Michezo

Shujaa yaponea shoka kwenye Raga ya Dunia baada ya kuingia 8-bora Paris 7s

June 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MAOMBI ya Wakenya ya karibu wiki nzima kwa timu yao ya raga ya wachezaji saba kila upande kuepuka kuangukiwa na shoka kwenye Raga ya Dunia yamejibiwa baada ya Shujaa kuingia robo-fainali kuu kwa kuchapa Wales 26-21 katika mechi yake ya mwisho ya Kundi B nchini Ufaransa, Jumamosi.

Vijana wa kocha Paul Murunga, ambao pia wamenufaika na Scotland kubwaga Japan 22-21 katika mechi ya D, ilianza kampeni yake ya Paris Sevens kwa kugawana alama dhidi ya Australia baada ya kuandikisha sare ya 19-19.

Kocha Paul Murunga. Picha/ Hisani

Charles Omondi, Andrew Amonde na Bush Mwale walifunga miguso ya Shujaa katika mchuano huu, huku Johnstone Olindi na Michael Wanjala wakichangia mkwaju mmoja kila mmoja.

Kenya ilipata pigo katika mechi yake ya pili pale ilipokung’utwa 29-12 baada ya kuongeza 12-10 wakati wa mapumziko kupitia kwa miguso miwili iliyofungwa na nahodha Jacob Ojee na Amonde naye Wanjala akafunga mkwaju mmoja.

Katika mechi iliyohakikishia Kenya tiketi ya kusalia katika mashindano haya ya kila mwaka yanayojumuisha timu 15 kushiriki duru zote 10 pamoja na timu moja alikwa, Shujaa ilionyesha ujasiri wa aina yake pale ilipotoka chini alama 14-0 na kunyamazisha Wales 26-21.

Jeffery Oluoch, ambaye alikuwa nahodha wakati wa duru za Hong Kong na Singapore mwezi Aprili, pamoja na Mwale walipachika mguso mmoja kila mmoja, huku Nelson Oyoo akipata miguso miwili. Wanjala aliongeza mikwaju ya miguso mitatu.

Jeffery Oluoch. Picha/ Hisani

Kabla ya mechi timu za taifa za Chipu (wanaume Under-20), Simbas (wanaume watu wazima), klabu za Ligi Kuu ya Kenya zikiwemo Mwamba na Nakuru, nahodha wa timu ya soka ya Kenya ya Harambee Stars Victor Wanyama na Wakenya wengi tu, walijaza jumbe za kheri njema wakitakia Shujaa kukwepa shoka.

Wanyama, ambaye timu yake ya Tottenham Hotspur italimana na Liverpool katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya nchini Uhispania leo usiku, aliambia Shujaa, “Jitumeni na mtapata matokeo mazuri.”

Ushindi wa Shujaa dhidi ya Wales na Scotland kubwaga Japana kulihakikishia Wakenya msimu wa 18 mfululizo kwenye Raga ya Dunia. Kenya, ambayo imekuwa katika raga hii tangu msimu 2002-2003, sasa haiwezi kufikiwa na Japan.

Alama chache ambazo Kenya inaweza kuzoa jijini Paris ni 10.

Inamaanisha kwamba ikipoteza katika robo-fainali dhidi ya Marekani ya kocha Mike Friday itamaliza msimu na alama 37.

Japan iliingia duru ya Paris ikiwa na alama 25. Ikishinda mduara wa kutafuta nambari 9-16 almaarufu Challenge Trophy itajiongezea alama nane pekee.

Vita vya kuangukiwa na shoka sasa vimesalia kati ya Japan na Wales, ambayo ina alama 30. Wales itasalia katika raga hii ikishinda Canada katika robo-fainali ya Challenge Trophy baadaye Jumamosi usiku.