• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mchakato wa kujifunza na kufundisha lugha ya kigeni

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mchakato wa kujifunza na kufundisha lugha ya kigeni

Na MARY WANGARI

MADA ya mchakato wa kujifunza lugha ya kigeni pamoja na ufundishaji wa lugha ya kigeni kwa jumla ni muhimu.

Aghalabu, shughuli ya kujifunza na kufundisha lugha ya kigeni katika jamii kwa kiasi kikubwa hutegemea taasisi husika.

Hata hivyo, kuna madhumuni ya jumla jinsi tutakavyoyaainisha ifuatavyo:

i. Haja ya kutaka kuwasiliana na wenyeji wa sehemu au nchi fulani.

ii. Kwa lengo la kujiandaa kusafiri kwenda nchi nyingine kwa shughuli mbalimbali.

iii. Kwa sababu za kufanya biashara.

iv. Kwa malengo ua kukidhi vigezo vya masomo.

v. Kwa nia ya kufanya utafiti katika taaluma husika.

vi. Kwa kusudi la kupata ajira nchi za ughaibuni.

Hatua za ufundishaji

Ni vyema kwa mfundishaji yeyote yule ajihadhari na ajiepushe kumfunza mwanafunzi sarufi za lugha hiyo kwanza.

Ni sharti utamfundisha hatimaye lakini lisiwe jambo unalolipatia kipaumbele.

Utaratibu mwafaka ni kuanza na maamkizi ya kawaida. Salamu katika utamaduni wa Mwafrika ni kitu cha muhimu sana; hivyo ni jambo la busara la kufundisha salamu ili kuwezesha mwanafunzi husika kuwasiliana.

Kwa jumla, malengo ya ubidhaishaji pamoja na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni ni kama yafuatayo:

i. Ili kumwezesha mwanafunzi kumudu lugha ya Kiswahili.

ii. Ili kumfanya mwanafunzi aweze kuwasiliana na wanajamii wanaotumia lugha ya Kiswahili.

iii. Ili kumwezesha mwanafunzi kung’amua mambo fulani kama vile jinsi ya kusema jambo fulani. Kwa mfano, jinsi ya kusema anataka kwenda msalani, mbona aseme, na amweleze nani na katika mazingira gani.

iv. Ili kuwapa wanafunzi mbinu mbalimbali za kujifunza lugha ya Kiswahili. Ni muhimu kwa wanafunzi wafanye kwa vitendo ili waweze kujichukulia misamiati ya kutosha

v. Ili wanafunzi wang’amue umuhimu wa lugha wanayojifunza.

Ili kuwawezesha wanafunzi waweze kutimiza malengo haya, ni sharti mwalimu awape wanafunzi fursa ya kutafiti, kudurusu, kugundua na pia kutalii masuala anuwai kuhusu lugha; kwa mfano lugha ya Kiswahili.

 

[email protected]

Marejeo

Chiraghdin, S. & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.

You can share this post!

AFCON: Senegal imani kwa kikosi cha Kombe la Dunia

Chuma ki motoni kwa maafisa wa serikali walevi

adminleo