Habari

Kundi jipya laibuka Mlimani

June 9th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

KUNDI jipya la kisiasa limeibuka katika ukanda wa Mlima Kenya huku makundi ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ yakiendelea kuzozana kuhusu siasa za 2022 na anayefaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Kundi hilo, linalojiita ‘Team Hema’ linahusishwa na mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria ambaye ametangaza azma ya kuwania urais 2022.

Kinyume na makundi ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ ambayo yanapinga au kuunga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022, kundi hilo linadai kwamba lengo lake ni kujali maslahi ya wakazi.

Tayari, kundi hilo limeanza kupata ufuasi katika kaunti zote 10 za eneo la Mlima Kenya, ngome ya Rais Kenyatta.

Wanachama wake wengi ni viongozi ambao hawajatangaza rasmi misimamo yao ya kisiasa.

Katika Kaunti ya Kiambu, anakotoka Bw Kuria, kundi hilo linahusishwa na wanachama wanane, wakiwemo Seneta Kimani Wamatangi, wabunge Wanjiku Kibe (Gatundu Kaskazini), Francis Waititu (Juja), Wainaina Jungle (Thika Mjini), Jude Jomo (Kiambu), Jonah Mburu (Lari) na Seneta Maalumu Isaac Mwaura.

Katika Kaunti ya Nakuru, kundi hilo lina wanachama watatu, wakiwemo wabunge Martha Wangari (Gilgil), Samuel Gachobe (Subukia) na Kimani Kuria (Molo).

Katika Kaunti ya Laikipia, wanachama wake ni Seneta Johh Kinyua na mbunge Patrick Mariru (Laikipia Magharibi).

Katika Kaunti ya Nyeri, wanachama wake ni wabunge Kanini Kega (Kieni), Gichuki Mugambi (Othaya) na Seneta Ephraim Maina.

Kaunti nyingine ambazo kundi hilo linatajwa kuwa na uungwaji mkono ni Embu, Meru, Tharaka Nithi, Murang’a na Kirinyaga.

Kauli ya Bw Kuria kwamba atawania urais kwa mara ya kwanza, ilipokelewa kwa hisia mseto.

Kuzaa matunda

Kulingana na baadhi ya wachanganuzi, huenda juhudi zake zikaanza kuzaa matunda, kwani ameanza kukumbatiwa kama “Njaamba ya Ruuriri” yaani Shujaa wa Jamii.

Bw Kuria amekuwa akihudhuria hafla nyingi za kuchangisha fedha katika maeneo mbalimbali nchini katika azma inayoonekana kama ya kujipigia debe.

“Nitawania urais ili kuwasaidia Wakenya kupata ajira. Nitahakikisha kuwa wawekezaji wadogo wadogo pia wanapata pesa, kwani hilo ndilo litakalowawezesha kujiinua kiuchumi,” alisema Bw Kuria.

Awali, Bw Kuria alikuwa katika kundi la ‘Tanga Tanga’ akimpigia debe Dkt Ruto kuwania urais, lakini akajiondoa akisisitiza kwamba atalainisha baadhi ya mambo ambayo serikali ya Jubilee imeshindwa kushughulikia.

Hata hivyo, azma yake imekuwa ikipingwa na baadhi ya wanachama wa makundi hayo mawili, wakisisitiza kuwa hana uwezo wowote wa kupata kura ikilinganishwa na Dkt Ruto.

“Tunataka kummweleza Dkt Ruto kuwa asibabaishwe na baadhi ya viongozi. Eneo la Mlima Kenya limetangaza wazi kuwa litamuunga mkono atakapowania urais 2022,” akasema Gavana Ferdinand Waititu wa Kiambu, ambaye ni mmoja wa wakosoaji wakuu wa Bw Kuria.

Kuibuka kwa makundi mbalimbali kunatokana na kimya cha Rais Kenyatta kuhusu mrithi wake katika eneo hilo.