hata hivyo, kampuni hizo si nyingi kwa hiyo, kuna uhaba wa wanunuzi.

Mara nyingi, bei ambayo wakulima hununulia nayo maharagwe yake ni Sh200 pekee kwa kilo moja.

Kampuni

Wakulima wengi, anaendelea kusema, huwa wanafanya mpango na kampuni hizi ili wanapovuna, wafanyakazi wa kampuni huyajia mazao ya mahagarwe moja kwa moja kutoka shambani.

Mbali na uhaba wa masoko ya hapa nchini, changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa kampuni nyingi zinazonunua maharagwe kutoka kwa wakulima wa bidhaa hii kwa lengo la kuuza katika masoko ya nje.

Hili linazuia idadi kubwa ya wakulima kupanda mmea huu kwa wingi.

Mwarano anasema kilimo hiki kina umuhimu mkubwa kwake kwani kimemwezesha kuelimisha watoto wake mbali na kumwezesha kununua shamba na kujenga makazi ya kudumu.

Wito anaotoa kwa serikali kuu pamoja na ile ya kaunti ni kuelimisha na kuhamasisha wakulima kuhusu kilimo hiki.

Anasema ya kuwa wakulima wanahitaji mafunzo zaidi ili wajue mbinu za kisasa na za kiteknolojia za kufanya kilimo ili kupata mazao mengi.

Kulingana naye, wawekezaji wa nje wanastahili kuruhusiwa waje wawekeze kwa viwanda vya kuongezea thamani katika mazao ya maharagwe haya ili kufikia viwango vya mahitaji ya masoko ya kigeni.

You can share this post!

AKILIMALI: Mwajiri wake amempa ardhi ajipige jeki kwa kilimo

Kocha Migne ataja kikosi cha Harambee Stars tayari kwa AFCON

adminleo