Barua kwa Wakenya: Amkeni mlete mageuzi
Na WANDERI KAMAU
MNAMO Desemba 1795, aliyekuwa mtawala wa Ufaransa mwenye uwezo mkubwa sana wa kijeshi, Napoleon Bonaparte, aliandika mojawapo ya barua maafuru sana za kimapenzi katika historia.
Alimwandikia Bi Josephine de Beauharnais, mwanamke ambaye aliibukia kumpenda sana, licha ya kumzidi umri kwa miaka sita.
Napoleon alionekana kutobabaishwa na tofauti hiyo, lakini alizidiwa na mapenzi aliyokuwa nayo kwake.
Akaandika: “Mpenzi wangu Josephine, unajua vile huwa unaifurahisha roho yangu? Huwa naanza kuhisi penzi lako kabla ya adhuhuri…natamani kukutana nawe. Hadi tutakapokutana tena, nakubusu mara elfu moja mpenzi wangu.”
Alimwandikia barua nyingi. Nyingi sana. Hatimaye alifanikiwa kuiteka roho yake na kumwoa, ingawa walitengana baadaye.
Vivyo hivyo, penzi hilo aliloonyesha Bonaparte kwa Josephine, ndilo nililo nalo kwa Wakenya wenzangu.
Maoni haya ni barua maalum kwao, kuwafahamisha kuwa Kenya imetekwa. Wao ni mahabusu wa kimfumo ambapo lazima wajikomboe.
Tu mahabusu wa ‘falme’ mbili kuu za kisiasa, ambazo lengo lake ni kuhakikisha zinaendeleza ukiritimba wao dhidi ya wananchi.
Lengo kuu la ‘abrakadabra’ za kisiasa zinazoendeshwa na familia za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ni kuendeleza udhibiti wao wa siasa za Kenya kupitia ushirikiano maalum uitwao “handisheki.”
Je, manufaa ya mwafaka huo yamekuwa yapi kwa mamilioni ya Wakenya? Katika eneo la Mlima Kenya, ambako ndiko ngome ya Rais Kenyatta, wakazi wanalia. Kilio chao kinafanana na kile cha Wayahudi walipolengwa na Adolf Hitler wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Kilimo, ambacho ndicho kitegauchumi kikuu cha wakazi, kimesambaratika. Ahadi zote walizopewa wakati wa kampeni zimegeuka hewa. Baadhi ya wakazi hata wamekaidi miiko na kung’oa mazao yao kama majanichai. Wakulima wa kahawa, miraa na pareto wametengwa. Kuna Kilio Kikuu Mlima Kenya.
Katika eneo la Nyanza, ambako ndiko ngome kuu ya Bw Odinga, hali ni kama iyo hiyo. Vilio vimegeuka chakula kwa maelfu ya wakazi waliojitoa mhanga ‘kumtetea’ Odinga kwa kila hali. Mamia walijeruhiwa, kuuawa na hata kufurushwa makwao. Amewasaliti kwa ‘kuungana’ na Rais Kenyatta, aliyechorwa kama ‘hasimu’ wa kisiasa wa Bw Odinga. Walisahau kuwa wao ni marafiki.
Wote waliwahadaa wafuasi wao.
Kilicho muhimu sasa kwa Wakenya ni kujikomboa. Amkeni! Amkeni kujitanzua kutokana na hadaa hii ya kisiasa. Amkeni kutetea mustakabali wa vizazi vyenu. Amkeni kuwachagua viongozi watakaojali maslahi yenu. Amkeni!
Nasema haya kwa mapenzi ya kweli; mapenzi aliyoonyesha Bonaparte kwa mpenziwe, Josephine au mapenzi aonyeshayo mama kwa mtoto wake.
Hata hivyo, taswira ya kisiasa inayoendelea kujengwa ielekeapo 2022 inaashiria wazi kuwa njama kuu iliyopo ni kwa familia hizo mbili kutumia ushawishi wake kuwafadhili viongozi watakaolinda maslahi yao. Hesabu ya Mkenya haipo!
Wakenya wenzangu, 2022 ni nafasi ya pekee ya kuzikaidi familia hizi mbili na kuanza mapambazuko mapya ya kisiasa. Amkeni!