Michezo

Sarri aomba ruhusa atoke Chelsea upesi

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Maurizio Sarri amesema yuko tayari kabisa kuachana na Chelsea kipindi hiki cha majira ya kiangazi na kurejea Italia “baada ya msimu mgumu”.

Hii ni kufuatia uvumi kwamba mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 60 yuko njiani kujiunga na vigogo wa Italia, Juventus baada ya kukutana na wakuu wa Chelsea kuhusu hatima yake.

Tayari Juventus imetangaza kuwa na nia ya kumtwaa kocha huyo wa zamani wa Napoli kwa mkataba wa Sh700 milioni kwa mwaka kuziba nafasi ya Massimilliano Allegri.

Chelsea haikuwa na mpango wa kumfuta kazi kocha huyo, hasa baada ya kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Europa League kwa mabao 4-1 dhidi ya Arsenal majuzi jijini Baku.

Mbali na ushindi huo, Sarri ambaye amekuwa Stamford Bridge kwa kipindi cha mwaka mmoja vilevile aliisaidia klabu hiyo ya ligi kuu ya Uingereza kumaliza msimu katika nafasi ya tatu nyuma ya Liverpool na mabingwa, Manchester City.

Kadhalika Chelsea ilizifunga Liverpool na Tottenham Hotspur na kusonga mbele hadi hatua ya fainali ya Carabao Cup ambapo ilishindwa na Manchester City kupitia kwa mikwaju ya penalti.

Imesemekana ni Sarri mwenyewe aliyeamua kuondoka baada ya kumjulisha mapema Mkurugenzi wa Michezo wa klabu ya Chelsea, Marina Granovskaia kwamba angependa kurejea nyumbani Italia kwa lengo la kuwa karibu na familia yake.

Mashabiki walalama

Sarri alikumbana na malalamiko tele kutoka kwa mashabiki wa Chelsea wakati wote wa msimu, akifokewa kutokana na mbinu zake za kubadilisha kikosi kilichokuwa kimetulia.

“Kwa sisi wananchi wa Italia, nyumbani ni muhimu. Kawaida tunapokuwa mbali na nyumbani tinahisi kukosa kitu fulani muhimu. Nimekuwa mbali na marafiki pamoja na wazazi wangu,” aliongeza.

“Nitakaporejea kwetu Tuscany nitaonekana kama mgeni. Tangu niondoke miezi 12 iliyopita, nimewahi kulala huko mara 30 pekee,” alisema.

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu wa bwanyenye Roman Abramovich anayemilili Chelsea, jicho lao sasa ni kwa makocha watano ambao huenda mmoja wao akapewa nafasi ya kujaza nafasi ya Sarri.

Katika orodha ya tajiri huyo wa Chelsea kuna Mauricio Pochettino, Frank Lampard, Patrick Vieira, Diego Semeone na Nuno Espirito Santo.