• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Matumizi ya viziada lugha katika sajili isiyo rasmi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Matumizi ya viziada lugha katika sajili isiyo rasmi

Na MARY WANGARI

KATIKA sajili isiyo rasmi, kuna matumizi ya viziada lugha mathalani kuashiria kwa vidole, kukonyeza jicho, kuonyesha uchangamfu au kukunja uso na kadhalika hutokea katika mazugumzo.

Matumizi ya viziada lugha husababishwa na mambo anuwai kama vile haja ya msemaji kutilia mkazo analosema, haja ya kuwavutia au kuwanasa wasikilizaji, hali ya kihisia ya mazungumzo, ikiwa pengine msemaji hana muda wa kutosha kusema aliyonayo, huwa ni jambo la kawaida kuambatanisha mazungumzo na matumizi ya viziada lugha.

Ukiukaji wa kanuni za kisarufi

Aghalabu kanuni za kisarufi hukosa kuzingatiwa sana katika mazungumzo ya kawaida.

Hali hii  husababishwa na ukweli kuwa kitu cha muhimu katika mazungumzo ya kawaida ni mawasiliano.

Mradi watu wanawasiliana na kuelewana, hata kwa kutozingatia kanuni za kisarufi, basi wahusika huridhika.

Isitoshe, ukosefu wa muda wa kufikiri, kupanga mawazo na kushughulikia kanuni za kisarufi huchangia hali ya kutotilia maanani kanuni na kaida za kisarufi.

Kusitasita

Ni nadra watu wanapozungumza kusema kwa mfululizo pasipo kusitasita.

Usemaji wa mfululizo huwa ni uwezo wa walumbi au msemaji anaposoma maandishi.

Katika mazungumzo ya kawaida, kusitasita hutamalaki.

Kusitasita kunaweza kusababishwa na: haja ya mzungumzaji kutaka muda wa kufikiria au kupanga mawazo anayotaka kutoa, mzungumzaji kutokuwa na uhakika wa anayokusudia kusema, kuwa na hisia kama vile kupandwa na hasira, hali ya kimaumbile ambayo watu wengine huwa nayo kama vile ugugumizi ambao huwafanya watu kusitasita.

Kubadilika kwa mada au maudhui

Mabadiliko haya hutokana na wahusika wa mazungumzo kukerwa au kutopendezwa na maudhui au mada fulani.

Iwapo mzungumzaji mmoja atazua jambo, ana uwezo wa kung’amua kama anawapendeza wenzake au anawachusha.

Ikiwa anawaudhi bila shaka patakuwa na haja ya mabadiliko ya maudhui.

Mabadiliko katika muktadha nayo husababisha mabadiliko ya maudhui.

Ukatizanaji kalima

Hali ya kukatizana kalima pia hujitokeza wahusika wanaposhiriki mazungumzo.

Ukatizanaji kalima husababishwa na ukosefu wa sheria au kanuni katika mazungumzo ya kawaida; ni nani anasema kwanza, atasema kwa muda upi na ni nani atamfuata.

Huenda linalosemwa na msemaji likamchoma au kumkera mwingine asiweze kuvumilia kumwacha akamilishe alisemalo.

 

[email protected]

 

Marejeo

Chiraghdin, S. & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.

You can share this post!

Rhonex, Tirop na Cheruiyot watwaa mataji Diamond League,...

Weupe wa Weke wasababisha farakano hafla ya harambee

adminleo