Boca Junior FC inavyokuza vipaji mashinani
Na JOHN KIMWERE
BOCA Junior FC ni timu ya wachezaji chipukizi inayoshiriki mechi za Kundi A kufukuzia ubingwa wa Ligi ya Kaunti ya FKF, Tawi la Nairobi Magharibi msimu huu.
Kikosi hicho ambacho hunolewa na kocha wa timu ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), George Makambi kimejikuta njiapanda mbele ya wapinzani wakuu ikiwemo MAA FC, South B United Academy, South C United FC na Raira University FC bila kuweka katika kaburi la sahau FISA Academy.
Timu hizo zimekuwa katika mstari wa kwanza kushusha ushindani mkali kufukuzia nafasi ya kupandishwa ngazi msimu ujao. FISA Academy ya kocha, Hannington Oduor imeonekana kurejea kivingine licha ya kukosekana kwenye mechi za FKF tangu mwaka 2016.
”Boca Junior iliasisiwa mwaka 2015 ili kukuza wachezaji chipukizi mashinani pia kushiriki kampeni za kufukuzia tiketi ya kufuzu kushiriki Ligi Kuu ya KPL miaka ijayo,” alisema kocha wake na kuongeza kwamba pia walikusudia kuwa wakipandisha ngazi baadhi ya wachezaji wazuri kuchezea timu ya KNH na Ushuru FC inayoshiriki Supa Ligi ya Taifa (NSL).
Timu hiyo ilianzishwa kwa ushirikiano wake kocha huyo na mwenzake Ken Kenyatta ambaye hufunza timu ya Uhsuru FC ambayo hushiriki ngarambe ya Supa Ligi ya Taifa (NSL).
Kocha George Makambi anasema bado hawajapata mfadhili mbali wao hutegemea fedha kiasi kutoka mifuko yao kufadhili shughulio za kikosi hicho.
Aidha anasema licha ya vijana hao kushindwa kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao ana imani wanayo nafasi ya kufanya kweli.
”Msimu ujao tutajitahidi kwa udi na uvumba kuhakikisha tumefaulu kumaliza kati ya nafasi mbili za kwanza ili kujiweka pazuri kubahatika kubahatisha kuwa miongoni mwa timu za kupandishwa ngazi kucheza mechi za kinyang’anyiro cha Nairobi West Regional League (NWRL),” alisema.
Kwa mtazamo wake kikosi hicho kinafanya vizuri kwenye kampeni za kipute Ligi ya kaunti lakini anakiri kuwa kilishuhudia upinzani mkali uliyozima juhudi za kukiwezesha kumaliza nafasi bora.
Aliongeza kwamba baada ya kufanya uchunguzi wake aligundua kuwa hakuna ligi rahisi kote nchini maana timu zote zimeonekana kujipanga vizuri kupigania tiketi za kusonga mbele msimu ujao.
Kama kocha anashauri wachezaji wanaokuja kutia bidii kwenye harakati za kupalilia talanta zao maana soka imegeuka ajira kama zingine kwa kuzingatia imebadilisha maisha ya wengi duniani.
Kundi hilo pia linajumuisha Re Union kati ya timu kongwe nchini inayong’ang’a kiume kufuata wenzao Gor Mahia FC na AFC Leopards.