Timu 18 zapigania ubingwa mashindano ya karate
Na LAWRENCE ONGARO
MASHINDANO ya karate ya Gorjuru Championship, yaliendelea mwishoni mwa wiki katika hoteli ya Utalii jijini Nairobi. Mashindano hayo yalijumuisha wanakarate wa umri wa chini hadi watu wazima.
“Mashindano hayo yalikuwa katika tabaka mbili ambapo ni (Kata na Kumite). Nimeridhika na wanakarate hao kwa sababu wameonyesha vipaji vya hali ya juu,” alisema mkuu wa mchezo huo Bw Kocha Kogi ambaye anayemiliki Black Belt 5th Dan.
Katika fainali ya kiwango cha watu wazima kwa wasichana mchezo wa Kata, Judith Mbula, aliibuka wa kwanza na kushinda dhahabu. Olivia Gatwiri alipata fedha katika nafasi ya pili, huku Carolyne Karanja akipata medali ya Shaba.
Katika mchezo wa kumite kwa wasichana Rose Wanjiku alishinda dhahabu Stela Musyoki, alipokea fedha, huku Mary Wanjiku akipata shaba.
Katika upande wa wanaume, mchezo wa kata, Julius Muya alipokea dhahabu . Naye Michael Ngaruiya aliridhika na fedha, huku Stephen Romario akipata Shaba.
Katika mchezo wa kumite kwa wanaume Collins Orieno alishinda dhahabu, Denis Ngamau alipata fedha, naye John Otieno alipokea Shaba.
Katika mchezo wa kata kwa wasichana wa miaka 9-11 Janet Dayana alipokea dhahabu, Susan kalondu aliridhika na fedha, halafu Joy kabisa alipata Shaba.
Katika mchezo wa Cadetes kwa wavulana wa miaka 16-17 Charles Nduati alipata dhahabu, Denis Ngamau alipokea fedha,huku Devid Muchoki alipata Shaba.
Mchezo wa kumite kwa wasichana wa miaka 6-8, Angela Wambui alipata dhahabu, Aizelene Njambi aliridhika na medali ya fedha, naye Sarah Mbuli alijishindia Shaba.
Kulingana na kocha huyo timu 18 zilishiriki kwenye mashindano hayo yaliyohudhuriwa na mashabiki wengi kutoka mitaa ya Mathare na Kariobangi.
Baadhi ya vilabu vilivyowakilishwa kwenye mchezo huo ni kutoka jijini Nairobi, Mombasa, Nakuru, Kisumu, Malindi Nyeri na Murang’a.
“Tutazidi kuwapa motisha vijana wachanga ili wazidi kujizatiti ili kuinua ujuzi wao zaidi katika mchezo huo wa karate,” alisema Kocha Kogi.
Alitoa mwito kwa wazazi popote walipo kuwapa wana wao nafasi ya kucheza karate kwa sababu ni mchezo unaodumisha nidhamu ya hali ya juu,” alisema Kogi.