JAMVI: Musyoka aendelea kupata upinzani ngomeni, lakini adai yuko ngangari
Na BENSON MATHEKA
Kiongozi wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka anaendelea kutengwa kisiasa katika ngome yake huku waliokuwa wandani wake waliogeuka mahasimu wakidai hawezi kuwa rais wa Kenya.
Vita vya kisiasa dhidi ya Bw Musyoka vimezidi baadhi ya viongozi wa Ukambani wakimtaka asahau ndoto yake ya kuwa rais wakimlaumu kwa kushindwa kuongoza na kutetea jamii yake licha ya kumuunga mkono kwa miaka mingi.
Kulingana na aliyekuwa Seneta wa Kitui David Musila, jamii ya Wakamba inafaa kumtafuta msemaji mwingine wa kuwakilisha maslahi yake katika siasa za kitaifa badala ya kumtegemea Bw Musyoka.
Bw Musila ambaye ni mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika sana eneo la Ukambani anahisi kwamba Bw Musyoka hajali jamii yake na haitanufaika ikiendelea kumuunga mkono kugombea urais.
Anasema kwamba badala ya kumuunga mkono Bw Musyoka, jamii ya Wakamba inafaa kuunga mgombeaji mwingine aliye na nafasi ya kushinda urais ili ipate nafasi ya kuwa serikalini.
“Mara tatu tumejaribu kupata urais kwa kuunga mmoja wetu na tumekuwa tukishindwa. Wakati umefika tuweze kubadilisha mbinu. Nafasi tuliyonayo ni kuketi kama jamii na kukubaliana kumuunga aliye na nafasi ya kushinda ili tuweze kupata nafasi kubwa katika serikali ijayo. Hivi ndivyo tulipaswa kufanya kwenye uchaguzi mkuu uliopita lakini tulipotoshwa,” alisema Bw Musila akiongea na kituo kimoja cha redio kinachotangaza kwa lugha ya mama.
Bw Musyoka amegombea urais mara moja na kuwa mgombea mwenza mara mbili. Aligombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 akitumia tiketi ya chama cha ODM- Kenya kwenye uchaguzi uliofuatiwa na ghasia na akateuliwa makamu wa rais katika serikali ya muungano.
Kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017 alikuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika miungano ya Cord na NASA mtawalia ambapo walishindwa na Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto.
Bw Musila ambaye ni mmoja wa waliokuwa wandani wa miaka mingi wa Bw Musyoka kabla ya kutofautiana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 anasema Bw Musyoka hana uwezo wa kushinda uchaguzi wa urais.
Kabla ya wawili hao kutofautiana, Musila alikuwa mmoja wa viongozi wa chama cha Wiper waliokuwa wakimmiminia sifa Bw Musyoka wakimpigia debe kuwa rais
Wadadisi wa siasa za Ukambani wanasema mizizi ya uhasama kati ya wawili hao wanaotoka eneo la Mwingi Kaunti ya Kitui imejikita mizizi kwa miaka mingi.
“Ukisoma kitabu cha maisha ya Bw Musila, Seasons of Hope, utagundua kwamba tangu akiwa afisa wa utawala chini ya serikali ya Kanu na hata baada ya kujiunga na siasa, uhusiano wake na Bw Musyoka haukuwa mzuri. Ushirikiano wao baada ya vyama vingi vya kisiasa kuanzishwa nchini ulitokana upepo wa kisiasa uliokuwa ukivuma nchini,” asema Bw Philip Wambua, mchanganuzi wa kisiasa.
Akinukuu kitabu cha Bw Musila, Bw Wambua anasema uhusiano wao wa kisiasa ulijawa na panda shuka na usaliti wa kisiasa.
Bw Musila anamlaumu Bw Musyoka kwa kuzima viongozi wa Ukambani wanaochipuka ili aendelee kuwa msemaji wa jamii na kuinyima nafasi ya kuunda miungano ya kisiasa inayoweza kuifaidi.
Magavana watatu wa Kaunti tatu za Ukambani Alfred Mutua wa Machakos, Profesa Kivutha Kibwana wa Makueni na Charity Ngilu wa Kitui wamekuwa wakimpiga vita Bw Musyoka wakimlaumu kwa kuendeleza siasa za kupalilia umasikini katika jamii.
Wadadisi wa siasa wanasema umoja wa magavana hao unaweza kuwa pigo kwa maisha ya kisiasa ya Bw Musyoka iwapo hatacheza siasa zake vyema.
Kulingana na Dkt Mutua, wakati umefika wa jamii ya Wakamba kubadilisha jinsi inavyocheza siasa ili kujinasua kutoka utando wa umasikini, kauli ambayo Bw Musila anaunga mkono.
Bw Wambua anasema kwamba kuendelea kutengwa na wanasiasa wenye ushawishi eneo la Ukambani kunaweza kuwa pigo kwa maisha ya kisiasa ya Bw Musyoka.
Hata hivyo, wadadisi wanasema itategemea mwelekeo wa kisiasa ambao Bw Musyoka atachukua siku zijazo.
Aliyekuwa seneta wa Machakos Johnson Muthama anasema kwamba wanaodhani wanaweza kufifisha umaarufu wa Bw Musyoka Ukambani wanaota mchana.
“Hakuna mtu anayeweza kushindana na kiongozi aliyetawazwa rasmi na wazee kuwa msemaji wa jamii yao. Mzee wa kijiji hawezi kushindana na kiongozi wa hadhi ya Musyoka. Wacha wanaopanga mambo yao waendelee, wakati ukifika, watajua walijidanganya,” asema Bw Muthama.
Kulingana na mwandani mmoja wa Bw Musyoka ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa sababu za kibinafsi, wanaompiga vita Bw Musyoka wamelipwa na mahasimu wake kufanya hivyo na wengine wanataka kumshinikiza afanye maamuzi ya kuwafaa binafsi.
“Hawa wanaopiga kelele watanyamaza uchaguzi mkuu ukikaribia watakapokosa pa kushika. Waliowalipa tunawajua na Bw Musyoka sio mtu wa kufuata maamuzi ya watu kiholela wanavyofikiria. Umaarufu wao utabainika uchaguzi ukikaribia ikiwa upo,” aeleza mwanasiasa huyo.
Anasema wanachosahau ni kwamba Bw Musyoka anacheza siasa za kitaifa wakiendeleza siasa za vijijini. “Upepo wa kisiasa nchini huwa unavuma kuanzia ngazi ya kitaifa na sio vijijini. Bw Musyoka yuko imara na watakosa cha kusema akiwa rais wa tano wa Kenya,” alieleza.
Wadadisi wanasema hata kama Bw Musyoka ana ukuruba wa kisiasa na viongozi wa kitaifa, huenda akapata pigo ngome yake ya kisiasa ikiendelea kugawanyika.