Michezo

Bingwa wa Olimpiki Ruth Jebet adaiwa kutumia pufya

March 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Ruth Jebet, ambaye alibadili uraia na kuwa Mbahraini mnamo Februari mwaka 2013, anakabiliwa na tuhuma za kutumia dawa za kusisimua misuli kupata ufanisi mashindanoni.

Bingwa huyu wa Olimpiki mwaka 2016 wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji anashikilia rekodi ya dunia ya mbio hizi ya dakika 8:52.78 aliyoweka katika Riadha za Diamond League nchini Ufaransa mnamo Agosti 27 mwaka 2016.

Gazeti la Guardian nchini Uingereza linasema ripoti kadhaa zinadai kwamba Jebet, 21, amepatikana na kosa la kutumia dawa za aina ya EPO alizotumia bingwa wa marathon kwenye Olimpiki za mwaka 2016, Mkenya Jemimah Sumgong, ambaye sasa anatumikia marufuku ya miaka mine.

“Ingawa habari hizi hazijathibitishwa, duru kadhaa zimedai Jebet amefeli vipimo vya matumizi ya dawa za kusisimua misuli za aina ya EPO,” gazeti hilo liliripoti Machi 4, 2018.

Ikithibitishwa ni mhalifu wa dawa hizo haramu, atakuwa mzawa wa Kenya aliye na jina kubwa kuwahi kufeli vipimo hivyo.

Mzawa wa Kenya ambaye amewahi kupatikana na hatia ya kutumia uhalifu wa dawa za kusisimua misuli kupata ufanisi ni Abraham Kiprotich.

Mfaransa huyu alipigwa marufuku mwaka 2013 miaka miwili baada ya kupatikana alitumia dawa za kusisimua misuli za EPO kushinda mbio za Istanbul Marathon nchini Uturuki mwaka huo. Alipokonywa taji hilo.

Kiprotich aliruhusiwa kurejea mashindanoni baada ya kukamilisha marufuku yake. Alinyakua taji la Lagos Marathon nchini Nigeria mwezi Februari mwaka 2018 na kujishindia zawadi ya Sh5,065,500.