• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
Nyota wa Cranes wazidi kujaajaa kambi ya mazoezi

Nyota wa Cranes wazidi kujaajaa kambi ya mazoezi

Na JOHN ASHIHUNDU

MSHAMBULIAJI matata, Emmanuel Arnold Okwi, kipa Robert Ondongkara wa Adama City FC ya Ethiopia, mlinzi hodari Ronald Brian Mukiibi wa Ostersunds na Nicholas Wakiro Wadada wa klabu ya Azam ya Tanzania ni miongoni mwa wachezaji walijiunga na kambi ya timu cha Uganda Cranes nchini Abu Dhabi na kufanya idadi ya kikosi hicho kufika 25.

Cranes ambayo inajiandaa kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) imepiga kambi katika Park Rotana Hotel kwa mazoezi ya pamoja kabla ya kuelekea Misri kwa michuano hiyo ya Afcon itakayoanza Juni 21 na kumalizika Julai 19.

Wadada aliingia kambini baada ya majuzi kuisaidia Azam kuibwaga Lipuli katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania. Kadhalika, aliyekuwa mchezaji wa AFC Leopards ya Kenya, Allan Kateregga ambaye sasa yuko na Maritzburg ya Afrika Kusini amejiunga na wenzake.

Kwa mujibu wa habari kutoka kwa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Ahmed Hussein, Charles Lukwago, naye alitarajiwa kujiunga na timu hiyo baada ya kuchezea kikosi cha pili cha Cranes katika michuano ya COSAFA ambapo walitolewa na Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti.

Mukiibi amejiunga na wenzake Abdu Lumala na Alexis Bbakka ambao pia husakatia nchini Sweden. Ni kiungo Micahel Azira pekee ambaye alikuwa akisubiriwa kufikia jana asubuhi.

Kuwasili kwa Ondongkara kuimefanaya idadi ya makipa kambini humo kufika watatu pamoja na kipa chaguo la kwanza Denis Onyango na Jamal Salim Magoola. Idara ya kiufundi inachunguza kwa makini kiwango cha kila mchezaji kambini wakati timu hiyo itarajiwa kucheza mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Turkmenistan na Ivory Coast Juni 9 na Juni 15 mtawaliwa.

Baada ya mechi hizo, kikosi hicho kitapunguzwa na kubakia wachezaji 23 ambao majina yao yatatumwa Cairo kuwakilisha Uganda katika michuano ya Afcon. Nchini Misri, Uganda wamo katika Kundi A pamoja na wenyeji Misri, Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kikosi

Kikosi cha Uganda kilicho nchini Abu Dhabi ni: Makipa: Denis Onyango (Mamelodi Sundowns, Afrika Kusini), Jamal Salim (Al Hilal-Sudan) na Robert Ondongkara (Adama City, Ethiopia).

Walinzi: Nico Wakiro Wadada (Azam, Tanzania), Brian Ronald Mukiibi (Ostersunds, Uswidi), Murushid Jjuuko (Simba, Tanzania), Bevis Mugabi (Yeovil Town, Uingereza), Isaac Muleme (FK Viktoria Zizkov, Jamhuri ya Czech), Hassan Wasswa Mawanda (hana klabu), Joseph Ochaya (TP Mazembe, DR Congo), Timothy Denis Awanyi (KCCA FC, Uganda), Godfrey Walusimbi (hana klabu).

Viungo ni: Allan “Dancing Rasta” Kateregga (Maritzburg, Afrika Kusini), William Kizito Luwagga (Shakhter Karagandy, Kazahstan), Khalid Aucho (Church Hill Brothers, India), Faruku Miya (HNK Gorica, Croatia), Tadeo Lwanga (Vipers SC-Uganda), Kirizestom Ntambi- Coffee FC, Ethiopia), Moses Waiswa (Vipers SC, Uganda) na Sadam Juma (KCCA FC-Uganda).

Washambuliaji: Alexis Bbakka (Carlstad United, Sweden), Patrick Henry Kaddu (KCCA FC, Uganda), Derrick Nsibambi (Smouha, Misri), Allan Kyambadde (KCCA FC Uganda), Emmanuel Arnold Okwi (Simba, Tanzania).

You can share this post!

Zogo la Malala, Oparanya kuhusu Mumias lachacha

Mahangaiko ya miaka 12 akingoja mumewe

adminleo