Usalama wa Ruto: Rigathi Gachagua ataka Kibicho achunguzwe
Na MWANGI MUIRURI
MBUNGE wa Mathira, Rigathi Gachagua amemtaka Katibu maalum katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho achunguzwe kuhusu baadhi ya amri zake kwa wadogo wake nyanjani.
Amesema kuwa Kibicho amekuwa akiwaagiza makamishna na makamanda wa vitengo vya kiusalama mashinani kutohudhuria hafla za Naibu Rais, Dkt William Ruto.
Mbunge huyo ameahidi kusukuma kuchunguzwa kwa Kibicho na kamati ya kiusalama bungeni na maandalizi ya kumfurusha nje ya baraza la mawaziri yazinduliwe.
Alimuonya Kibicho kuwa “jina lako likitua bungeni litapata wingi wa wafuasi wa Ruto na hutakuwa na bahati ya kuhepa kitanzi kwa kazi yako.”
Hata hivyo, Kibicho amekuwa akilalamika kuwa afisi ya Ruto huwa haitoi ratiba ya safari zake mashinani ili kuandaa maafisa hao wa kiusalama, hali ambayo mara kwa mara huzua hitilafu ya kimikakati.
Aidha, amekuwa akijitetea kuwa hakuna wakati wowote amekuwa akiwaagiza maafisa hao wamhujumu Dkt Ruto.
“Tunasisitiza kuwa jukumu la usalama wa hafla zake unaanza naye mwenyewe. Atupe ratiba yake na tutakuwa aliko,” akasema Kibicho.
Hata hivyo, Gachagua ambaye pia alikuwa afisa wa utawala wa kimaeneo katika serikali ya rais mstaafu Daniel Moi kabla ya kujiuzulu kujiunga na siasa; akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Kameme alisema kuwa wanaowekwa katika hatari ya kikazi ni maafisa hao ambao wanashawishika kutoheshimu Dkt Ruto.
“Ikiwa huyu Dkt Ruto ataibuka kuwa rais baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, maafisa hawa watategemea nini kutoka kwa huyu wanayeonyesha dharau akiwa Naibu wa rais?” akahoji.
Akasema: ‘Tumeshuhudia hali kadhaa ikiwemo katika Kaunti yangu ya Nyeri ambapo kumezuka uchochezi wa kiafisi kwa baadhi ya maafisa wa kiusalama nyanjani wasihudhurie hafla ya Naibu Rais. Tunataka kujua jinsi amri hizi hutolewa.”
Bw Gachagua alisema Katiba ya nchi imezima maelekezi ya maamuzi kwa masuala ya kikatiba kupokezanwa kutoka kwa wakubwa hadi kwa wadogo kupitia simu au neno la mdomo.
“Maamuzi ya aina hiyo yanafaa kuwekwa katika barua rasmi na itiwe sahihi na anayeitoa kwa manufaa ya msasa kuhusu uhalali wa amri hizo,” akasema.
Alisema kuwa Naibu Rais akitembelea eneo la hapa nchini hafanyi hivyo kama mtu binafsi bali hufanya hivyo chini ya uratibu wa hafla za kitaifa katika mikakati ya kuziandaa.
“Tunapouliza kisiri, tunaarifiwa kuwa Kibicho ndiye ametoa amri hizo. Ajue kuwa sisi tuko na uhuru bungeni wa kumumulika. Asifikirie kuwa tunanyamaza kwa upole wa uoga. Hapana; chuma chake ki motoni,” akasema.
Ni hivi majuzi Dkt Ruto akiwa katika kituo cha redio cha Kameme alisema kuwa hilo la Dkt Kibicho kudhaniwa kumhujumu kisiasa mashinani “halinijalishi kwa kuwa serikali ni kama kampuni kubwa ambayo katika kitengo cha usalama kuna wazembe, wakora na washenzi.”
“Suala hilo nitalishughulikia kimyakimya ndani ya serikali ikizingatiwa kuwa mimi ni Naibu Rais wala sio mtu mwingine ndani ya serikali,” akasema.