HANDISHEKI: Raila awaka
Na SAMWEL OWINO, PETER MBURU na VALENTINE OBARA
KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, amekasirishwa na jinsi wakuu wa chama hicho wameanza kuchukua misimamo inayokinzana na ya Serikali ya Jubilee.
Masuala ambayo yamemshikisha moto Bw Odinga ni hatua ya vigogo wa ODM kupinga uzinduzi wa noti mpya, pamoja na kusema kuwa handisheki haina maana iwapo referenda haitafanyika kufikia Machi 2020.
Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Odinga, ambaye alikuwa Uingereza aliwasiliana na baadhi ya viongozi wa chama hicho na kuwaamrisha waunge mkono uamuzi wa serikali kuzindua noti mpya.
Ni amri hiyo ambayo iliwafanya viongozi hao kuandaa kikao cha wanahabari jijini Nairobi jana na kubadilisha kauli yao kuhusu noti hizo.
Hapo wikendi, baadhi ya viongozi akiwemo Mwenyekiti John Mbadi, Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Kiongozi wa Wachache katika Seneti James Orengo walipinga noti hizo kwa msingi kuwa Katiba hairuhusu sarafu za Kenya kuwa na sura ya mtu yeyote.
“Kiongozi wa chama anataka kuwe na msimamo mmoja chamani kuhusu noti mpya. Wanachama wetu wamekuwa wakitoa maoni yanayotofautiana kuhusu suala hilo,” mwanachama mwenye mamlaka makubwa katika chama hicho aliyeomba asitajwe jina aliambia Taifa Leo.
Abadili msimamo
Jumanne, Bw Mbadi aliye pia Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa alilazimika kubadili msimamo wake wa awali.
Kwenye kikao cha habari alichoitisha katika makao ya Bunge, Mbunge huyo wa Suba Kusini alithibitisha kuwa vigogo wa chama walishauriana ndipo akapewa jukumu la kutoa msimamo halisi wa chama kuhusu suala hilo.
Kulingana naye, uamuzi wa ODM kuchukua msimamo huo ulitokana na kuwa utasaidia kukabiliana na ufisadi kwa kuondoa pesa haramu mikononi mwa matapeli wanaopora pesa za umma na kuzificha manyumbani mwao.
Wanachama kadhaa pia wameanza kutilia shaka umuhimu wa handsheki hiyo kwani kulingana nao, Bw Odinga na Rais Kenyatta hawajaonyesha nia kikamilifu ya kuwezesha marekebisho ya Katiba kufanikishwa haraka iwezekanavyo.
Ushirikiano wa Bw Odinga na Rais umeonekana kufanya usemi wake ufifie kuhusu masuala mbalimbali.
Kwa mfano, wakati chama kilipokuwa kikiendeleza juhudi za kumwadhibu Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ilifichuka Bw Odinga alijaribu kuingilia kati kumwokoa lakini hatua zake hazikufua dafu.
Vilevile, usemi wake ulitiliwa shaka zaidi kwenye uchaguzi mdogo wa Ugenya wakati Chris Karani wa ODM aliposhindwa na Bw David Ochieng wa MDG.