• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
DINI: Maisha ni kuingia na kutoka, acha sifa za kuigwa ukiondoka duniani

DINI: Maisha ni kuingia na kutoka, acha sifa za kuigwa ukiondoka duniani

Na FAUSTIN KAMUGISHA

KUINGIA na kutoka ni mtihani.

Kuna kitendawili kisemacho: aliingia kwenye nyama akatoka bila kula. Jibu ni kisu.

Mwanafunzi akiingia shuleni kujifunza na kutoka bila ushindi ametoka kama kisu kwenye nyama. Timu ya mpira ikiingia uwanjani na kutoka ikiwa imefungwa bila kufunga ni kama kisu kuingia kwenye nyama na kutoka bila kula.

Tunahitaji hekima kujua namna ya kuingia na kutoka. Suleimani au Solomoni alisali: “Ee Bwana…sijui inipasavyo kutoka wala kuingia…Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima” (1 Wafalme 3: 7-9).

Maisha ni kuingia na kutoka.

Tunaingia shuleni na kutoka. Tunaingia kazini na kutoka.

Tunaingia Kanisani na kutoka.

Tunaingia nyumbani na kutoka.

Tunaingia hotelini na kutoka.

Tunaingia kiwanjani na kutoka.

Tunaingia dukani na kutoka.

Tunaingia shambani na kutoka.

Tunaingia duniani na kutoka.

Unapotoka nyumbani toka umesali, muombe Mungu aratibu siku yako.

Unapotoka nyumbani toka na malengo, toka na ratiba ya siku, toka na mpango wa kazi, toka na mpango wa siku, toka na ndoto, toka na matumaini na toka na imani ya kufanikiwa.

Unapotoka nyumbani toka na mkakati wa kuboresha maisha, unapotoka nyumbani toka na moyo wa kucharika. Unapotoka nyumbani toka na mpango wa mambo unayotaka kufanya. Unapotoka nyumbani toka na ramani.

Kama hujui unapokwenda utafikaje?

Hakuna mahali kama nyumbani. Unapotoka nyumbani bakisha sehemu ya moyo wako nyumbani.

Kuna methali isemayo, “Mtu mwenye busara na kobe husafiri lakini hawaiachi nyumba yao.”

Unapoingia kwenye nyumba yako, ingia kwa upendo.

“Ni rahisi kuwapenda watu walio mbali. Si rahisi kila mara kuwapenda wale walio karibu na sisi. Ni rahisi zaidi kutoa kikombe cha mchele kumaliza njaa kuliko kumaliza upweke na mateso ya mtu ambaye hapendwi nyumbani kwetu. Leta upendo nyumbani kwako maana hapa ndipo upendo kati yetu hauna budi kuanzia,” alisema Mama Teresa wa Calcutta; mshindi wa Tuzo ya Nobel mwaka 1979 (1910 – 1997).

Vazi la wema

Unapoingia nyumbani kwako ingia umevaa vazi la wema.

“Ni vizuri zaidi kuwa mwema nyumbani kuliko kwenda mbali kuunguza ubani.” Ni methali ya Kichina.

“Mbali na nyumbani wanatazama nguo zako. Nyumbani wanatazama kilicho chini ya nguo.” Ni methali ya Kichina. Kinachopaswa kuwa chini ya nguo ni wema.

Unapoingia nyumbani ingia kwa moyo wa ukarimu.

“Kama nyumbani hupokei wageni ukienda nchi za nje hutakuwa na mwenyeji.” Ni methali ya Kichina.

Kwenye nyumba kuna ukarimu.

“Hatari kubwa katika maisha ya familia, katika jamii ambayo miungu yake ni anasa, faraja na kujitegemea ipo katika ukweli kuwa hufunga mioyo yao na kuwa wachoyo,” alisema Mtakatifu Yohane Paulo 11.

Unapoingia nyumbani ingia kwa moyo wa shukrani. Achana na moyo wa kutothamini.

Achana na moyo wa kutoshukuru. Achana na moyo wa kutokutia moyo. Unaowakuta nyumbani wathamini, washukuru, watie moyo.

Mtoto anapoingia duniani analia, waliomzunguka wazazi, ndugu na jamaa wanafurahi.

Mtu anapotoka duniani, waliomzunguka, ndugu na jamaa wanalia, yeye kama ameishi vizuri roho yake inafurahi.

Patrick Henry alipokuwa kwenye kitanda cha mauti aliwaita watoto wake wakiwa wamemzunguka aliwaambia, “Niko karibu kuwaachia mali yangu ya duniani.

Kuna jambo ambalo nataka kuwaachia, kwa kulitaja imani kwa Mungu.

Kama ningewaachia hiyo tu bila kitu kingine, mngekuwa matajiri kweli. Kama ningewaachia vitu vingine vyote bila hicho, mngekuwa maskini kweli.”

Utakapotoka duniani acha mfano wa kuigwa, rithisha mikoba ya imani na mafanikio.

Watoto wako warithishe biashara na miradi.

You can share this post!

Eden Hazard kula mshahara wa juu kuliko wote Real Madrid,...

Kundi jipya laibuka Mlimani

adminleo